Miaka 54 ya Mapinduzi Dk Shein ataka amani na utulivu Zanzibar

Muktasari:

Serikali itaendelea kuhakikisha amani inadumishwa muda wote na kuwavutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kufika Zanzibar kwa ajili ya kuwekeza.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein amewataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo ili kuwa chachu ya kuendelea kuwa kivutio kikubwa kwa uwekezaji miradi mikubwa ya maendeleo visiwani hapa.

Dk Shein alitoa kauli hiyo jana katika ghafla ya uwekaji jiwe la msingi la mji mpya wa kisasa unaotambulika kwa jina la ‘Fumba Town Development’ huko Fumba Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele chake kinafanyika leo.

Alisema kuwa pamoja na wawekezaji wengi kuonyesha nia ya kufika visiwani hapa kwa ajili ya kuwekeza katika miradi mikubwa ya maendeleo, ili lengo lao hilo litimie na kuleta tija kwa jamii, amani ni ngao kubwa.

“Lazima tutambue kuwa hivi sasa wawezekaji wengi wameonekana kuwa na nia ya kufika visiwani humu kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali, ila lazima ifahamike kuwa kuja kwa wawekezaji hawa kunatokana na uwepo wa amani hivyo si busara hata kidogo kuona amani inatoweka kwa masilahi ya wachache,” alisema Dk Shein.

Alisema Serikali itaendelea kuhakikisha amani inadumishwa muda wote na kuwavutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kufika Zanzibar kwa ajili ya kuwekeza.

Alisema Zanzibar bado kuna maeneo mengi yanayohitaji kuwekezwa mjini na vijijini. Aliyataja maeneo ya mjini yanayohitaji uwekezaji kuwa ni Kwahani, Kijangwani, Kwalimsha na Kariakoo na kwa upande wa vijijini ni Mkokotoni, Chwaka na Tunguu. Pia alisema Pemba nako kuna maeneo mazuri ya uwekezaji.

“Tukifanikiwa kuibadilisha miji yetu kwa ujenzi wa nyumba za kisasa ambapo jicho kubwa lipo kwa wawekezaji, ni dhahiri kuwa mandhari ya miji yetu inaweza kuwa ya kuvutia kwa wenyeji pamoja na wageni wanaofika visiwani humu kwa ajili ya kutalii,” alisema Dk Shein.

Akizungumzia suala la ardhi, Dk Shein aliwataka wananchi kuacha tabia ya kugombania ardhi kwa kuwa husababisha migogoro isiyo na tija ambayo inarudisha nyuma maendeleo.

Alisema Serikali itafanya kila njia kuandaa matumizi bora ya ardhi ili kuwawezesha wananchi kupata makazi bora ya kuishi.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed alisema miradi mikubwa ya maendeleo tayari imeanzishwa ikiwa ni pamoja na nyumba za makazi ambazo huuzwa kwa bei nafuu.

“Pamoja na hilo lakini pia hivi sasa tuna miji ya kisasa 14 Unguja na Pemba ambayo kwa ukweli tunajivunia nayo, ila sisi kama Serikali bado tunaendelea kutoa elimu kwa wawekezaji ili kuja kwa wingi kuwekeza nchini humu lengo ni kuwa na Zanzibar yenye miji ya kisasa zaidi,” alisema.

Msimamizi wa Mradi wa Fumba Town, Sebastian Dezot alisema lengo ni kurahisisha upatikanaji wa makazi bora ya kuishi kwa wananchi wa Zanzibar kwa gharama nafuu ambayo kila mmoja anaweza kuimudu.