Mfumuko wa bei wazidi kushuka Julai

Muktasari:

  • Kupungua kwa bei za bidhaa zikiwemo samaki wabichi, mchele na mahindi na vinywaji baridi kumechochea kushuka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioshia Julai 2023, ikilinganishwa na mwaka ulioishia Juni 2023.

Dar es Salaam. Kupungua kwa bei katika baadhi ya bidhaa za chakula na vinywaji baridi kumefanya mfumuko wa bei wa Taifa kushuka hadi kufikia asilimia 3.3 katika mwaka ulioishia Julai 2023 ikilinganishwa na asilimia 3.6 katika mwaka ulioishia Juni 2023.

Hii ikiwa na maana kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Julai, 2023 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Juni, 2023.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonyesha kupungua bei kwa mwaka ulioishia Julai, 2023 ni ngano kutoka asilimia 4.8 hadi asilimia 3.1, mchele kutoka asilimia 17.0 hadi asilimia 11.4, mahindi ulitoka asilimia 22.9 hadi asilimia 7.2.

“Unga wa ngano ulipungua kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 1.5, unga wa mahindi ulipungua kutoka asilimia 30.5 hadi asilimia 16.5, mikate na vyakula vingine vya kuoka kutoka asilimia 11.6 hadi asilimia 11.1, samaki wabichi kutoka asilimia 8.9 hadi asilimia 6.1,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Vingine vilivyoshuka bei ni dagaa wabichi kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 14.5, dagaa wakavu kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 10.9, mafuta ya kupikia bei imepungua kwa asilimia 12.1, karanga mbichi kutoka asilimia 7.2 hadi asilimia 3.0, viazi vitamu bei imepungua kwa asilimia 5.1, viazi mviringo bei imepungua kwa asilimia 1.3.

“Maharage kutoka asilimia 33.5 hadi asilimia 28.3, choroko kavu kutoka asilimia 1.2 hadi asilimia 0.9, njegere kavu kutoka asilimia 8.6 hadi asilimia 5.9 na kunde kavu (kutoka asilimia 18.4 hadi asilimia 13.4.

Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Julai, 2023 pia umepungua hadi asilimia 6.1 kutoka asilimia 7.8 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2023.

Katika mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi umeongezeka hadi asilimia 2.2 kutoka asilimia 1.8 kwa mwaka ulioishia Juni, 2023.