Miaka 20 ya matokeo halisi chini ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)

Wednesday December 02 2020
New Content Item (1)
By Mwandishi Wetu

Mwezi Oktoba 10, 2020 uliashiria tarehe muhimu katika uhusiano unaokua kati ya China na Afrika (Sino-Africa). Ni siku ambayo Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) lilianzishwa katika Mkutano wa kwanza wa Mawaziri uliofanyika Beijing. Rais wa wakati huo wa Tanzania, Marehemu Mhe. Benjamin William Mkapa, alijiunga na Rais mwenzake wa China (mstaafu) Mheshimiwa Jiang Zemin na Marais na Wakuu wengine wa Nchi kutoka Togo, Zambia, Algeria na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (OAU) Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim kwenda kushuhudia kuzaliwa kwa kile ambacho leo hii ni alama kubwa katika ulimwengu na pande nyingi ambapo washirika wote wako ndani yake kwa faida ya pande zote.

Alama hiyo inajulikana kwa jina la Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) FOCAC, inayojumuisha Nchi 53 za Kiafrika, Tume ya Umoja wa Afrika, na Jamhuri ya Watu wa China kama washirika, iliundwa ili kupanga mwelekeo wa kukuza ushirikiano mpya, thabiti, na wa muda mrefu ulio na usawa na faida kati ya nchi za China na Afrika. FOCAC ni moja wapo ya njia bora zaidi na yenye nguvu ya kimataifa ambayo ilikuza ushirikiano wa nchi za kusini mwa dunia.

FOCAC ina utaratibu wa kufanya mikutano yake ya viongozi wakuu wa nchi na Serikali kila baada ya miaka mitatu. Mbali na hafla ya mwaka 2000 juu ya kuanzishwa kwa FOCAC huko Beijing na mikutano mingine miwili iliyofanyika Beijing mnamo 2006, mikutano mingine imefanyika nchini Ethiopia, Misri, na Afrika Kusini.


Mkutano wa mwisho wa Wakuu wa nchi na serikali ulifanyikia Beijing mnamo Septemba 2018. Mkutano huo uliweka mkazo wa Ushirikiano kwenye biashara, uwekezaji, misaada ya maendeleo, mikopo nafuu, teknolojia, diplomasia, vyombo vya habari, kilimo, utamaduni, na wananchi wa nchi wanachama kutembeleana.

Kwa upande wa Tanzania sherehe ya kuadhimisha miaka 20 ya FOCAC iliambatana na maadhimisho miaka 55 ya kutiwa saini kwa Mkataba wa Urafiki kati ya Tanzania na China. Tangu kusainiwa kwa Mkataba huo, uhusiano wa nchi zetu mbili umekuwa wa mfano katika nyanja zote.

Advertisement

Nchi zetu mbili kila wakati husisitiza kushirikiana na kuungana mkono katika mambo ya msingi yenye maslahi kwa pande zote katika medani za kimataifa. Kwamba urafiki na uhusiano wetu ni wa majira yote ya raha na shida bila kutetereka.

Ni vyema ifahamike kuwa, nchi hizo mbili zilidumisha mashauriano ya kisiasa kwa kiwango cha juu, haswa kupitia mawasiliano ya pande mbili kati ya viongozi wa nchi na viongozi waandamizi wa serikali. Mawasiliano hayo yaliwawezesha kutathmini ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali na kukagua uwezekano wa kuukuza, haswa katika uwanja wa uchumi, biashara, uwekezaji, utalii, miundombinu, na maeneo yanayohusiana na elimu ya juu, afya, na jeshi.

Mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 mwanzoni mwa mwezi Januari 2020 umewezesha ulimwengu kushuhudia hali thabiti ya urafiki wa Watanzania na Wachina kwa mara nyingine. Baada ya kuenea kwa virusi huko Wuhan, Watanzania walielezea mshikamano na huruma yao ndugu zao China.

Serikali ya Tanzania ilieleza utayari wa kujitolea kutuma timu ya madakatari na watalaam wa afya kutoka Tanzania kwenda jimbo la Hubei ili kuungana na wenzao wa China katika vita dhidi ya COVID-19.

Kadhalika, Tanzania ilipokabiliwa na janga hilo la COVID- 19 mwezi Machi 2020, serikali ya China ilionyesha haraka mshikamano wao na Tanzania na ikatoa misaada ya kupambana na janga hilo kwa Tanzania.

Mbali na msaada huo, China pia ilishiriki katika mapambano dhidi ya COVID-19 Tanzania kupitia kubadilishana uzoefu wake katika kupambana na virusi kupitia mikutano kadhaa ya video na wataalamu wetu wa afya na kutoa nyaraka mbali mbali za namna ya kuwahudumia wagonjwa na kudhibiti kuenea kwake.

Kwa kusaidiana katika nyakati ngumu, Tanzania na China kwa pamoja wamefungua ukurasa mpya katika rekodi ya ushirikiano wao wenye manufaa kwa pande zote. Wameuonyesha ulimwengu kwamba dhana ya kujenga jamii yenye maisha yenye manufaa kwa binadamu, inayokuzwa na China, inahitaji vitendo kutoka kwa wanajamii wa jumuiya ya kimataifa.


Katika eneo la biashara, China imekuwa mmoja ya mshirika mkubwa wa kibiashara wa Tanzania na sasa inaongoza kama chanzo kikuu cha Uwekezaji wa moja kwa moja wa nchi ya Kigeni.

Katika miaka 20 iliyopita, biashara za Wachina zimeimarisha uwepo wao nchini Tanzania na kushiriki katika mipango ya maendeleo ya Tanzania, haswa katika nyanja ya ujenzi wa miundombinu kama barabara, reli, madaraja, bandari, na ujenzi wa nyumba.

Ushirikiano wa pande mbili pia unajionyesha katika nyanja za afya, kilimo, na jeshi. Maeneo mengine ni elimu, ziara za kubadilisha uzoefu katika sekta mbalimbali zikiwemo za waandishi wa habari, sana na utamaduni.

Mpango Mkakati unaojulikana kama “Belt and Road Initiative (BRI)” uliozinduliwa na Rais wa China Mheshimiwa Xi Jinping mnamo mwaka 2013, ni fursa ya nyingine inayozidi kuzileta karibu nchi zetu katika ushirikiano wa kiuchumi.

Mkakati huu umejikita katika kuyanganisha mataifa mbali mbali na miundombinu na kuongeza uwekezaji. Kama mshirika muhimu wa China barani Afrika, Tanzania itachukua jukumu muhimu katika kutekeleza mpango huu, na kunufaika na faida ya eneo lake la kijiografia, uwezo wa kiuchumi, na uzito wa kidiplomasia.

Ushiriki wa Tanzania katika BRI utawezesha uratibu utakaozingatia mipango ya maendeleo na namna ya kufungamanisha miundombinu yake na ilyomo katika BRI ili kuleta matunda yanayotarajiwa. Miradi kama Ujenzi wa Reli ya Kisasa, ufufuaji wa Reli ya TAZARA na reli ya zamani ya kati, kuboresha na kupanua Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Zanzibar, ujenzi wa uwan-ja mpya wa ndege Dodoma, Upanuzi wa Viwanja vya Uwanja wa ndege vya Dar es Salaam (Terminal III) na Zanzibar (Terminal III) na Barabara za Juu Ubungo utachangia sana katika utekelezaji wa BRI.

Chini ya uongozi wa Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, matarajio ya kiuchumi, biashara na uwekezaji ndani mifumo ya FOCAC na BRI baada ya janga la COVID-19 kudhibitiwa duniani ni mazuri na makubwa kwa pande mbili Tanzania na China.

Advertisement