Mgogoro wa kugombea mgodi madini ya Tanzanite wapatiwe ufumbuzi

Ofisa madini mkazi (RMO) Mirerani mhandisi Mernad Msengi akizungumza na waandishi wa habari wakati akisoma taarifa ya mgogoro wa kugombea mgodi wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Wachimbaji wawili Njake Enterprises na Patrick Miroshi walikuwa wanagombea mgodi wa madini ya Tanzanite uliopo kitalu C Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Mirerani. Sakata la mgogoro wa kugombea mgodi wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kati ya kampuni ya Njake Enterprises na Patrick Miroshi umemalizika kwa kuonyesha mgodi huo ni mali ya kampuni ya Njake.

Ofisa madini mkazi wa Mirerani (RMO) mhandisi Mernad Msengi akizungumza na Mwananchi digital leo alhamisi Machi 30 amesema eneo lenye mgogoro lipo ndani ya leseni ya Njake.

Mhandisi Msengi amesema kwa mujibu wa matakwa ya sheria ya madini, mgodi huo upo kwenye leseni namba PML 00416SMN ya Japhet Lema inayomilikiwa na kampuniya Njake Enterprises.

“Wahusika wa pande zote mbili walifika eneo hilo na kukubaliana upimaji ulivyofanyika kupitia vifaa vya kitaalam zaidi vyenye ufanisi tofauti na vifaa vya GPS ya kawaida,” amesema.

Amesema kwa upande wa mipaka ya Patrick Miroshi vipimo vimeonyesha kuwa mgodi huo upo nje ya eneo la umiliki wake kwa umbali wa mita 1.9 kulingana na mipaka ya leseni ya awali. 

Amesema wamependekeza kuwa wachimbaji hao Miroshi na Njake wachimbe katika mipaka ya leseni zao na sivyo vinginevyo ili kuepusha na kumaliza migogoro inayojitokeza.

“Pande zote zizingatie sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji madini na eneo tengefu ili kuwepo uchimbaji wa tija kwa maendeleo ya sekta ya madini na Taifa kwa ujumla,” amesema.

Meneja wa mmiliki wa awali wa mgodi huo Mangoshi Seleman ambaye aliuuza mgodi huo kwa Njake Enterprises, Mohamed Mughanja amesema uamuzi huo umetenda haki.

“Sisi tuliiuzia mgodi huu Kampuni ya Njake Enterprises jirani yetu Miroshi akawa analalamika kuwa amedhulumiwa mgodi jambo ambalo siyo kweli na Wizara imetoa majibu mazuri,” amesema Mughanja.

Meneja wa Kampuni ya Njake Enterprises, Hassan Salehe amesema wanaridhika na uamuzi huo kwani kabla ya kununua mgodi huo walichunguza kwanza mmiliki halali ndipo wakanunua.

Hata hivyo, uongozi wa Mgodi wa Miroshi umedai kuwa hauridhiki na uamuzi huo hivyo watatafuta wataalamu huru wenye vifaa stahiki ili kurudia upimaji huo.