Mchengerwa ataka ushindani 'mwendokasi'

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed  Mchengerwa ameelekeza Uongozi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), kuongeza watoa huduma ili kuboresha huduma ya usafiri wa haraka kwa wananchi wa Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed  Mchengerwa ameelekeza Uongozi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), kuongeza watoa huduma ili kuboresha huduma ya usafiri wa haraka kwa wananchi wa Dar es Salaam.

 Waziri Mchengerwa ameyasema hayo Oktoba 24, 2023 kwenye ziara yake kwa Wakala huo ili kupata taarifa ya utendaji kazi wa Dart.

Amesema huduma ya mabasi yaendayo haraka ni muhimu sana kwa maisha ya wakazi wa Dar es salaam  na inatakiwa kusaidia kupunguza adha ya usafiri, hivyo uwepo wa mtoa huduma mmoja, kunamfanya azidiwe na hivyo kusababisha changamoto kwa baadhi ya maeneo.

Amesisitiza kuwa suala la kuongeza watoa huduma kwa sasa haliepukiki na linatakiwa kuwa kipaumbele kwanza kwa kuwa kuna njia mpya zitakazoanza hivi karibuni.

“Mtoa huduma mliyenaye kwa sasa ni Udart pekee, muda umefika sasa kuwa na mtoa huduma zaidi ya mmoja ili kuleta ushindani kwenye kutoa huduma za usafiri, ili wananchi wapate huduma bora," amesema Mchengerwa.

Pia Waziri Mchengerwa amewataka uongozi wa Dart kuimarisha mifumo ya kutoa taarifa mara tu panapoteka changamoto yeyote ya usafiri.

"Sijapenda kuendelea kuona vurugu kwenye vituo vya kusubiria mabasi, ni vyema panapotokea hitilafu kuwe na mifumo ya kutoa taarifa ili kupunguza manung’uniko kwa wananchi ambao huenda wamekaa pale muda mrefu kusubiria basi," amesema.

Awali, akitoa taarifa za utendaji kazi wa wakala huo, Mtendaji Mkuu wa Dart Dk Edwin Mhede amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya sita, uwezo wa kusafirisha abiria kwa siku umeongezeka kutoka abiria 90,000 mpaka 210,000 na umetokana  na maboresho makubwa yaliyofanyika kwa wakala huo.