Meya manispaa ya Moshi aanika vipaumbele vyake

Muktasari:

Mstahiki Meya wa manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Juma Raibu amesema kwa kushirikiana na baraza la madiwani atahakikisha vipaumbele vilivyowekwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM vinatekelezwa ili kuleta maendeleo yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Moshi. Mstahiki Meya wa manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Juma Raibu amesema kwa kushirikiana na baraza la madiwani atahakikisha vipaumbele vilivyowekwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM vinatekelezwa ili kuleta maendeleo yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Ameeleza hayo leo Ijumaa Desemba 4, 2020 mara baada ya kutangazwa na katibu tawala Wilaya ya Moshi, Angelina Marco kuwa mshindi  wa nafasi hiyo

Katika uchaguzi huo alipata  kura 29 kati ya kura zote 29 zilizopigwa huku diwani  mmoja wa Chadema akitoka nje ya ukumbi kabla ya kuanza kwa shughuli ya kupiga kura.

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, ambayo ilikuwa chini ya Chadema kwa miaka 10 mfululizo katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020, CCM ilishinda katika kata 20 huku Chadema ikishinda katika kata Moja.

Raibu amesema katika kuendesha baraza la madiwani atasimamia na kufuatilia misingi bora ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo ikiwemo miradi mbalimbali ya ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi ya Nganga mfumuni,dampo la kisasa,Moshi kuwa jiji pamoja na kiwanda cha mbolea.

"Nitahakikisha maendeleo yanakuwepo kwa wananchi pasipo kubagua mtu ama chama ,nawasisitiza madiwani kuwa chachu katika kutatua kero za wananchi wa Manispaa ya Moshi "Amesema Raibu