Mdee na wenzake sasa wasubiri uamuzi wa Dk Tulia

Wabunge wa Viti Maalumu, Grace Tendega (kushoto) na Salome Makamba wakiuliza maswali bungeni jijini Dodoma leo wakati wa kikao cha 50 cha mkutano wa Saba wa Bunge la Bajeti. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Ni ukweli ulio wazi kuwa sasa hatma ya wabunge 19 wa viti maalum akiwemo Halima Mdee waliofukuzwa uanachama Chadema ipo mikononi mwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.


Dodoma. Ni ukweli ulio wazi kuwa sasa hatma ya wabunge 19 wa viti maalum akiwemo Halima Mdee waliofukuzwa uanachama Chadema ipo mikononi mwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Hiyo ni baada ya Mahakama Kuu Dar es Salaam kutupa maombi ya kina Mdee kutaka kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama wa Chadema.

Wabunge wengine wanaosubiri hatma ya Dk Tulia ni Ester Bulaya, Salome Makamba, Cecilia Pareso, Tunza Malapo, Nustrat Hanje, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Grace Tendega na Esther Matiko.

Wengine Hawa Mwaifunga, Jesca Kishoa, Asia Mohammed, Kunti Majala, Sophia Mwakagenda, Conchesta Rwamlaza, Anatropia Theonest na Agnes Lambart.

Hatua ya kutupilia mbali kwa kesi hiyo imetokana na Chadema kuweka pingamizi ikiomba mahakama isisikilize madai hayo kwa kuwa yalikuwa na kasoro za kisheria.

Mei 16, 2022 Dk Tulia alisema anasubiri uamuzi wa mahakama kuhusu wabunge waliofukuzwa uanachama na kwamba wabunge hao wataendelea na ubunge wao hadi hapo mahakama itakapotoa uamuzi.

“Bunge haliwezi kuingilia mchakato huo mpaka Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi, ninalazimika kutokutangaza kuwa nafasi za viti maalumu 19 vya Chadema viko wazi mpaka pale mahakama itakapokamilisha kazi yake ya kutoa uamuzi” alisema Dk Tulia.

Hata hivyo, jana jioni na leo asubuhi Alhamisi Juni 23, 2022 wabunge hao bado wameendelea kuwepo bungeni kama kawaida ambapo leo katika kipindi cha maswali na majibu bungeni Dk Tulia alimpa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza Salome Makamba.

Katika swali hilo, Makamba alihoji ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba katika vituo viwili vya afya vya Kambarage na Magua viliovyopo Shinyanga Mjini ambavyo vinahudumia wakazi wengi.

Akijibu swali hilo la nyongeza, Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange amesema kipaumbele cha Serikali ni kupeleka vifaa tiba kwa vituo vya afya ambavyo vimekamilika ili viweze kutoa huduma kwa watu wengi.