Mbwambo:  Miaka mitatu inatutosha kumpa shahada mwanafunzi wa sheria  

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Iringa, Andrew Mbwambo

Iringa. Katika hafla ya kusherehekea miaka 25 ya Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Iringa, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Andrew Mbwambo amesema chuo hiko kitaendelea kutoa shahada ya sheria kwa miaka mitatu kwasababu inatosha ‘kumpika’ mwanafunzi.

Hayo ameyasema leo Jumatatu Julai 3, 2023, huku baadhi ya vyuo hufundisha kozi hiyo kwa miaka mine.

“Sisi hapa tunafundisha kwa miaka mitatu bila kupunguza chochote huku ikiongezwa kusoma kwa vitendo zaidi,”amesema.

 Mbwambo amesema siri ya chuo hicho ni ufundishaji na kuwaandaa wanafunzi wake kwa kozi ya sheria kwa muda wa miaka mitatu, tofauti na vyuo vingine ambavyo huwahitaji wanafunzi kusoma kwa miaka minne.

"Leo mafanikio yetu katika Kitivo cha Sheria, tumekuwa tukiendeleza utamaduni wa kufundisha wanasheria bora kwa zaidi ya miaka 25," amesema Mbwambo.

Mkuu wa Kitivo cha sheria katika chuo hicho, Halima Miigo amesema ni jukumu la wanafunzi kusoma kwa bidi na kufanyia kazi kwa vitendo yote wanayosoma darasani ili kuleta tija katika tasnia ya sheria.

Akizungumza na Mwananchi Digital, mmoja ya wanafunzi wa kozi hiyo, Johanson Omary amesema miaka mitatu wanayosoma chuoni hapo inawatosha kwasababu ya uwepo wa vitendo katika masomo hgayo.

"Miaka mitatu ni muda mfupi sana kwa wanafunzi kupata elimu kamili ya sheria. Lakini kwa chuo chetu tumekuwa tukifundishwa mambo yote kwa muda huo na hakuna kinachopungua," amesema.