Mawaziri marafiki wa Magufuli walivyomwangusha
Muktasari:
Bali ilikuwa vigumu kuamini kuwa angeweza kutengua uteuzi wao kwa shinikizo au kwa kashfa.
Dar es Salaam. Haikuwa ajabu kwa Rais John Magufuli kumteua Charles Kitwanga na Profesa Sospeter Muhongo katika baraza lake la kwanza la mwaziri, hata kama alichukua muda mrefu kuliunda.
Bali ilikuwa vigumu kuamini kuwa angeweza kutengua uteuzi wao kwa shinikizo au kwa kashfa.
Wawili hao ni watu wa karibu na Rais, ambaye amewahi kusema hadharani kuwa ni marafiki zake wa karibu.
Lakini Rais hakuendekeza urafiki huo baada ya kuhisi mambo yanamuharibikia.
Wakati Kitwanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, alipokuwa akisumbuliwa na kashfa, Rais Magufuli alionekana kama anasita kuchukua hatua.
Wakati kashfa ikipamba moto bungeni, Kitwanga aliiingia ndani ya ukumbi wa chombo hicho akiwa amelewa. Magufuli hakusubiri kosa jingine. Alitengua uteuzi wake mara moja.
Profesa Muhongo, ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini, naye alikumbana na makali ya Bunge wakati wa kashfa ya uchotwaji fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow. Alistahimili vishindo vya wabunge hadi lilipofikia maazimio, mojawapo likiwa la kutaka mamlaka ya uteuzi wake imwajibishe.
Muhongo alitangaza kujiuzulu saa chache kabla ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kutangaza uamuzi wake kuhusu maazimio ya Bunge.
Tangu ateuliwe tena kuwa waziri baada ya uchaguzi wa 2015, Profesa Muhongo alionekana kuwa ni mchapakazi, aliyejikita zaidi katika kuhakikisha wananchi, hasa wa vijijini wanapata umeme.
Wakati Rais Magufuli alipotangaza kwa mara ya kwanza kuzuia mchanga kusafirishwa nje mwaka jana, Muhongo aliendelea na shughuli zake na mchanga ukaendelea kusafirishwa nje.
Ikambidi Rais atangaze tena kuzuia na baadaye kuunda kamati hizo mbili, moja ikiibuka na matokeo ambayo Magufuli asingeweza kuvumilia tena mtu aliyewahi kumuelezea kuwa ni mchapakazi aliyekuwa akihesabu urefu wa nyaya za umeme wakati yeye akihesabu kilomita za barabara; akamtimua.
Na Rais aliweka bayana.
“Ninampenda sana Muhongo na ni rafiki yangu. (Lakini) Kwa hili, ajifikirie, aji-assess na bila kuchelewa nilitaka aachie madaraka,” alisema Rais Magufuli juzi wakati wa kupokea taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa kiwango cha madini kilichomo katika mchanga uliokuwa unasafirishwa nje ya nchi kwenda kuyeyushwa ili kupata mabaki ya madini baada ya dhahabu kuchenjuliwa mgodini.
Na muda mfupi baadaye, Ikulu ikatoa taarifa ya kutengua uteuzi wake.
“Kwa Rais Magufuli ni kazi kwanza, urafiki baadaye,” alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana.
“Na hilo ni jambo jema katika utumishi wa umma kwa sababu uchapakazi ndiyo msingi wa ufanisi wake.”
Dk Bana alisema Rais Magufuli amekuwa muwazi kwa kuzungumzia mambo anayotaka kuona yanafanyika na hata pale anapokuwa amechukia.
Alisema Rais Magufuli anapenda mtu mfanyakazi na anapoteua mtu wake wa karibu naye akashindwa kufanya kazi aliyopewa kikamilifu, anaumia na kuchukua hatua ya kutengua uteuzi bila kujali urafiki wao.
“Profesa Muhongo ali-focus (alijikita) kwenye masuala ya umeme kuliko madini wakati huko ndiyo kwenye matatizo makubwa. Nadhani waziri ajaye atajifunza kwa makosa ya watangulizi wake,” alisema.
Maoni kama hayo alikuwa nayo mhadhiri mwingine wa UDSM, Faraja Kristomus aliyesema ni jambo la kawaida katika siasa kwa Rais kuteua rafiki zake anaowaamini lakini wakamwangusha.
Alisema toka mwanzo wa utawala wake, Rais Magufuli alionyesha aina fulani ya utendaji ambao ukikosea hana simile. Hata hivyo, mhadhiri huyo alisema makosa ya mawaziri hao hayafanani, hivyo hawawezi kuhukumiwa sawa.
“Tatizo ninaloliona si aina ya mtu kwenye wizara, bali aina ya utendaji ndani ya wizara. Wizara ya Nishati na Madini ina sekta kubwa mbili ambazo zina changamoto nyingi. Sekta ya madini ina mikono mingi ya watu wachafu,” alisema mwanazuoni huyo.
Akiwa na mtazamo tofauti na huo, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema kumekuwa na utamaduni kwamba Rais hakosei, lakini kwa hili la kuwatumbua mawaziri wake linaonyesha wazi kwamba alifanya makosa kuwateua rafiki zake wasio na uwezo.
Hata hivyo, Lissu alisema kilicho cha muhimu zaidi ni sababu za kutumbuliwa kwa mawaziri hao na si kuwaangalia kwa makosa ya kimfumo ambayo yamekuwepo nchini kwa muda mrefu.
Alisema mchanga wa madini ulianza kusafirishwa mwaka 1998 wakati wa Rais Benjamin Mkapa.
Alisema Sheria ya Madini na mikataba mibovu ndiyo iliyosababisha nchi kuibiwa kiasi kikubwa cha madini.
“Tatizo letu kubwa ni sheria. Kwa mfano, sheria inataka Serikali ilipwe mrabaha wa Sh4 kwa kila Sh100 anayozalisha mwekezaji. Halafu, sheria inasema lazima watangaze taxable pay (malipo yanayoweza kukatwa kodi) ndiyo wagawane na Serikali,” alisema Lissu na kusisitiza kwamba lazima mwanya huo wa wizi uondolewe.
Lissu pia ameikosoa ripoti hiyo kwa madai kwamba kiwango cha dhahabu kinachotajwa kupatikana katika makontena 277 yaliyozuiwa Bandari ya Dar es Salaam ni kiwango kikubwa mno kwa sababu migodi ya Tanzania kwa sasa imepunguza uzalishaji.
Pia mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la CUF, Julius Mtatiro alisema vyeo vipo kwa ajili ya watu na haoni ajabu kuondolewa kwa watu waliokuwa marafiki wa Rais Magufuli bali mjadala mkubwa unatakiwa kuwa ni ajenda ya vipaumbele vya Taifa.