MCC yaichagua Tanzania kupata ruzuku
Muktasari:
- Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle amesema kutokana na Tanzania kufanya vizuri katika ukuzaji wa demokrasia ya vyama vingi, Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC), litaipa ruzuku.
Dar es Salaam. Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC), limechagua Tanzania kupata ruzuku ya maandalizi ya programu ya awali itakayosaidia kufikia malengo ya uchumi na mageuzi.
Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle amesema uamuzi huo umetokana na Tanzania kufanya vizuri katika demokrasia ya vyama vingi ya maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi mpya.
Mwaka 2016, Bodi ya MCC ilisitisha mkataba wa awamu ya pili wa kutoa zaidi ya Dola milioni 700 za Marekani (Sh1.4 trilioni) kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za umeme.
Uamuzi huo wa Bodi ya MCC iliyoketi Desemba 2015 ulitokana na kitendo cha kurudia uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani bila kushirikisha wadau na utekelezaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Leo Ijumaa, Desemba 22, 2023 katika salamu zake za sikukuu za mwisho wa mwaka, Balozi Battle amesema amefurahishwa na falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imekuwa nguzo za demokrasia za vyama vingi nchini Tanzania.
Tangu aingie madarakani Machi, 2021, Rais Samia amekuwa muumini wa falsafa za 4R yenye maana ya maridhiano (Reconciliation), mabadiliko (Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya (Rebuilding).
Kwa nyakati tofauti Rais Samia amekuwa pia akiwasisitizia wasaidizi na watendaji wake wa Serikali na CCM kuzisimamia 4R katika utekelezaji wa majukumu yao, akisema ndiyo mwelekeo wa kujenga Taifa lenye umoja na mshikamano.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Balozi Battle amesema, “ninawahimiza timu yetu ya ubalozi kufanya kazi kwa kuzingatia falsafa hii kuitia moyo Tanzania ichukue hatua muhimu, stahiki na zenye maana kuelekea mageuzi ya kweli ya kidemokrasia.
“Ili kujenga jamii salama, familia zenye afya, kufikia mustakabali bora kwa vijana wa Tanzania, ni muhimu kuendelea kupanua nafasi ya ushiriki wa wananchi ambao ndio hazina na rasilimali kubwa zaidi ya nchi hii na tunajivunia kushirikiana nao kuunga mkono mageuzi makubwa ya Tanzania,” amesema Balozi Battle.
Amesema kuelekea kumaliza mwaka 2023, Marekani kupitia MCC imeichagua Tanzania kupata ruzuku itakayosaidia Taifa hili wakati likijiandaa na uwekezaji mkubwa zaidi na uwezekano wa makubaliano kamili na MCC (MCC compact).
“Ni nchi chache duniani zinaweka kipaumbele katika suala la amani na utulivu kama sehemu ya tunu zake kuu, kama wanafanya Watanzania, tunashukuru kwa ushirikiano wetu wa kijeshi unaodhihirika kupitia mafunzo ya pamoja ya kubadilishana ujuzi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
“Wema na ukarimu wa Tanzania unatugusa sisi sote hapa ubalozini, unatupa hamasa ya kutekeleza programu za kimkakati na zenye ufanisi zitakazoimarisha urafiki wa muda mrefu baina ya mataifa yetu kwa siku nyingi zijazo,” amesema Balozi Battle.
Balozi Battle ameongeza kuwa biashara na uwekezaji kati ya Marekani na Tanzania ni miongoni mwa maeneo ya kipaumbele chake kwa mwaka 2024 kutokana na mkutano wa kihistoria kati ya Rais Samia na makamu wa rais wa nchi yake, Kamala Harris aliyetembelea Tanzania Machi mwaka huu.
“Tulijizatiti na kukamilisha majadilino ya kibiashara na wenzetu Watanzania, hii ni ahadi na azma ya Serikali zetu kuboresha biashara na uwekezaji wa pande zote mbili, mazingira ya kufanya biashara kupitia teknolojia, uwazi na mageuzi ya kikanuni na kisheria,” amesema Balozi Battle.