MIAKA 2 BILA JPM: Chato ya sasa si ile ya zamani

Aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alipokwenda kumtembelea nyumbani kwake Chato mkoani Geita. Picha na Maktaba

Safari ya Dunia kulizunguka jua ni juu ya uwezo wa binadamu. Basi majira yanabadilika, kutahamaki mwaka mwingine. Dunia inavyojizungusha yenyewe kwenye mhimili wake, usiku unaingia, nuru ya jua inaangaza, siku nyingine. Kisha wiki na mwezi, inakuwa miezi.

Imetimia miaka miwili tangu dunia ilipotangaziwa kifo cha aliyekuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli. Inakuwa rahisi kutazama nyuma, yale aliyoyasimamia na mwendelezo wake baada ya yeye kupata hifadhi kwenye tumbo la ardhi.

Magufuli alifariki dunia kipindi ambacho mji aliozaliwa wa Chato, ukitoa ahadi kubwa ya ukuaji wa kiuchumi. Ilikuwepo mpaka mipango ya kuipandisha hadhi Chato, kutoka wilaya kuwa mkoa. Miaka miwili baada ya kifo chake, Chato ni ya kuishikia tama. Inasikitisha. Kituo Kikuu cha Mabasi Chato, kimezeeka ndani ya muda mfupi, kabla hata hakijaanza kutumika. Hakuna shughuli za usafirishaji zenye kuendelea. Fremu za biashara kwenye kituo ziko wazi. Chato hakuna mzunguko wa kifedha.

Huenda hali ingekuwa tofauti kama Magufuli angekuwepo. Nyasi zimeota hadi kufunika sakafu za marumaru. Fedha nyingi zilizotumika kujenga kituo ni hasara tupu. Yapo majengo hata mbao zilizowekwa kama nyenzo za ujenzi, hazijatolewa. Hili lisingewezekana mbele ya uso wa Magufuli. Wapo wangekiona cha moto.

Tawi la Benki ya CRDB Chato, lilifungwa muda mfupi baada ya Magufuli kufariki dunia. Naikumbuka hotuba ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Charles Kimei, siku ya uzinduzi wa tawi hilo.

Kimei alisema, wataalamu wa benki walifanya utafiti mara mbili na kutoa ripoti kuwa mzunguko wa kibiashara haukushawishi kufungua tawi Chato.

Hata hivyo, Magufuli alipopewa majibu hayo, alisema naye angefanya utafiti wake. Magufuli akarejesha majibu CRDB kuwa mzunguko ulikuwepo na ingewezekana kufungua tawi. Ndipo, CRDB kupitia utafiti wa Magufuli, walipofungua tawi Chato. Likaanza kazi. Baada ya kifo chake, likafungwa.

Kauli ya Kimei kuwa tawi lilifunguliwa kwa utafiti wa Magufuli, ilitoa tafsiri kwamba CRDB walilazimishwa kuwekeza Chato, wakati mazingira ya kibiashara hayakushawishi. Miaka miwili baada ya kifo cha Magufuli, hakuna shaka tena kwamba benki ilifunguliwa kwa nguvu ya mamlaka yake.

Vuta picha, Magufuli yule tunayemfahamu, Rais wa Tanzania, ghafla anafufuka leo na kuona Chato hakuna benki tena. Kituo cha mabasi ndege wamefanya makazi. Chato yake aliyotumia nguvu kuiinua kiuchumi, imekuwa duni mno.

Uwanja wa Ndege wa Chato ndege zimekuwa adimu. Mashirika hayafanyi safari kwa kuwa hakuna abiria. Wanaokwenda Geita, watashuka Uwanja wa Ndege wa Mwanza na kupanda magari hadi mwisho wa safari. Wengine hushuka Uwanja wa Ndege Bukoba na kupanda magari.

Kutokana na abiria kuwa wachache wenye kutumia Uwanja wa Ndege wa Chato, gharama kwa abiria ni kubwa, ndio maana wapo ambao huamua kutumia Uwanja wa Ndege wa Mwanza, wengine Bukoba, kulingana na ukaribu wa anapoelekea kutokea uwanja wa ndege husika.

Aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, wakati akipinga bungeni ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato, alisema kuwa ni hatari sana Serikali kuwekeza kwa matakwa ya kiongozi, kwani akiondoka, yote ambayo yalifanywa kumwelekea hupotea.

Sugu alimtolea mfano aliyekuwa Rais wa Zaire (siku hizi DRC), Mobutu Sese Seko, alivyofanya uwekezaji mkubwa kwenye mji aliozaliwa wa Gbadolite, Jimbo la Nord-Ubangi. Akajenga uwanja mkubwa wa ndege akiwa na lengo la ndege kubwa ya Concorde ya Shirika la Ndege la Ufaransa, iwe inatua na kupaa Gbadolite.

Mobutu alitaka awe anaweza kusafiri kwenda nchi yoyote duniani na kurejea Zaire, akitumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Gbadolite.

Si hivyo tu, Mobutu aliujenga mji wa Gbadolite na kuupendezesha kuliko majiji mengi Afrika. Mobutu aliita Gbadolite “Versailles of the Jungle”, akiufananisha mji huo na makazi ya zamani ya Mfalme wa Ufaransa, Versailles, Paris.

Versailles in the Jungle, maana yake ni Versailles ya Msituni. Mobutu aliipendezesha Gbadolite kwa kujenga vyuo, majengo makubwa ya biashara, malls, supamaketi, vile alikuwa na ikulu tatu ndani ya Gbadolite. Aliweka umeme wa uhakika kutoka Mto Ubangi. Wananchi wa Gbadolite walipata ajira kwa urahisi.

Leo, Gbadolite sio ile tena. Nguvu nyingi kuujenga mji huo ili uwe Versailles of the Jungle, ilikwenda bure. Uwanja wa ndege umegeuka makazi ya kunguru kulala na kuzaliana. Ndegu zimekuwa adimu. Ni matokeo ya kuwekeza kwa ajili ya fahari ya mtu, badala ya mipango madhubuti ya kuinua shughuli za uchumi za eneo husika.

Sasa, maonyo yaliyotolewa kuhusu Chato kupitia mfano wa Gbadolite, ndiyo yanayodhihirika kwa sasa. Nguvu kubwa ya kuifanya Chato kuwa mji wa utalii mpaka kutoa wanyama kwenye mbuga nyingine na kuwapeleka Burugi, haijashawishi maendeleo baada ya kifo cha Magufuli.

Magufuli alipokuwa hai, Ikulu, ndege kubwa, Airbus na Boeing za Air Tanzania zilitua Uwanja wa Ndege wa Chato, ambao eneo lake la ndege kutua na kuruka (runway) lina viwango vya kimataifa. Runway ya Chato ina urefu wa kilomita tatu (mita 3,000).

Kwa vipimo hivyo, Uwanja wa Chato unazidiwa na viwanja vitatu tu vya kimataifa Tanzania, ambavyo ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na Uwanja wa Ndege wa Songwe. Runway ya Chato inalingana kabisa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume, Zanzibar, vilevile wa Mwanza.

Hivyo, kama Gbadolite baada ya Mobutu, ndivyo na Chato ilivyo miaka miwili baada ya kifo cha Magufuli. Gbadolite ilidhihirisha kuwa mji wote ulikumbwa na uyatima kwa kuondolewa madarakani kisha kufariki dunia Mobutu. Chato ni yatima kwa kifo cha Magufuli.


Miradi mikubwa

Magufuli alipokuwa hai, alipata kutoa hotuba akihofia kuwa miradi mikubwa ambayo alikuwa akiitekeleza ingeweza kukwama bila uwepo wake. Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) mpaka Reli ya Standard Gauge, kasi ya ujenzi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kubwa kuliko hata alivyokuwepo yeye. Vipimo vimeonyesha.

SGR sasa hivi inaelekezwa Kigoma kutokea Tabora, wakati Samia aliikuta Morogoro. JNHPP ilikuwa asilimia 37 wakati Magufuli anaaga dunia, lakini miaka miwili ya Samia imeshazidi asilimia 80. Kumbe, Magufuli hakupaswa kuiwazia miradi mikubwa ya nchi, maana ingeendelea tu, alitakiwa kuifikiria Chato, ambayo kwa hakika inaakisi uyatima mkubwa bila uwepo wake.

Sugu alihoji, nani atakwenda Chato baada ya Magufuli? Rais wa Nne wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kiongozi wa upinzani Kenya, Raila Odinga na viongozi wa nchi mbalimbali duniani, walitua Chato kumfuata Magufuli.

Mawaziri na wabunge walikwenda Chato kama hija. Mwigulu Nchemba, aliapishwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Chato. Leo nani anakwenda? Chato ni yatima.