Mchengerwa kukutana na makatibu muhtasi nchini

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa anatarajiwa kufungua mkutano wa nane wa mwaka wa Chama cha Makatibu Muhtasi nchini (Tapsea) kesho Ijumaa Mei 21, 2021 jijini Arusha.

Arusha. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa anatarajiwa kufungua mkutano wa nane wa mwaka wa Chama cha Makatibu Muhtasi nchini (Tapsea) kesho Ijumaa Mei 21, 2021 jijini Arusha.

Mwenyekiti wa Tapsea, Zuhura Maganga amesema hayo leo Alhamisi Mei 20,2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari kuwa zaidi wa wanachama 2,900 wameshawasili kushiriki mkutano huo wa kitaaluma.

"Mkutano huu ni kwa mujibu wa katiba yetu kwa ajili ya kujadili mambo yanayohusu kada ya makatibu muhtasi  ambao wanachama wake wanatoka taasisi za serikali, mashirika ya umma na binafsi," amesema Zuhura.

Amesema mkutano huo wa siku mbili, makatibu makhususi watajifunza mada mbalimbali zitakazowasilishwa na wakufunzi wabobezi kutoka vyuo vya Serikali ili kuwanoa wanachama wake kufanya kazi katika mazingira ya kisasa.

Mwenyekiti huyo amesema makatibu muhtasi  ni kada muhimu kwenye shughuli za utawala wa taasisi hivyo kujifunza mbinu mpya kutawasaidia kuwapa uwezo wa kushindana kwenye soko la ajira la Afrika Mashariki.

"Nipende kuishukuru serikali kwa uamuzi wa kuanzisha shahada ya uhazili mwaka 2017 baada ya kuwasilisha maombi yetu sasa hivi tunajivunia wanachama wetu wamepewa ruhusa na waajiri kuongeza kiwango cha elimu hadi ngazi hiyo," amesema Zuhura.

Katibu Mkuu wa Tapsea, Anneth Mapima amesema mbali na mada zinazowasilishwa wanachama wanapata nafasi ya kujadili kwa kina changamoto zinazowakabili kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi.