Mgogoro wa Kanisa Anglikana wahamia kwa Askofu wa Mwanza

Muktasari:

  • -Maaskofu wawili wakataliwa kuchunguza
  • Maaskofu hao ni Michael Hafidhi kutoka Zanzibar na John Lupaa kutoka Dayosisi ya Manyoni Singida.

Nyumba ya Wahudumu wa Dayosisi ya Victoria Nyanza ya Kanisa la Anglikana wamewakataa maaskofu wawili waliokwenda kwa kujitolea kuchunguza mgogoro unaoendelea dhidi ya Askofu wa dayosisi hiyo, Boniface Kwagu.

Maaskofu hao ni Michael Hafidhi kutoka Zanzibar na John Lupaa kutoka Dayosisi ya Manyoni Singida.

Askofu Kwangu amekuwa kwenye mgogoro na viongozi wa kanisa hilo huku baadhi ya waumini wakimtuhumu kutumia madaraka yake vibaya kwa kukiuka katiba ya kanisa.

Akizungumza katika ibada maalumu jana, mwenyekiti wa nyumba ya wahudumu, Mchungaji Andrea Kashirimu alisema wamefikia hatua hiyo baada ya maaskofu hao kukiuka muongozo na hadidu za rejea zilizotumwa Agosti 2 na Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Jacob Chimeledya.

Alisema taarifa za kuwakataa waliitoa polisi na jeshi hilo kuamuru watu hao waondoke.

Lakini Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema, “Sisi hatuwezi kuingilia migogoro ya kanisa. Tunachofanya ni kuhakikisha hakuna ugomvi kwa hiyo tulisema hakuna kufunga milango waache waumni waendele na ibada, hatutaki kuona vurugu kwenye mkoa wetu.”

Walipotafutwa kwa simu Askofu Hafidhi alisema atafutwe baadaye kwani yupo kwenye kikao huku Askofu Lupaa akituma ujumbe mfupi kwamba atafutwe baada ya saa tatu yupo kwani pia kwenye kikao.

Kashirimu alidai kuwa maaskofu hao badala ya kuchunguza mgogogro huo kama hadidu zinavyoelekeza, walisababisha uchochezi na vurugu maeneo mbalimbali ndani ya dayosisi hiyo katika maeneo ya Sengerema, Magu, Ngudu wakati wakifanya vikao mbalimbali.

“Kwa hiyo sasa tunaunga mkono uamuzi wa nyumba ya maaskofu ambao waliufanya Julai 6, walipokaa na kumshauri Askofu Kwangu kustaafu kwa hiari ili kulinda heshima yake ndani na nje ya kanisa,” alisema mchungaji Kashirimu.

Miongoni mwa hadidu za rejea walizopewa na askofu mkuu ni kukutana na makundi mbalimbali kuona chanzo na kiini cha mgogoro, kuchunguza malalamiko ya kutofuatwa kwa katiba, kuchunguza malalamiko juu ya askofu na uhusianao wake na wamisionari, wachungaji na waumini na kuchunguza malalamiko kubadili taratibu za ibada, fedha na kuchunguza malalamiko mengine.

Mchungaji wa Parishi ya Sengerema Mjini, Dk Elisha Ndema alisema, “Walipokuja kwenye kikao walisababisha waumini kuwafungia mlango wasiingie ndani na kutaka kupigwa baada ya kuonekana hawafuati taratibu na kuunda makundi katika Parishi ya Bomani.”

Askofu Chimeledya aliwaagiza maaskofu hao kuchunguza, kubaini chanzo cha migogoro na kumshauri hatua za kuchukua bila wao kufanya uamuzi wowote.