Mgomo wa madaktari Kenya, wagonjwa wakimbilia hospitali za Tanzania

Miongoni mwa wagonjwa wakishuka kwenye gari wakitokea mpakani mwa Kenya na Tanzania wakifuata matibabu katika Hospitali ya Ngoyoni iliyopo Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro baada ya madaktari nchini humo kuingia kwenye mgomo. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Mgomo wa madaktari wa hospitali za umma nchini Kenya ulianza Machi 15, 2024 ukihusisha wanachama wa Umoja wa madaktari, wafamasia na madaktari wa meno (KMPDU), unaotajwa kuwa na wanachama karibu 7,000 nchini humo.

Rombo/Arusha. Wagonjwa raia wa Kenya, wameanza kuingia nchini Tanzania kutafuta huduma za matibabu kutokana na mgomo wa madaktari na maofisa tabibu wa hospitali za umma nchini Kenya unaoendelea, huku idadi ya wagonjwa ikiendeelea kuongezeka.

Uchunguzi wa Mwananchi Digital umebaini uwepo wa ongezeko la wagonjwa kutoka Kenya katika hospitali zilizopo jirani na mpaka wa Kenya na Tanzania katika wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro na wilaya ya Longido katika mkoa wa Arusha.

Wakati hali katika hospitali za wilaya hizo mbili ikiwa hivyo, uongozi wa Serikali mkoani Mara umekaa mguu sawa kufuatilia wagonjwa watakaovuka mpaka na kuingia mkoani Mara kutoka Kenya, kwa lengo la kutafuta huduma ya matibabu.

Mgomo wa madaktari wa hospitali za umma nchini Kenya ulianza Machi 15, 2024 ukihusisha wanachama wa Umoja wa madaktari, wafamasia na madaktari wa meno (KMPDU), unaotajwa kuwa na wanachama karibu 7,000 nchini humo.

Miongoni mwa madai ya madaktari hao ni kushinikiza walipwe malimbikizo ya mishahara yao, kuajiriwa kwa mkataba kwa madaktari wanafunzi, kukatiwa bima ya matibabu kwako na wategemezi wao na kuchelewe kulipwa mshahara.

Mbali na madaktari hao, mgomo huo ulioingia wiki ya tatu umeongezewa nguvu na maofisa tabibu ambao wamejiunga na mgomo huo na kuvuruga huduma za matibabu katika hospitali za umma katika eneo lote la nchi hiyo.

Itakumbukwa huo ni mgomo wa pili baada ya ule wa 2016/2017 ulidumu kwa siku 100  ukienda sambamba na mgomo wa wauguzi 45,000 nchi nzima na maofisa tabibu ambao wenyewe ulidumu kwa siku 20.

Kama ilivyo mgomo wa sasa wa baadhi ya raia wa Kenya kuingia nchini, mwaka 2017 pia ulishuhudiwa raia wa nchi hiyo wakiingia nchini akiwemo Bahati Tabu (37) aliyejifungua pacha la watoto watano katika Hospitali ya Faraja, wilayani Himo mkoani Kilimanjaro.

Mgomo huo uliohusisha madaktari na wauguzi zaidi 5,000 wa hospitali za Serikali nchini humo, ulianza Desemba 6,2016 na inaelezwa zaidi ya wagonjwa 40 walipoteza maisha, hivyo Bahati akaamua kukimbilia Tanzania ili kujifungua.


Hali ilivyo sasa Kilimanjaro

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Digital baada ya kufika katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma pamoja na Hospitali ya Ngoyoni wilayani Rombo, umebaini uwepo wa baadhi ya wagonjwa waliotoka Kenya kupatiwa huduma katika hospitali hiyo.

Baadhi ya wagonjwa waliokuwepo hospitalini hapo ambao wametokea Loitokitok nchini Kenya, wanasema wameamua kufuata huduma hiyo Tanzania, kutokana na mgomo unaoendelea nchini kwao.

Mmoja wa wazazi aliyemfikisha mwanaye hospitalini hapo, ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema alitumia  usafiri wa bodaboda akitokea nchini humo, ili kunusuru maisha ya mwanaye kwa sababu huduma hospitali binafsi Kenya ni ghali.

"Tumekuja hapa kwa sababu nchini kwetu kuna mgomo wa madaktari na kwa sababu sisi na Tanzania ni majirani tukaamua kukimbilia huku kunusuru maisha ya ndugu zetu, ni umbali mrefu nimetumia zaidi ya Sh15,000 kwa bodaboda hadi kufika hapa,” amesema.

Raia huyo wa Kenya ameongeza kusema:-"Licha ya gharama kubwa za usafiri hadi kufika hapa, mtoto wangu amepewa huduma ya kwanza, lakini kutokana na hali yake kutokuwa nzuri, tumepewa rufaa kwenda Hospitali ya KCMC kwa matibabu makubwa zaidi.”

Naye mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo, ambaye hakutaka jina lake liandikwe amesema wagonjwa kutoka nchi jirani wapo, lakini idadi yao si kubwa kama ilivyotokea kwenye mgomo uliotokea Desemba 2016 hadi 2017.

"Wagonjwa wapo lakini si wengi sana kama kipindi kilichopita cha mgomo kwenye hii nchi jirani, kipindi kile wagonjwa walifurika na wengine waliletwa hadi na mabasi kuja kutibiwa hapa hali ambayo tulikuwa tulifanya kazi usiku na mchana,”amesema.

Akizungumzia ongezeko la wagonjwa kutoka nchini Kenya, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Deogratius Maruba amesema baadhi ya hospitali za wilaya hiyo wameongezeka tofauti na ilivyokuwa hapo awali kabla ya mgomo huo.

"Kwenye baadhi ya vituo kumekuwa na ongezeko la wagonjwa mara mbili ya wagonjwa waliokuwepo kutoka nchini Kenya hasa katika hospitali ya Ngoyoni," amesema mganga huyo.

Akizungumzia hilo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Jairy Khanga amekiri kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma vya mpakani, hususani kwa wilaya ya Rombo huku akisema ongezeko zaidi ni la wajawazito na watoto.

"Ni kweli kuna ongezeko kubwa na hii taarifa nimeipata Halmashauri ya Wilaya ya Romb, wajawazito wengi na watoto wamekuja kupata huduma kwenye hospitali na vituo vyetu, lakini hili ongezeko halijaathiri utoaji wa huduma huku kwetu.

"Serikali haiwezi kujipanga kwa issue ya Kenya lakini tumeliona hili, kuongezeka kwa wagonjwa kutoka kwa jirani zetu Kenya na mkakati ambao tunataka tuende nao sasa ni lazima hawa wenzetu wachangie huduma za afya ambazo huku hatuchangii,” amesema na kuongeza;

“Bila hivyo rasilimali ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya watu wetu hazitaweza kutosha. Gharama ambazo hazitozwi kwa watanzania ikiwemo wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, kwa hawa wenzetu tutawatoza,”amesisitiza.

“Lakini pia tunataka kushirikiana na watu wa uhamiaji, ili kuona kwamba hao watu wanapokuja kupata huduma kama wamepitia kwenye njia sahihi za kuingia nchini."

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi upande wa Horohoro mkoani Tanga, hakuna dalili za wagonjwa kuingia nchini.


Hali ilivyo Longido

Kama ilivyo wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, Kaimu Mkuu wa Idara ya afya, ustawi wa jamii na lishe Wilaya ya Longido, Dk Mathew Majani naye amesema kwa sasa katika Kituo cha afya Orendeke hali ya wagonjwa wanaotoka nchini Kenya imeongezeka.

Eneo la Namanga wilayani Longido ni mpaka kati ta Tanzania na Kenya ambapo kwa mujibu wa Kaimu huyo amesema licha ya kutokuwa na takwimu sahihi, ila idadi ya wagonjwa kutoka nchini humo imeongezeka tangu kuanza kwa mgomo huo Machi 2024.

"Ikizingatiwa hapa ni eneo la mpakani kwa taarifa nilizonazo zinaonyesha idadi ya wagonjwa wanaotoka nchini Kenya kuja kupata huduma za kiafya hasa kituo cha Orendeke imeongezeka tofauti na ilivyokuwa awali,"amesema Dk Majani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Marko Ng'umbi amesema kwa asili watu wa eneo hilo ambao ni raia wa Kenya na wale wa Tanzani huingiliana.

Amesema raia wa Kenya hufika kupata huduma upande wa Tanzania, halikadhalika wa Tanzania huingia Kenya kupata huduma mbalimbali zikiwemo za afya na masoko.

"Kiukweli baada ya mgomo wa madaktari na wauguzi nchini Kenya, bado hatujaangalia kama kumekuwa na ongezeko zaidi la wagonjwa, nadhani kwa sasa tutaanza kufuatilia na kuliangalia hilo, ili kubaini kama wameongezeka au vipi,” amesema.


Mara nao wakaa mguu sawa

Wakati madaktari na wauguzi nchini Kenya wakigoma kutoa huduma kwa wagonjwa wakishinikiza kuboreshewa maslahi yao, uongozi wa Mara umekaa mguu sawa kufuatilia wagonjwa watakaovuka mpaka kuingia mkoani humo kwa lengo la kupatiwa matibabu.

Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Tarime Vijijini, Joseph Mziba na kwamba tayari wasimamizi wa vituo vya afya vilivyopo mpakani wilayani humo wameshapewa muongozo wa hatua za kuchukua wakibaini kuna mgonjwa aliyeingia kutoka Kenya.

“Hakuna kituo chochote kilichoripoti kuwepo ongezeko la wagonjwa hasa kutoka nchini Kenya, tunaendelea kufanya ufuatiliaji kubaini kama wapo, lakini naamini wagonjwa hao wanamezwa na vituo binafsi vya afya,” amesema Dk Mziba katika mahojiano hayo.

Amesema uwepo wa mwingiliano wa jamii inayoishi kuzunguka mpaka huo ni miongoni mwa sababu za msingi zinazotakiwa kuongezewa umakini na ufuatiliaji wa karibu, huku akiahidi kutoa taarifa itakapobainika kuna wagonjwa kutoka Kenya wameingia nchini kutafuta matibabu.

“Kama wanaweza kuona kuna dalili zozote za wagonjwa kuongezeka tumewasisitiza watupatie taarifa, pia tumewasisitiza kukagua sifa za wagonjwa ikiwemo lafudhi na muonekano iwapo ni wa Watanzania wakibaini kwamba si Watanzania, basi watoe taarifa,” amesema Dk Mziba.

Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi), Janeth Joseph na Florah Temba (Rombo), Janeth Mushi (Arusha) na Mgongo Kaitira (Mwanza).