Mhifadhi: Mbwa Mayele katusaidia kuwaona simba wavamizi

Mbwa Mayele anayesifika katika kata ya Maboga Wilayani Iringa kwa kuonyesha uelekeo wa Simba na watoto wake na askari wa Wanyama pori kuthibitisha hilo.

Muktasari:

Siku chache baada ya Simba kuvamia vijiji mbalimbali katika Kata ya Maboga wilayani hapa, doria iliyofanywa kwa usaidizi wa mbwa alinayeitwa Mayele, yatajwa kuleta mafanikio baada ya kuonekana kwa Simba.

Iringa. Siku chache baada ya Simba kuvamia vijiji mbalimbali katika Kata ya Maboga wilayani hapa, doria iliyofanywa kwa usaidizi wa mbwa alinayeitwa Mayele, yatajwa kuleta mafanikio baada ya kuonekana kwa Simba huyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Afisa Uhifadhi daraja la pili Said Stuard amesema mbwa hao waliungana na Askari wa Wanyamapori toka siku ya kwanza ya doria. “…uwezo wa mbwa Mayele umetusaidia kuona njia aliyopita Simba na watoto wake, na tumefanikiwa kuwaona,” amesema na kuongeza;

“Alikuwa na watoto wadogo katika msitu, njia inayoelekea kijiji cha Makongati japokuwa tumeshindwa kumdhibiti kutokana na mazingira, maana kuliwa na wananchi; hivyo kwa kuhofia usalama wao tukashindwa.”

Hata hivyo Mhifadhi huyo amewashukuru wananchi kwa kujitolea nguvu zao lakini pia kuwatoa mbwa wao ili kumsaka Simba huyo mwenye watoto.


Kwa upande mwingine amewataka wananchi hao kuwa watulivu na kutotembea katika mazingira yaliyojificha kwani ni hatari na kwamba hata Simba wakionekana, inakuwa vigumu kuwadhibiti juu ya uwepo wa watu.

Juhudi za muda mrefu zilifanywa ili kudhibiti suala la uvamizi wa Simba hao, ikujumuisha ushirikiano kati ya Serikali, wataalamu wa uhifadhi, na jamii; pamoja na kuzinduliwa kwa programu za kuelimisha wananchi namna bora za kuwaepuka na kujilinda dhidi ya wanyama hao hatari.

Imeelezwa kuwa mara baada ya kuanza doria, Mayele alipewa jukumu la kuongoza kikosi kilichokuwa kinajumuisha Askari Wanyamapori na baadhi ya wananchi, ambapo alionyesha uwezo wa kipekee katika kufuatilia harufu na kuelekeza njia ya walipo Simba hao.

Walipofika eneo ambalo Simba walikuwa wamejificha, walikuwa na tahadhari kubwa kwa sababu ya uwepo wa watu na walihofia kujeruhi au kusababisha madhara kwa watu waliokuwepo maeneo hayo hali hiyo iliwafanya washindwe kuwaua simba hao.

Mwanakijiji huyo amejipatia sifa kwa ushujaa wa mbwa wake ambaye sasa kajipatia umaarufu mkubwa kwa uwezo wake katika kusaidia maficho ya simba hao.

Nae Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kiponzelo Daines Kunzugala amesema bado wanafanya jitihada ili kumaliza tatizo hilo linalowafanya kuishi kwa hofu.

"Wananchi wengine waelewa na wamesimamisha shughuli zao zote za kiuchumi lakini Kuna baadhi Yao bado hawafuati maelekezo yanayotolewa ya kutulia majumbani hivyo elimu bado inatolewa," amesema Kunzugala 

Petro Msilu Mkazi wa Kijiji cha Kiponzelo amesema mbwa wake (Mayele) anauelewa wa ajabu hivyo aliamua kumtoa ili asaidie katika kazi ya kuwata Simba hao ambao wamekuwa wakiua ng'ombe, na wanyama wengine wa kufugwa.

"Toka mdogo Mayele namfundisha mambo ya msingi na ana uelewa wa ajabu sio kama mbwa nyingine," amemsifia.