Membe adai wapo wana-CCM waliokichoka chama

Muktasari:

Membe ameyasema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini hapa ambapo alikuwa akitoa taarifa ya kuwa bado ni mgombea wa kiti cha urais kupitia chama chake.

Dar es Salaam. Mgombea urais kupitia chama cha ACT- Wazalendo, Bernard Membe amesema walipokea maombi ya watu 42 walioenguliwa Chama cha Mapinduzi wakitaka kujiunga na chama chao.

Membe ameyasema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini hapa ambapo alikuwa akitoa taarifa ya kuwa bado ni mgombea wa kiti cha urais kupitia chama chake.

Membe alisema walipokea maombi hayo siku moja baada ya kura za maoni ambapo wanachama wa CCM ikiwemo waliokuwa wabunge walioenguliwa katika mchakato huo walianza kukihama chama.

“Siku ya pili tu baada ya kuenguliwa tulipokea maombi 42 ya watu walioenguliwa CCM wakitaka kujiunga ACT, sina hakika katika vyama vingine walikwenda wangapi,”

“Lakini sisi walikuwa 42,  wabunge walioenguliwa kutoka CCM wakisema tumechoka lakini nilifuatilia kwa karibu sana niligundua siku ya tatu baada ya kura za maoni ilitengenezwa operesheni maalum ya CCM ya kuwazuia wabunge walioenguliwa kujiunga na vyama vingine ”

“Walizuiliwa kwa kuahidiwa kuwa zipo kazi nyingi watapewa, tutawaaajiri, hatutawatumbua,” amesema Membe

Amesema hiyo inamaanisha kuwa ndani ya CCM kuna watu wengi ambao wamechoka huku akibainisha kuwa katika kipindi ambacho alikuwa kimya katika kampeni aliwapigia simu, kuzungumza nao na kufanya nao kazi.

“Na nimegundua kwamba ndani ya Chama cha Mapinduzi watu wamechoka,” amesema Membe.