Mhandisi mradi wa EACOP akutwa amefariki hotelini

Muktasari:

Mhandisi mshauri katika mradi wa mradi wa Bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) Uganda-Tanga kwa upande wa Tanga ambaye ni raia wa Afrika Kusini, amakutwa amefariki dunia katika chumba cha hoteli aliyokuwa amepanga kwa muda wa mwezi mmoja na nusu.

Tanga. Raia wa Afrika Kusini, Mhandisi Abraham Jacobus (47) amekutwa akiwa amefariki dunia chumbani katika hoteli ya Tanga beach jijini Tanga.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na  Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,  David Chidingi ni kuwa mtaalamu hiyo alifariki usiku wa kuamkia leo Jumapili Mei 22, 2022.

Taarifa zimemesema kuwa Abrahamu ana mwezi mmoja na nusu akiishi katika hoteli hiyo na kwamba umauti umempata usiku wa kuamkia leo akiwa peke yake chumbani.

Raia huyo wa Afrika Kusini alikuwa anafanya kazi katika mradi wa bomba la mafuta kwa upande wa Tanga kama mhandisi mshauri.

"Dereva wake wakati alipomfuata kwa lengo la kumchukua kuelekea kazini alimpigia simu kwa muda mrefu haikupokelewa na ndio akatoa taarifa kwa uongozi wa hoteli na wakafungua na kumkuta amefariki na wakatoa taarifa polisi " amebainisha Kaimu Kamanda Chidingi.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini alikuwa na tatizo la athma na kwamba mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo kwa uchunguzi zaidi.

"Marehemu ni raia wa kigeni hivyo kuna taratibu ili kufanya uchunguzi wa kina na kubaini hasa chanzo cha kifo chake ".amesema Kaimu kamanda huyo.