Mgogoro Ngorongoro pasua kichwa

Muktasari:

Joto la mgogoro wa eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), limezidi kupanda kutokana na kuongezeka kwa shinikizo la kuitaka Serikali iwaondoe wafugaji wa kijamii ya kimasai ambao idadi yao imekuwa ikizidi kuongezeka siku hadi siku na kutishia uhifadhi wa wanyama katika eneo hilo.

Dar es Salaam. Joto la mgogoro wa eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), limezidi kupanda kutokana na kuongezeka kwa shinikizo la kuitaka Serikali iwaondoe wafugaji wa kijamii ya kimasai ambao idadi yao imekuwa ikizidi kuongezeka siku hadi siku na kutishia uhifadhi wa wanyama katika eneo hilo.

Tayari kuna msuguano mkubwa juu ya hatima ya eneo hilo kutokana na madai kuwa baadhi ya watu wenye idadi kubwa ya mifugo wamewaajiri wafugaji wa kimasai watunze mifugo hiyo katika eneo hilo na hivyo kutishia uhai wa wanyama na mazingira.

Inadaiwa wamiliki hao wa mifugo wamekuwa wakitumia fedha zao kuendesha harakati za kuzuia watu kuondolewa kwenye eneo hilo wakihofia endapo hatua hiyo itatekelezwa watapoteza mifugo yao au mifugo hiyo itakosa malisho ya uhakika wanayoyapata hivi sasa.

Kuna baadhi ya watu wanaotaka wafugaji wa kimasai waendelee na shughuli zao kwakuwa ni sehemu ya vivutio duniani huku wengine wakitaka waondolewe ili kuinusuru hifadhi hiyo.

Hata hivyo Mwananchi lina taarifa kuwa huenda mgogoro huo ukapatiwa dawa na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa anayetarajia kufanya ziara katika eneo hilo na kuzungumza na viongozi na wakazi wa Loliondo na Ngorongoro.

Siku chache zilizopita akiwa bungeni Waziri Mkuu alisema anatarajia kufanya ziara hiyo baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa mkoa wa Arusha pamoja na wale wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Inakadiriwa kuwa wafugaji wa Kimasai wamekuwepo eneo la Ngorongoro na Loliondo mkoani Arusha tangu miaka ya 1700 na hata kabla ya hapo inaelezwa kuwa baadhi ya wafugaji walikuwa wakiishi kwenye hifadhi za wanyama.


Udhibiti wa watu

Agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka watendaji wa Serikali na taasisi zake kuangalia eneo la Ngorongoro lilifanyiwa kazi na mamlaka zilizo chini yake ikiwemo NCAA iliyoanza kudhibiti ongezeko la watu lakini hatua hizo zinachukuliwa kama manyanyaso na uonevu kwa wafugaji wa kimasai.

Tayari kampeni ya kutaka wafugaji waondolewe katika hifadhi hiyo zimezidi kushika kasi kuanzia kwa wanasiasa, wanaharakati, wabunge, vyombo vya habari na kwenye jumuiya mbalimbali za watu wanaojipambanua ni walinda na wahifadhi mazinngira.

Ziara ya Waziri Mkuu ndiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na wakazi wa maeneo husika ambao watajua mwelekeo wao


Waeleza matumaini yao

Mkurugenzi wa Shirika la kutetea wanawake na watoto(MIMUTIE) Rose Njilo alisema ziara ya Waziri Mkuu itasaidia kutatua mgogoro wa ardhi na wanataka katika utatuzi huo ulinde haki za wanawake na watoto.

James Moringe Diwani wa CCM Kata ya Alaitole iliyopo ndani ya mamlaka hiyo, alisema mgogoro uliopo Ngorongoro ni wa kutengenezwa kwa lengo la kuonyesha jamii ya kimasai ndio tatizo.

Mwenyekiti wa baraza la wafugaji Ngorongoro, Edward Maura alisema ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa itaanika ukweli na wanaamini tatizo ni uongozi wa Ngorongoro kushindwa kusimamia mamlaka hiyo.

Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria, Chuo Kikuu Cha Tumaini Makumira Dk Elifuraha Laltaika alisema wanataka mgogoro wa Loliondo umalizwe kwa maridhiano na mazungumzo ya pande zote.

Laltaika alisema ni muhimu mazungumzo ni muhimu kwani

Sheria iliyounda mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ya mwaka 1959 inatambua uwepo wa jamii ya kifugaji Ngorongoro.

Mwenyekiti wa viongozi wa mila Ngorongoro,Metui ole Shaudo alisema mazungumzo pekee ndio yataleta mwafaka kwa kuwa baada ya kuitunza hifadhi hiyo kwa miaka 60 leo wanaonekana sio watu muhimu.


Shaudo ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa CCM wilaya ya ngorongoro na mjumbe wa bodi ya mamlaka ya hifadhi Ngorongoro, alisema hawana mpango kuhama Ngorongoro.

Kiongozi huyo akiwa bungeni siku chache zilizopita aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii, kutoa semina kwa wabunge ambayo ilifanyika jana bungeni ili wawakilishi hao wa wananchi wajue kwa kina kiini cha mgogoro na kutoa mapendekezo ya njia bora ya kuutatua.


Bungeni moto

Baadhi ya wabunge waliochangia taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kipindi cha Januari, 2021 hadi Februari, 2022 walishauri wafugaji hao waondolewe hifadhini kwakuwa baadhi yao wanatumika kuhudumia mifugo ya matajiri wasioishi eneo hilo.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga ameishauri Serikali iwaondoe kwa nguvu kwa Wamasai katika eneo hilo.

“Kama kule Mtwara wakati watu wanagoma gesi iondolewe mpaka wajue watafaidikaje, mlipeleka vifaru vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, mkapeleka ma buldoser na vitu vingine kwamba iwe keki ya Taifa ili kila mmoja anufaike, tunaogopa nini? Au kwa sababu kuna matajiri? Kama mling’ata jongoo Mtwara, ng’ateni hayo majongoo sehemu nyingine.

Hata hivyo hoja hiyo ilipingwa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka aliyetetea kuwepo kwa wafugaji wa kimasai.

“Wamasai hawa wamekuwa waungwana kwa uhifadhi. Kama kuna kabila lililoonyesha uhifadhi na kuishi na wanyama katika eneo moja bila kuwadhuru ni tarafa ya Ngorongoro. Wananchi hao hao walitoa ardhi yote ya Serengeti, walitoa ardhi yote ya Tarangire, walitoa ardhi yote Ngorongoro, yote ya Manyara,” alisema Ole Sendeka.

Chimbuko la Wafugaji ndani ya Ngorongoro

Akichangia mjadala wa mgogoro wa Ngorongoro katika mtandao wa Twitter, Makamu Mwenyekiti wa Chadema anayeishi nchini Ubeligiji, Tundu Lissu alisema, wafugaji wamekuwepo kwenye hifadhi za wanyama kwa zaidi ya miaka 7000.

Lissu aliyewahi kufanyia utafiti eneo hilo mwaka 1996, alisema Wamasai wenyewe wamekuwepo hapo tangu karne ya 18 (miaka ya 1700).

“Kama wangekuwa ni waharibifu wa mazingira msingekuta mnyama hata mmoja katika eneo hili,” alisema.

Hata hivyo, alisema baada ya kuja kwa Wakoloni Wajerumani na baadaye Waingereza, ndipo walipoanza kuweka vikwazo.

“Kwa Tanganyika, uhifadhi ulianza na Wajerumani na baadaye wakaja Waingereza. Mwaka 1921, Ngorongoro ikatangazwa kuwa eneo tengefu la wanyamapori. Hata hivyo, Wamasai waliachwa ndani hifadhi wakiishi na wanyama.

“Mwaka 1930, uwindaji ukapigwa marufuku, lakini bado wenyeji hawakuonekana ni tatizo”

Taarifa hii imeandaliwa na Elias Msuya, Daniel Mjema na Mussa Juma.