Mfumo wa dijitali mwarobaini Dart -3

Dar es Salaam. Baada ya kuzungumzia mazingira magumu wanayokutana nayo abiria wa mabasi yaendayo haraka na kugusia masuala ya ubia yalivyoathiri mradi huo, leo tutaangazia uzoefu wa kimataifa, nafasi ya mifumo ya kidijitali na hali inayotamaniwa kwa awamu zijazo.

Wakati Serikali ikifungua milango, uzoefu unaonyesha miradi mingi ya mabasi yaendayo haraka huendeshwa na manispaa na majiji.

Mathalani miradi ya mabasi yaendayo haraka ya majiji ya New York, Tokyo na London iko chini ya usimamizi wa mameya wa maeneo hayo.

Kwa mujibu wa tovuti ya GoBRT, Jiji la New York linaloendeshwa na Mamlaka ya Usafiri ya Metropolitan (MTA), linahudumia zaidi ya abiria milioni 2.5 wa mabasi ya umma katika njia 365 zinazotumia mabasi zaidi ya 450.

“Majiji mengi ninavyofahamu yanaendeshwa na meya, yeye ndiye anaweza kupanga huduma za jiji au mji zinahitajika wapi, sasa kwetu inaonekana tofauti,” kilieleza chanzo kutoka Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), inayoendesha mradi huo wa mwendokasi.

Kwa mujibu wa tathmini ya Benki ya Dunia (WB) ya mwaka 2021, mahitaji tisa ya sekta binafsi kabla ya kuingia katika uwekezaji huo ni uwezo wa mitaji kutoka taasisi za kifedha, miongozo ya kisheria na kikanuni katika uendeshaji, mfumo na muundo imara wa biashara, sera na utashi wa kisiasa.

Mengine ni uhimilivu wa soko, uimara wa kitaasisi katika uendeshaji wa mifumo ya mradi huo, vivutio vya kulinda mitaji ya uwekezaji, ushirikishaji wa wamiliki wa daladala katika mipango ili kuepuka vitisho vya soko na uchambuzi wa thamani ya mradi.


Dart na dijitali

Mwanzoni mradi wa BRT nao ulikumbatia matumizi ya dijitali, ndani ya basi abiria alikuwa akipewa dondoo kuhusu safari kupitia skrini za mbele na pembeni, miongoni mwa taarifa muhimu zilikuwa muda wa safari hadi kituo cha mwisho.

Taarifa nyingine ni kujua jina la kituo kinachofuata na muda wa kuwasili, huduma ya sauti ya taarifa hizo iliwasaidia wasioweza kuona, lakini pia malipo ya nauli yalikuwa yanafanyika kidijitali, jambo lililoweka urahisi wa kupangilia bajeti ya nauli kwa kipindi fulani.

Ukiwa kituoni ulipata taarifa ya basi linalowasili linaelekea njia gani na kujua iwapo basi hilo ni la moja kwa moja (express) au la kawaida.

Mambo yote hayo siku hizi hayapo, hivyo kidijitali hakuna tofauti ya mwendokasi na daladala za kawaida.

Hata hivyo, Dart inajivunia kuishi katika mifumo ya kidijitali, ikiwamo mfumo wa kiganjani uitwao Mwendokasi App, mifumo ya ukusanyaji wa nauli (GoT-AFCS) na uongozaji wa mabasi (ITS) lakini Serikali hairidhishwi na huduma hiyo inayodhibiti upotevu wa mapato na kuimarisha huduma.

Programu hiyo tumizi ya mwendokasi itasaidia katika ukataji tiketi, kupanga safari, kutoa taarifa ya tukio lililotokea, kufahamu changamoto iliyotokea njiani ikiwamo ajali, kufuatilia uelekeo wa mabasi na ratiba husika, kufahamu maswali yanayoulizwa mara kwa mara.

Serikali inakiri bado kumekuwa na changamoto za matumizi ya mifumo hiyo, ikiagiza marekebisho kwa lengo la kuimarisha usalama na mapato.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Edwin Mhede, alinukuliwa na gazeti hili akisema mifumo iko katika maandalizi ya utoaji huduma za tiketi.

Alisema tayari kadi zimewasili na mfumo kutengenezwa kwa ajili ya mageti matatu ya kuanzia.

"Tunaanza na mageti matatu, tukisubiri mengine yaje, lakini niahidi litafanyika ndani ya kipindi kifupi kijacho," alisema Dk Mhede.


Awamu sita Dar

Kwa mujibu wa utafiti wa Dart, ifikapo mwaka 2030 watumiaji watafikia 3,050,000 kwa siku kwa mahitaji ya mabasi 3,290 katika njia zipatazo 129. Idadi hiyo itakuwa ni zaidi ya robo ya wakazi wa jiji hilo linalokadiriwa kufikia wakazi milioni 10 ifikapo mwaka 2030.

Utafiti huo unaonyesha mahitaji ya watumiaji wa usafiri wa umma yataongezeka hadi kufikia 2,590,000 kwa siku mwaka 2025 kwa mahitaji ya mabasi 1,975 katika njia 80.

Awamu ya kwanza inayotoa huduma hivi sasa ilijenga kilomita 20.9 kwa thamani ya Dola 260 milioni (Sh652.6 bilioni).

Awamu ya pili inatarajiwa kujenga kilomita 20.3 kwa Dola 141.7 milioni (355.6 bilioni), awamu ya tatu kilomita 24.3 kwa Dola 148.2 milioni (371.9 bilioni) na awamu ya nne kilomita 30.1 kwa Dola 97.9 milioni (Sh245.7 bilioni).

Awamu ya tano Euro 178 milioni (Sh500 bilioni) na awamu ya sita Dola 261 milioni (Sh650 bilioni).

Kwa sasa, awamu ya pili ya mradi huo ni kutoka Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu na una kilomita 20.3, unatarajiwa kuanza wakati wowote baada ya mzabuni wa manunuzi ya mabasi kupatikana.

Mkurugenzi wa Udhibiti wa Vyombo vya Barabara kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Johansen Kahatano anasema daladala 2,461 zitaondolewa katika barabara hiyo awamu ya pili mradi utakapoanza.

Awamu ya tano ya mradi huo wenye thamani ya Euro 178 milioni (Sh427 bilioni), inatarajiwa kuanza Desemba mwaka huu na kukamilika mwaka 2025.

Ujenzi wa awamu ya tano wenye urefu wa kilomita 26, utaanzia makutano ya daraja la juu la Kijazi Ubungo kupitia Barabara ya Mandela na kwenda kuungana na barabara ya mwendo wa haraka ya Mbagala. Pia itahusisha barabara ya Segerea.

Meneja Uhusiano wa Umma wa Dart, William Gatambi anasema tayari hati za ununuzi zimewasilishwa kwa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) bila pingamizi kwa wafadhili kwenye mradi huo.