Mfumuko wa bei wapanda kwa kasi ndogo

Tuesday June 08 2021
Mfumuko pc

Mkurugenzi wa sensa ya watu na takwimu za jamii,Ruth Minja akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 8,2021 kuhusu mfumuko wa bei.Picha na Jonathan Musa

By Jonathan Musa

Dodoma. Mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021 umebaki kuwa asilimia 3.3 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia Aprili, 2021.

Hali hiyo inatokana na kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021 zimebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Aprili, 2021.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Juni 8,2021 na Mkurugenzi wa sensa ya watu na takwimu za jamii, Ruth Minja wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Amesema mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Mei, 2021 kuwa sawa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioshia Aprili 2021 umechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizokuwa za vyakula kwa kipindi kilichoishia Mei, 2021 zikilinganishwa na bei za Mei, 2020.

Mkurugenzi huyo amesema, baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoongezeka bei kwa Mei, 2021 zikilinganishwa na bei za Mei, 2020 ni unga wa ngano kwa asilimia 4.1, nyama kwa asilimia 4.0, viazi mviringo kwa asilimia 7.5, mihogo mibichi kwa asilimia9.2, ndizi za kupika kwa asilimia 2.4, maharage kwa asilimia 5.0 na njegere kwa asilimia 7.1.

Katika hatua nyingine, ametaja baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizopungua bei kwa Mei 2021 zikilinganishwa na bei za Mei, 2020 ni gesi ya kupikia kwa silimia 1.2, mafuta ya taa kwa asilimia 6.0, petroli kwa asilimia 7.7, huduma ya malazi kwenye hoteli na nyumba za wageni kwa asilimia 5.8.

Advertisement

Amesema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021 umeongezeka kidogo hadi asilimia 4.9 kutoka asilimia 4.8 kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili 2021.

Kuhusu hali ya mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika mashariki kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021, kuna mabadiliko.Kwa mfano nchini Kenya, mfumuko wa bei ya mwaka ulioishia mwezi Mei 2021 umeongezeka hadi asilimia 5.87 kutoka asilimia 5.76 kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili,2021.

Upande wa Uganda, mfumuko wa bei uliofanyiwa marejeo kwa mwaka ulioshia mwezi Mei, 2021 umepungua hadi asilimia 1.9 kutoka asilimia 2.1 kwa mwaka ulioshia mwezi Aprili, 2021.

Advertisement