Mfahamu Sista Hellen aliyeteuliwa mjumbe bodi ya Tanesco

Mjumbe mpya wa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco, Sr Dk Hellen Bandiho

Muktasari:

  • Dk Hellen amesema hakutarajia kuteuliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo

Mwanza. “Sikutarajia kuteuliwa lakini kwa sababu imeonekana naweza kufanya jambo niko tayari kulitumikia Taifa huku nikiendelea na majukumu yangu.”

Hayo ni maneno ya Dk Hellen Bandiho, mtawa wa Kanisa Katoliki aliyeteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Sista, Hellen aliyeteuliwa Machi 14, mwaka huu na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, ni miongoni mwa wajumbe wanane wa bodi ya wakurugenzi wa Tanesco watakaohudumu kwa miaka mitatu akiungana na mwenyekiti wao, Dk Rhimo Nyansaho.

Wajumbe wengine ni Dk Lucy Mboma, Isaack Chanji, Boma Raballa, Grace Joachim, Balozi Zuhura Bundala, Profesa Ninatubu Lema, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Mwingine anayeungana nao katika uteuzi huo utakaoanza Machi 18, 2024 ni Idris Kikula, aliyewahi kuwa mwenyekiti Tume ya Madini Tanzania, pia kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Uteuzi wa mtawa huyo kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi Tanesco siyo tu uliwavutia wengi, bali uliibua mjadala katika mitandao ya kijamii ukiwemo mtandao wa ‘X’ (zamani Twitter) huku wengine wakimpongeza kwa kuaminiwa kulitumikia Taifa katika wadhfa huo licha ya kuwa mtawa.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kutokana na mijadala hiyo, Mwananchi Digital limemtafuta leo Jumapili, Machi 17, 2024 mtawa huyo kujua alivyopokea uteuzi huo pamoja na jinsi atakavyoweza kutekeleza majukumu yake ya kitawala na haya ya ujumbe wa bodi.

Dk Hellen amesema hakutarajia kuteuliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo huku akiahidi imani aliyopewa na Dk Biteko ni deni lake kwa taifa.

“Ninaamini nimeteuliwa kwa sababu nina vigezo kama wengine na nimekidhi vigezo hivyo wakati ambao nimeshakuwa mtawa. Kwa hiyo, kuna watu imewashtua kidogo, wengine imewafurahisha lakini kwa wasiyofahamu nilishawahi kuwa mwenyekiti wa bodi,” amesema Dk Hellen.


Sista Hellen ni nani?

Ni mzaliwa wa Kijiji cha Kishanje, Halmashauri ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera. Ni mtoto wa pili kati ya watoto wanane ambao wamebaki watano katika familia ya Antony Bandiho na Selestina Bandiho.

Amesema safari ya maisha yake kitaaluma ilianza kunoga baada ya kuhitimu elimu ya msingi kijijini hapo kisha kwenda kujiunga katika chuo cha Nyegezi Social Training Institute (NSTI) na kusoma Stashahada ya Usimamizi wa Malighafi.

“Nilipohitimu nikabaki NSTI na kuanza kufanya kazi kama mkufunzi msaidizi, baadaye nikaombwa kwenda Hospitali ya Bugando ilikuwa inarudi kusimamiwa na Kanisa Katoliki kwa hiyo nikaenda kuwa ofisa usambazaji.

“Ilipofika mwaka 1990, nilienda kusoma Shahada ya Sayansi na Usimamizi wa Biashara (BSBA) katika Chuo cha Edgewood kilichopo Winsconsin Marekani, kisha nikaunganisha kusoma shahada ya uzamili nilipohitimu nikarudi Tanzania kufundisha NSTI pale Malimbe, Nyegezi jijini Mwanza,” amesema.

Huku akiendelea kufundisha, mchakato wa kuipandisha NSTI kuwa taasisi inayotoa elimu ya juu (Chuo Kikuu) ulioanza chini ya uongozi wa Padri Deogratius Rweyongez; na moja ya matakwa ni kuwa na walimu wenye elimu ya uzamivu.

Kufuatia takwa hilo, NSTI ilimwezesha kurejea Marekani kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Utawala wa Elimu katika Chuo Kikuu cha Duquesne kilichopo Pennyslavia nchini humo, alipohitimu alirejea nchini na kuasisi uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine (SAUT) mwaka 1998.

“Nilirudi SAUT nikafundisha wakati huo nikiwa Mkuu wa Kitivo cha Usimamizi wa Biashara cha chuo, baada ya hiyo nikawa Mkurugenzi wa Elimu ya Juu chuoni, kisha nikaambiwa nikawe Mkuu wa chuo tawi la SAUT lililopo Arusha. Baadaye nikarudi Washington DC kufanya tafiti mbalimbali,” amesema.

Amesema baada ya kuhitimisha tafiti hizo, alirejea nchini na kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Mashirika ya Kitawa ya Afrika Mashariki na Kati (nchi 10) yenye makao makuu yake Nairobi nchini Kenya.

Baada ya utumishi katika mashirika hayo, Mkutano Mkuu wa Shirika la Masista wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu kutoka Jimbo Katoliki la Bukoba ulimchagua kuwa Mama Mkuu wa shirika hilo tangu 2021 ambapo ataliongoza kwa miaka sita.


Utumishi wake serikalini

Sista Hellen siyo tu kwamba ni mtawa katika imani, pia amewahi kuwa mtumishi wa Serikali katika nyadhifa mbalimbali ikiwamo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi na Ugavi Kitaifa (PSPTP) katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.

Ulipofika utawala wa awamu ya tano chini ya Hayati John Magufuli, Sista Hellen amesema aliaminiwa na kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Mafunzo na Elimu ya Uvuvi (Feta), mjumbe wa bodi ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi Shirikishi (Cuhas) na Taasisi ya Maendeleo ya Mwanamke (ASEC).

“Mimi pia ni mjumbe niliyepitishwa na Bodi ya PSPTP na Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania, kwa hiyo sidhani kama nimeteuliwa kwa sababu ni mtawa bali nimeteuliwa kwa sababu nina vigezo vya kuteuliwa. Nilishakuwa mwenyekiti wa bodi,” amesema.

“Sikutarajia kuteuliwa; mwanzoni nilipata taarifa za uteuzi wangu kwenye mtandao wala awali sikuwa na habari yoyote, lakini uteuzi huu ni mfano wa kitu ambacho nilishawahi kukipata miaka ya nyuma.

“Kwa hiyo mkisema kama ninaweza kufanya kazi chochote kwenye bodi hii, niko tayari kutumikia Taifa na huku nikiendelea na majukumu yangu ya utawa,” anasema mtawa huyo.


Anavyojigawa, ahadi yake

Akizungumzia anavyoweza kutenganisha majukumu ndani ya kanisa na Serikali, Sisita Hellen amesema mgawanyo wa majukumu katika taasisi hautofautiani na wa mwalimu ama mzazi ambaye ni mtumishi serikalini.

Amesema utekelezaji wa majukumu yoyote hutegemea nidhamu na ushirikiano wa watumishi katika taasisi husika hivyo, anaamini weledi, ubunifu na mchango wa utumishi wake katika majukumu mapya ndani ya Tanesco utasaidia kuiboresha taasisi hiyo ili kukidhi matarajio ya watanzania.

“Nina imani kwamba huwa kuna wengine wanaoteuliwa wenye madaraka kama yangu lakini labda ni mkuu wa shule ama mkuu wa chuo ana maelfu ya wanafunzi kwa hiyo lazima ujue kipi cha kufanya na lini, haya majukumu hatuyafanyi peke yetu. Kwa mfano kwenye uongozi wa watawa nina wajumbe wa baraza katika timu ya uongozi mwingine anaangalia elimu, afya na mambo mengine ya masista lakini inahitaji nidhamu ujue utafanya nini na lini.

“Kwa sababu sisi tunahudumia watu na watu wako kila sehemu kwa hiyo kupata fursa kama hizi tunaendeleza mission (kusudi) letu la kuwafikia watu na kuwatumikia. Wengine ni madaktari na manesi wote hao wanatekeleza matarajio ya Mungu ya kuwatumikia watu,” amesema.

“Ule mshangao wa watu nilikuwa naushangaa kwa sababu wengine wanasema haijawahi kutokea Sista kuteuliwa kwenye bodi za Serikali nafikiri hawakuwa na taarifa tu, tumeshawahi kuingia kwenye bodi mbalimbali za nchi hii.”


Awafunda vijana

Kufuatia uteuzi wake, Sista Hellen anatuma ujumbe kwa wasichana ambao wako shuleni kuamini kwamba kila jambo linawezekana huku akiwataka kuongeza bidi katika elimu kwa kile anachodai elimu ni dhamana ya kuwafikisha katika nafasi mbalimbali ikiwemo uteuzi.

“Ni vigezo vya elimu ambavyo vitakupeleka mbali, wavumilie watapitia matatizo ndiyo lakini wawe na kitu ambacho kinashikika wasitegemee kwamba watapewa kilele mama lazima uwe na kitu ambacho kitakulinda. Mimi siwezi kusema kwamba utawa ndiyo umenilinda, hapana! Ni elimu ndiyo imenibeba,” anasisitiza.



Kauli ya SAUT

Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Agostino (SAUT) Mwanza, Profesa Costa Mahalu ameeleza kufurahishwa na uteuzi wa Dk Hellen kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Tanesco huku akisema uteuzi huo umekipatia chuo hicho heshima na kutambulika.

“Sikuwahi kufanya kazi na Dk Hellen lakini ninapoona watu ambao wametengenezwa na SAUT wanapewa dhamana ya kushiriki kutoa maamuzi ya taasisi za nchi inanifurahisha. Ninamtakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yake,” amesema Profesa Mahalu.

Huku akimuita Sista Hellen ‘Mama’, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano kwa Umma (BAMC) SAUT Mwanza, Dk Peter Mataba amesema anaamini misimamo na ubunifu wa mtawa huo utakuwa na mchango mkubwa kwa taifa huku akiwashauri wajumbe wenzake na watumishi wa Tanesco kumtumia kufikia malengo.

“Namfahamu Sista Hellen alikuwa mwalimu wangu na ametulea hata wakati naanza kazi SAUT kama mhadhiri. Kwa miaka yote niliyomfahamu ni Sista ambaye ni mchapakazi, asiye na mzaha kwenye mambo ya kazi na mwenye roho nzuri sana, mimi na Dk Tibaijuka tunamuita Mama,” amesema Dk Mataba.

“Ni mwana taaluma halisi, mtulivu kwenye kufanya maamuzi naamini ndiyo maana ameteuliwa zaidi ya mara moja katika bodi mbalimbali. Ataleta mchango mkubwa ndani ya Tanesco,” amesema msomi huyo.

Uteuzi wa wajumbe wapya wa bodi ya wakurugenzi Tanesco akiwamo mtawa, Dk Hellen ulifanyika kwa mujibu wa kifungu namba 19 (1) na (3) cha Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992.

Bodi iliyopita iliongozwa na mwenyekiti, Omary Issa na wajumbe walikuwa Nehemiah Mchechu, Balozi Mwanaid Majaar, Christopher Gachuma, Mhandisi Cosmas Massawe, Lawrence Mafuru, Zawadi Nanyaro, Abubakar Bakhresa na Abdallah Hashim.