Mgogoro watishia uhai wa wafugaji, watumishi

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo), Profesa Daniel Mushi

Mwanza. Vitendo vya wafugaji kuvamia na kulisha mifugo ndani ya shamba la Serikali Mabuki, vimezua uvunjifu wa amani baada ya kuibuka mapambano kati ya wavamizi na wafanyakazi wa shamba hilo.

Shamba la Mabuki lenye ukubwa wa ekari zaidi 25 lilianzishwa mwaka 1967 na hadi Desemba, 2023 lilikuwa na ng’ombe 2,845, kati yao 500 ni mitamba iliyopelekwa na Serikali chini ya mkakati wa kuongeza uzalishaji. Shamba hilo pia lina mbuzi wa maziwa 356, nyati maji 60 na punda 150.

Katika utekelezaji wa mipango ya Serikali, ikiwamo mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT Life) unaotoa mafunzo kwa vitendo kwa vijana, zaidi ya vijana 55 wamepelekwa kwenye shamba hilo kujifunza mbinu bora za ujasiriamali, ufugaji na unenepeshaji mifugo.

Hata hivyo, mipango hiyo inatatizwa na uvamizi wa wananchi wa vijiji jirani ambao si tu huingiza mifugo ndani ya eneo la shamba, bali pia huwashambulia kwa silaha za jadi askari na wafanyakazi wa shamba hilo wanapojaribu kuzuia au kukamata mifugo iliyovamia.

Meneja wa shamba hilo, Lini Mwalla amesema vitendo vya uvamizi vinaongezeka kwa wafugaji kuingiza na kuchunga mifugo kwa idadi kubwa zaidi.

“Tunalazimika kutumia askari wetu na watumishi kufanya doria ambazo pia zinaibua migogoro na wakati mwingine mapigano kati ya watumishi wa shamba na wafugaji wanaolazimisha kuingiza mifugo na kuchunga ndani ya eneo la shamba kimabavu,’’ amesema Mwalla.

Akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo), Profesa Daniel Mushi hivi karibuni, Mawalla amesema ongezeko la idadi ya mifugo ya wananchi inayochungwa ndani ya shamba hilo si tu inamaliza malisho, bali pia huharibu miundombinu ya shamba na kueneza magonjwa ya kuambukiza ya mifugo.

“Kumewahi kutokea mashambulizi ya kukata kwa panga mifugo na askari wetu wakijaribu kuingilia kati nao wanashambuliwa,” amesema Mwalla akiomba msaada wa Serikali kuingilia kati suala hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paul Chacha ameunga mkono maelezo hayo akisema uongozi wa Serikali ulifikia hatua ya kuwawekea ulinzi maalumu viongozi wa shamba baada ya kuwepo tishio la usalama.

"Kuna wakati tulimpa ulinzi meneja wa shamba kwa sababu kulikuwa na tishio la watu kutaka kumdhuru. Kuna askari mmoja alishambuliwa kwa silaha za jadi wakati yeye na wenzake wanazuia mifugo inayoingizwa shambani kinyume cha sheria,’’ amesema Chacha.

Kamati ya usalama ya Wilaya ya Misungwi kwa kushirikiana na uongozi wa shamba ilipitisha kiwango cha faini ya Sh100,000 kwa kila ng’ombe anayekamatwa ndani ya shamba, lakini kiwango hicho kikubwa cha faini hakijasaidia na wafugaji bado wanaingiza mifugo na kutumia mabavu kuzuia isikamatwe.


Vurugu za kila mara

Februari 16, 2020, John Lugata, mkazi wa kijiji cha Misasi alifariki dunia baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari polisi waliofika eneo la shamba hilo kutuliza ghasia zilizoibuka kati ya wafanyakazi na wafugaji walioingiza mifugo ndani ya eneo la shamba la Serikali.

Watu wawili kutoka upande wa wafugaji walijeruhiwa katika vurugu hizo zilizoibuka wakati wafugaji wakizuia mifugo yao iliyokutwa ndani ya shamba la Serikali kukamatwa, ili itozwe faini ya Sh100,000 kwa kila mfugo.

Kwenye tukio hilo, askari polisi wawili walijeruhiwa kwa kushambuliwa na silaha za jadi yakiwamo mawe yaliyokuwa yakirushwa kwa kutumia kombeo.

Aprili 2023, mwili wa Juma Shilatu (40), mkazi wa Kijiji cha Mwanangwa, Kata ya Mabuki ulikutwa eneo la shamba la mifugo Mabuki, ikidaiwa walinzi wa shamba hilo ndio walihusika kumshambulia baada ya kumkuta akichunga mifugo ndani ya eneo la shamba, madai ambayo yalikanushwa.


Diwani aomba uzio

Diwani wa Kata ya Mabuki, Malale Lutonja amekiri uwepo wa migogoro ya mara kwa mara kati ya wananchi wanaoishi vijiji jirani na watumishi wa shamba hilo, akidai hali imekuwa mbaya zaidi baada ya uongozi wa shamba kuanza kuwatumia walinzi kutoka Suma JKT, aliodai hukamata hata mifugo ya wananchi inayokutwa nje ya mpaka wa shamba kwa lengo la kuwatoza faini.

“Naiomba Serikali ijenge uzio kuzunguka eneo lote la shamba kumaliza migogoro ya mifugo ya wananchi kuingia eneo la shamba na kutozwa faini ya Sh100,000 kwa kila mfugo,’’ amesema.

“Wafugaji hawana maeneo ya malisho, wakati mwingine hujikuta wameingia ndani ya eneo la shamba, ambalo halina alama ya mipaka wala uzio. Naiomba Serikali ijenge uzio kwenye mipaka ya shamba hili kumaliza mgogoro huu unaosababisha madhara kwa pande zote,’’ amesema.


Waliotozwa faini

Malando Shija, mmoja wa wafugaji wanaoishi vijiji vinavyopakana na shamba la Mabuki ameshauri malipo yote ya faini ya Sh100,000 kwa kila mfugo unaokamatwa ndani ya shamba hilo yafanyike kwa kuzingatia kanuni ya malipo serikalini kwa wanaolipa kupewa stakabadhi.

“Kabla ya mwaka 2018, malipo ya faini kwa kila ng’ombe anayekamatwa ndani ya eneo la shamba ilikuwa Sh20,000 na hakukuwa na mgogoro mkubwa kati ya uongozi wa shamba na wafugaji. Hali imekuwa mbaya zaidi kuanzia mwaka 2018 baada ya faini kuongezeka hadi Sh100,000 kwa kila ng’ombe anayekamatwa. Kibaya zaidi hakuna risiti ya malipo,’’ amesema Shija.

Mmoja wa wafugaji hao, Maduhu Petro ameshauri uongozi wa shamba hilo, serikali za vijiji na wataalamu wa ardhi wa Halmashauri ya Misungwi kuweka alama za mpaka katika eneo lote la shamba kuondoa mwingiliano unaotokana na mpaka kutojulikana.

“Kwa sasa ni vigumu mtu, hasa watoto wanapochunga, kujua mpaka kati ya shamba la Serikali Mabuki na vijiji jirani kwa sababu hakuna alama. Hili ni tatizo linalotakiwa kutatuliwa na Serikali kwa kushirikisha pande zote. Mipaka iwe wazi na ijulikane kwa wafugaji na wafanyakazi wa shamba la Mabuki,’’ amesema Petro.


Hatua kuchukuliwa

Ombi la Petro limesikika kwa  Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla na ameuagiza uongozi wa Serikali wilayani Misungwi kushirikiana na uongozi wa shamba kwa ulinzi wa Polisi, kweke alama zinazoonekana kirahisi katika mipaka yote ya shamba hilo.

"Namwelekeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ataleta kikosi cha askari wa kutuliza ghasia (FFU) na kikosi hicho kitakaa hapa kufanya doria kuhakikisha hakuna mtu anayeingia eneo la shamba hili kinyume cha sheria,’’ ameagiza Makalla.

Amesema kamwe Serikali haitaruhusu baadhi ya watu kujimilikisha eneo la shamba la Mabuki na kuligeuza eneo la malisho ya mifugo yao kinyume cha sheria.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Daniel Mushi amesema Serikali itatumia vyombo na mamlaka yake kulinda shamba hilo na miundombinu yake kutokana na umuhimu wake katika kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kutengeneza fursa za ajira kupitia sekta ya kilimo.

“Shamba hili ni miongoni mwa vituo atamizi ambako vijana walioko kwenye BBT Life wanapata mafunzo ya ujasiriamali, ufugaji na unenepeshaji mifugo. Tuna wajibu wa kupalinda kwa sababu ni eneo muhimu,” amesema Profesa Mushi.