Ripoti maalumu: Mradi wa mwendokasi shubiri kwa watumiaji -1

Abiria wakigombania kupanda katika basi la mwendokasi. Picha na mtandao

Muktasari:

  • Ni miaka minane tangu mradi huo umeanzishwa bado haujakidhi matazamio ya watumiaji. Uchache wa mabasi wageuka mwiba kwa msongamano, kupoteza muda, waendeshaji wautetea, Serikali yautetea

Dar es Salaam. Ikiwa imetimia miaka minane tangu kuanzishwa kwa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT), bado una changamoto nyingi zinazoufanya usiwe wa uhakika na kuaminika kwa watumiaji.

Abiria wanaotegemea usafiri huo kwa wastani wanapoteza dakika 40 kila siku kusubiri usafiri kituoni kutokana na upungufu wa mabasi, unaofanya mahitaji ya usafiri huo kuwa makubwa.

Kwa mujibu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), mabasi yaliyopo hivi sasa ni 210, yakiwemo makubwa yanayohudumia wastani wa abiria 160 kila moja na madogo ya abiria 60 kila moja.

Kwa jumla mabasi yote yanakadiriwa kutoa huduma kwa zaidi ya abiria 200,000 kwa siku katika jiji lenye wakazi milioni 5.38.

Huduma ya usafiri huo kwa sasa inapatikana katika maeneo ya Kibaha, Kimara, Kivukoni, Gerezani, Mbezi Luis, Morocco na Muhimbili.

Hata hivyo, takribani vituo 50 katika njia za mabasi hayo vimeonekana kukusanya abiria wengi kuliko idadi ya mabasi yanayohudumia kila siku na hivyo licha ya kupoteza muda, kumekuwepo msongamano wa abiria kwenye mabasi, hali inayotishia usalama wao na mali zao.

Kumekuwepo na mahitaji makubwa ya usafiri huo kwa siku za Jumatatu hadi Ijumaa, hususan asubuhi na jioni wakati wa kwenda na kutoka katikati ya mji kwenye majukumu mbalimbali, ingawa baadhi ya watumiaji hukumbana na adha mbalimbali.

Mtumiaji wa usafiri huo ambaye ni fundi ujenzi, Mohammed Waziri anasema ameshawahi kupoteza zaidi ya kazi 20 kutokana na muda unaopotea kwenye huduma hiyo.

“Nilipigiwa simu Kariakoo nikachukue kazi ya ujenzi wa nyumba, lakini nikachelewa kituo cha mwendokasi Kimara kwa zaidi ya dakika 40, baadaye jamaa akanipigia simu ameahirisha hadi siku nyingine,” anasema Waziri.

Paulina Martin, pia mkazi wa Kimara, anasema hutumia zaidi ya saa moja kupata usafiri huo, kwa kuwa mabasi katika vituo yanakawia kufika.

“Mbaya zaidi tunaopandia hapa Kimara mwisho ndio tunateseka, kwani ndiko wanakoshushwa watu wa Kibaha, hivyo bila nguvu ya kugombania basi, hata kuweka mguu huwezi,” anasema Martin.

Kwa upande wake, Amandina Kiwelu anasema wakati usafiri huo unaanza, aliamini ungemsaidia kuwahi kukaanga samaki anaowachukua Soko la Feri, lakini sasa imemlazimu awe anawakaanga hukohuko feri.

“Jambo hili limeathiri biashara yangu, kwani baadhi ya wateja hupenda kuona samaki akiwa freshi anapikwa kwa kuhofia udanganyifu wa kukaangwa na mafuta yasiyo safi.

“Lakini nashindwa kuwaridhisha katika hili kwa kuwa na mimi nakimbizana na muda ili niweze kufanya biashara,” anasema.

Baadhi ya huduma zilizokuwa zinatolewa wakati mabasi yanaanza mwaka 2016 ambazo sasa hazipo ni pamoja na utoaji wa taarifa kwa mfumo wa vinasa sauti kwa abiria kabla, wakati na muda wa kushuka.

Licha ya msongamano wa abiria, mabasi hayo yalitoa huduma za malipo ya kadi kwa muda unaohitajika kutumia usafiri huo, masuala ambayo miundombinu yake sasa imechakaa.

Hali hiyo inazungumziwa pia na Innocent Iman, anayesema uwepo wa mabasi machache yanayotoa huduma, unachangia pia uharibifu wa hayo yaliyokuwepo, kwani watu wakati wa kuyapanda hugombea kwa kusukuma milango.

“Tazama mabasi ndani yalivyochoka kwa kuwa yamezidiwa, ustaarabu uliokuwepo mwanzo wakati usafiri huu unaanza sasa ni tofauti,” anasema Iman.

Kwa upande wake Alma Mussa anasema kuna wakati hulazimika kupanda bajaji kuanzia Kimara Kona hadi Manzese ili kupanda mwendokasi, kwa kuwa pale walau kuna baadhi ya abiria wanashuka na nafasi kupatikana.

“Ni bora wangerudisha daladala tujue moja, kwani kuna wakati hata unalazimika kutoka ndani ya kituo licha ya kuwa umeshalipa nauli na kuchukua bodaboda au usafiri mwingine kuwahi unakokwenda, tunaomba Serikali iliangalie hili, tatizo nini, hawataki kuleta mabasi mengine,” anasema Alma.

Alma anasema mpangilio wa mabasi kwenye mzunguko unatia shaka, kwa kuwa wakati mwingine yanafika kituoni kwa pamoja bila kujali mahitaji yaliyopo.

“Yaani walau kila baada ya dakika tatu basi lingekuwa linaingia tena, yale marefu yenye kubeba abiria wengi, lakini hii unakaa nusu saa, saa nzima ndio unaona basi inatutesa,” anasema Hellena George, mkazi wa Kibamba.

Wakati watumiaji wakisema hayo, Ofisa Uhusiano wa Dart, William Gatambi amesema mradi huo umekuwa wa mafanikio na miongoni mwayo ni kupunguza gharama na muda.

Alisema watu waliokuwa wanatumia wastani wa Sh20,000 za mafuta ya gari (binafsi) kwenda mjini na kurudi, sasa hutumia nauli Sh1,500 na foleni ikipungua saa tatu hadi dakika 45 kufika katikati ya jiji hilo.

Gatambi alifafanua kuwa mradi huo kwa miaka saba umekuwa kivutio na nchi 12 zimeutembelea kujifunza. Nchi hizo ni Zambia, Zimbabwe, Uganda, Kenya, Ethiopia, Senegal, Ghana, Rwanda, Angola, Botswana, Nigeria na Liberia.


Mkakati wa Serikali

Leo Jumatatu Januari 8, 2024 Mwananchi Digital ilizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa ambaye amekiri mradi huo kutomfurahisha tangu Septemba mosi mwaka jana alipoingia ndani ya ofisi hiyo.

“Hii ni wizara kubwa na ni wizara kama injini ya nchi, ina taasisi nyingine na ni wizara ambayo imetoa mamlaka kwa serikali za mitaa, wilaya na mikoa na wizara ambayo lazima ifanye jambo ili kama Taifa tuwe na utulivu.

Moja ya taasisi zilizoko chini yangu ni hii inayohusika na mwendokasi, Dart ambayo ndani yake kuna Udart,” amesema.

Waziri huyo amesema, “katika maeneo lazima nikiri ni hii, ina changamoto nyingi na nikiri bado hatujazifanyia kazi na ni sehemu ambayo naiangalia kwa jicho la kipekee, ili kupata mfumo wa kudumu, hasa mabasi ya mwendokasi, urasimu wa uendeshaji ambayo leo tuna mwendeshaji mmoja anayeshirikiana na Serikali.”

Amesema Serikali imejenga miundombinu ili kuweka ufanisi, ni lazima kuwepo na mwendeshaji zaidi ya mmoja, tofauti na ilivyo sasa.

Katika kulifanya hilo, amesema “kuna mapendekezo tumeyawasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mwenye dhamana ya Tamisemi, akiridhia tutatangaza kwa umma jinsi utakavyokuwa.”

Waziri Mchengerwa alisema miongoni mwa mambo aliyoyakuta alipoingia kwenye ofisi hiyo ni mapendekezo ya Serikali kuingia dhamana kukopa mabasi, “na gharama yake ni kubwa sana, yaani kama Sh1.5 bilioni kwa basi moja, na hii inaingia kwenye deni la Serikali, mimi kama waziri nimekataa.”

Katika toleo la kesho, tutaangazia mapato na marejesho, sakata la ubia, hofu na matumaini kwa wananchi