Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mfanyabiashara maarufu mjini Moshi, Dodoma ajiua kwa kujinyonga

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema limetokea Julai 10, 2025, akieleza kuwa chanzo ni msongo wa mawazo uliotokana na kuugua afya ya akili kwa muda mrefu.

Moshi. Mfanyabiashara maarufu katika mji wa Moshi na mkoani Dodoma, Ronald Malisa (35), anadaiwa kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia shuka katika choo cha nyumba yake, eneo la Msufuni, Kata ya Msaranga, huku chanzo cha tukio hilo kikidaiwa kuwa ni msongo wa mawazo.

Inadaiwa mara kadhaa mfanyabiashara huo alijaribu kujiua kwa kunywa sumu na alikuwa akiokolewa na familia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema tukio hilo limetokea jana, Julai 10, 2025, akisema chanzo ni msongo wa mawazo uliotokana na kuugua afya ya akili kwa muda mrefu.

“Saa 12:30 asubuhi, Julai 10, 2025, huko Msaranga, mfanyabiashara mkazi wa Dodoma na Msaranga aligundulika kufariki kwa kujinyonga kwenye dirisha la choo kilichopo chumbani kwake kwa kutumia shuka,” amesema Kamanda Maigwa.

Kamanda Maigwa amesema mfanyabiashara huyo amekuwa akijaribu kujiua mara kadhaa kwa kunywa sumu, lakini alikuwa akiokolewa na mama yake mzazi.

“Mfanyabiashara huyu alikuwa akijaribu kujiua kwa kunywa sumu na kuokolewa kwa muda wa miaka mitano. Mama yake alipomuuliza ni kwa nini anafanya hivyo, alidai kuna mtu anamsumbua kwenye kichwa chake,” amesema Kamanda Maigwa.

Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC, kwa uchunguzi zaidi.

Akielezea tukio hilo, mdogo wa mfanyabiashara huyo, Lucy Malisa, amesema kaka yake huyo amekuwa akiwaeleza kuwa kuna mtu anamsumbua katika kichwa chake, lakini hakuwahi kuweka wazi sababu ni nini.

Lucy amesema jana asubuhi walipoamka, alimuamsha kaka yake waende maombi, lakini alimgongea bila mafanikio, ndipo baadaye walipobaini kuwa amefariki kwa kujinyonga.

“Niliamka asubuhi kumuamsha kaka ili aende kwenye maombi. Nikakuta amefariki kwa kujinyonga chooni,” amesema na kuongeza:

“Ni jaribio lake la tatu au la nne la kutaka kujiua. Chanzo kikubwa hatujui, ila mara kwa mara alikuwa akisema kuna mtu anamchezea, na alikuwa haweki wazi.”

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa wa Msaranga, Timothy Ngowi, amesema tukio hilo ni la kusikitisha na kwamba kijana huyo alikuwa mtu mwenye ushirikiano katika jamii.

“Nilipata taarifa kwamba kajinyonga, na mimi sikujua kama yupo Moshi maana anaishi Dodoma. Kwa kweli ni tukio la kusikitisha, maana alikuwa mtu mwenye ushirikiano na watu kwenye jamii,” amesema mwenyekiti huyo.

Naye, jirani wa mfanyabiashara huyo ambaye pia ni mjumbe wa serikali za mtaa, Abrahaman Zuberi, amesema tukio hilo ni la kushangaza kwa kuwa mfanyabiashara huyo alikuja Moshi kwa ajili ya kusalimia ndugu zake.

“Jana asubuhi nikiwa kwenye shughuli zangu, saa moja nilipigiwa simu kwamba jirani yangu kajinyonga. Alikuja kwa ajili ya kusalimia ndugu zake. Imetuuma sana kwa kweli,” amesema Zuberi.