Mdee: Hatujakata rufaa, muda bado upo

Mdee: Hatujakata rufaa, muda bado upo

Muktasari:

Halima Mdee, alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) amesema yeye na wenzake 18 waliofukuzwa uanachama wa chama hicho baada ya kula kiapo cha ubunge wa viti maalumu bila ridhaa ya chama, bado wana muda wa kukata rufaa kupinga adhabu hiyo.

Dar es Salaam. Halima Mdee, alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) amesema yeye na wenzake 18 waliofukuzwa uanachama wa chama hicho baada ya kula kiapo cha ubunge wa viti maalumu bila ridhaa ya chama, bado wana muda wa kukata rufaa kupinga adhabu hiyo.

Akizungumza na gazeti hili, Mdee alisema hadi kufika leo wana siku 17 zaidi za kukata rufaa baraza kuu kupinga uamuzi wa kamati kuu ya chama hicho iliyowavua uanachama na nyadhifa zao zote.

Mbali na Mdee wengine ni Ester Bulaya, Ester Matiko, Agnesta Lambert, Grace Tendega, Salome Makamba, Jesca Kishoa , Nusrat Hanje, Tunza Malapo, Conchestar Rwamlaza.

Wengine ni Naghenjwa Kaboyoka, Hawa Mwaifunga, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Asia Mohammed, Sophia Mwakagenda, Cecilia Pareso na Felister Njau ambao walivuliwa uanachama na kamati kuu Novemba 26 baada ya kukiuka msimamo wa chama hicho.

Desemba mosi, Mdee aliwaeleza wanahabari kuwa hawana mpango wa kuondoka ndani ya chama hicho na kwamba wana mpango wa kukata rufaa baraza kuu ili haki itendeke dhidi yao.

Novemba 30 walipewa barua za uamuzi wa kufukuzwa uanachama na hivyo kuwa na fursa ya kukata rufaa wakitakiwa kufanya hivyo ndani ya siku 30 tangu kupokea barua hiyo.

“We have 30 days (tuna siku 30 tulizopewa) kwa ajili ya kukata rufaa. Sasa nashangaa hapa haya yanayoendelea hapa katikatika deadline ni Desemba mwishoni. Tutapeleka rufaa zetu kwa sababu bado tunakipenda Chadema. Watu wasitulazimishe tukate rufaa leo au juzi bado siku zipo,” alisema Mdee.

Katika rufaa hiyo, Mdee na wenzake wataeleze namna walivyokwenda kuapa wakati chama chao kikilumbana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhusu aliyewatuma waende, mtu aliyepeleka majina katika tume hiyo.

Wakati hayo yakijiri Chadema kilitangaza kuanza kutumia nguvu ya mahakama kupinga mchakato wa uteuzi wa wabunge hao 19 na mtu aliyesaini fomu zao kwa nafasi ya katibu mkuu.Hata hivyo kwa nyakati tofauti, Spika wa Bunge alisisitiza Mdee na wenzake ni wabunge halali na watekeleze majukumu yao ya kibunge popote walipo.