Mgambo wavunja meza za wauza magazeti Dodoma
Muktasari:
Mgambo wa Jiji la Dodoma wamevunja meza za wauza magazeti na kuchukua magazeti yaliyokuwa yakiuzwa hivyo kusababisha taharuki kwa wafanyabiashara hao.
Dodoma. Mgambo wa Jiji la Dodoma wamevunja meza za wauza magazeti na kuchukua magazeti yaliyokuwa yakiuzwa hivyo kusababisha taharuki kwa wafanyabiashara hao.
Kuvunjwa kwa meza hizo kunatokana na operesheni ya Jiji la Dodoma ya kuwaondoa wamachinga wote waliopo katikati ya Jiji iliyoanza Oktoba 31 mwaka huu.
Wamachinga hao wamemishiwa katika soko la Machinga lililopo Bahiroad Jijini hapa.
Hata hivyo wauza magazeti hao walikuwa wakiendelea na biashara kama kawaida kabla ya jana kutoka agizo kwa Mkurugenzi wa Jiji Joseph Mafuru kwamba wanatakiwa kuondoa meza zao.
Mwananchi imeshuhudia leo Novemba 19 ,2022 saa nne asubuhi askari hao na baadhi ya watumishi wa Jiji hilo wakiwa katika gari lenye namba za usajili DFPA 6898 Nissan Double Cabin katika mtaa wa Independence Kata ya Majengo wakivunja meza ya muuza magazeti na kisha kuchukua magazeti kwa nguvu.
Mara baada ya kuivunja meza hiyo waliipakia katika gari pamoja na magazeti na kisha kuondoka nayo.
Muuzaji wa meza hiyo, Mwajuma Kisungura amesema anashangaa kuona mgambo hao wakimvunjia pamoja na kumchukulia magazeti yake.
“Nitarejesha nini jioni magazeti yangu yote wameyachukua kwanini wanatuonea hivi tumewakosea nini? Alihoji muuzaji huyo.
Rehema Ahmed amesema Jiji linajichanganya kwani wauza magazeti wanatakiwa kuwepo katikati ya Jiji.
Akilitolea ufafanuzi hilo,Mkurugenzi Mafuru amesema katika kuwahamisha wamachinga wamekutana na changamoto ya kutokuwepo kwa maeneo ya wauza magazeti, shoe shine na bodaboda.
Amesema wanaandaa maeneo yao katika soko la wamachinga na mpaka Jumatatu utaratibu utakuwa upo vizuri.
“Wakati wa zoezi hili tuliwaondoa wote kabisa lakini tutawarudisha kwa kuwapanga wiki ijayo kuanzia Jumatatu wasiwe na wasiwasi tutakuwa tumeishakamilisha vichanja vyao,”amesema Mkurugenzi Mafuru.