Meya Ubungo akomaa na Makonda

Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob

Muktasari:

  • Jana, Meya Jacob alifika kwenye ofisi hiyo ya Sekretarieti katika kile alichosema kuwa ni kuitika wito kuhusiana na suala lake alilofikisha hapo.
  • “Nitaeleza kwa kifupi tu kile tulichojadiliana huko juu na Sekretarieti,” alisema Meya Jacob baada ya kushuka kutoka ghorofa ya nne ya Jengo la Sukari zilipo ofisi hizi na kukutana na waandishi wa habari waliokuwa wakimsubiri.

Dar es Salaam. Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob ameapa kuendelea kupambana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ili kuhakikisha mashtaka aliyoyafikisha Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya kiongozi huyo wa mkoa yanafanyiwa kazi na kusisitiza kuwa hayuko tayari kuyafuta.

Jana, Meya Jacob alifika kwenye ofisi hiyo ya Sekretarieti katika kile alichosema kuwa ni kuitika wito kuhusiana na suala lake alilofikisha hapo.

“Nitaeleza kwa kifupi tu kile tulichojadiliana huko juu na Sekretarieti,” alisema Meya Jacob baada ya kushuka kutoka ghorofa ya nne ya Jengo la Sukari zilipo ofisi hizi na kukutana na waandishi wa habari waliokuwa wakimsubiri.

Meya huyo ambaye mahojiano yake na Sekretarieti yalidumu kwa takriban saa nne, alidai kwamba amekuwa akiombwa kufuta shauri hilo na mara kadhaa.

Alidai kwamba watendaji wa Sekretarieti walimwarifu kuhusu ombi la mkuu wa mkoa kukutana naye kwa ajili ya kushauriana jinsi ya kulimaliza shauri lake.

Hata hivyo, hakuna ofisa wa Sekretarieti aliyekuwa tayari kuzungumzia mahojiano na meya huyo wakisema msemaji ni Kamishna Honoratus Seleke ambaye ilielezwa kuwa yuko Dodoma.

Meya huyo amemshtaki Makonda kwenye tume hiyo akidai kwamba ameghushi vyeti jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya utumishi wa umma.

“Mkuu wa mkoa ametumia jina lisilo lake na amekula kiapo kwa kutumia jina ambalo pia siyo lake mambo ambayo kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 398 ni kosa na ndiyo maana nimeiomba Sekretarieti isimamie sheria wala isiangalie jambo lingine,” alisema : “Lakini sasa nasikia serikali ya mkoa wanataka tumalizane… mimi nasema hili haliwezekani lazima lifikishwe mwisho wake.

“Najua baraza hili halina mamlaka ya kumwajibisha mkuu wa mkoa litakachofanya ni kutoa ushauri tu, mtu mwenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Rais lakini itakuwa jambo la heri iwapo tukajulishwa ukweli kwamba tunafanya kazi na Daudi Albert Bashite au la… sisi tukijua hilo hatutakuwa na kinyongo tutaendelea kumpa ushirikiano” alisema.

Aliitaka sekretarieti hiyo kutembea katika kweli ili uamuzi wake uendelee kuweka kumbukumbu itakayoheshimika daima.

“Sekretarieti iamue moja, ifanye maamuzi yatayoifanya iheshimike milele au itoe uamuzi utakaofanya idharaulike milele,” alisema.