Miaka miwili bila Mzee Mkapa, BMF na Watanzania waendelea kumuenzi

Hayati Benjamin Mkapa

Muktasari:

Aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa anatimiza miaka miwili tangu alipofariki usiku wa kuamkia Julai 24, 2020 kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa anatimiza miaka miwili tangu alipofariki usiku wa kuamkia Julai 24, 2020 kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Akilitangazia Taifa taarifa za msi­ba huo mkubwa, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli alisema Hayati Mzee Mkapa amefariki wakati akipatiwa matibabu hospitalini mjini Dar es salaam.

Baada ya kustaafu urais mwaka 2005 Hayati Benjamin Mkapa alikuwa aki­jishughulisha na masuala mbalim­bali ikiwemo kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mkuu wa Chuo Kikuu cha Cavendish, Uganda, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chuo Kikuu cha Aga Khan nk.

Pia, aliunda Taasisi ya Benjamin Wil­liam Mkapa (BMF) inayohusika na utoaji wa huduma za afya hasa katika maeneo ya pembezoni mwa nchi.

Katika kumuenzi kiongozi huyo mashuhuri barani Afrika na duni­ani kwa ujumla Taasisi ya Benjamin William Mkapa imekuwa ikiandaa makongamano maalumu kila mwaka yanayowakutanisha viongozi wa ngazi za juu kutoka ndani na nje ya nchi, watendaji wa serikali, mashirika ya kimaendeleo, asasi zisizo za kisreikali, wadau mbalimbali na wananchi kwa lengo kujadili na kukumbuka mambo makubwa aliyoyafanya Hayati Mkapa.

Huu ni mwaka wa pili kongamono hilo linafanyika na kuhudhuriwa na vion­gozi wa ngazi za juu kutoka ndani na nje ya Tanzania akiwemo Rais Samia Suluhu, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Rais Mstaafu wa Msumbiji Joaquim Chissano na viongozi wen­gine wa Serikali.

Akizungumza kwenye kongamano hilo ambalo kwa mwaka huu limefanyika Zanzibar, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Taasisi ya Benjamin Wil­liam Mkapa ni mfano bora wa taasisi binafsi zinazotoa mchango mkubwa katika sekta ya afya nchini.

“Kupitia taasisi hii kwa miaka 16 sasa, watumishi wa afya wa kada mbalim­bali wapatao 10,041 wakiwemo kada za madaktari, wauguzi, matabibu, wafamasi pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wamesambazwa kote nchini,” amesema Rais Samia.

Amesema watumishi hao wame­ongeza tija na ufanisi katika utoaji huduma bora za afya kwa wananchi wa Tanzania.

Hata hivyo Rais Samia amesema bado ushirikiano wa sekta binafsi na Seri­kali katika baadhi ya maeneo hauko sawa, jambo ambalo linahitaji msuku­mo mpya ili kuwawezesha Watanzania kufaidika na ushirikiano huo.

“Bado wengi wetu tumeelemewa na kasumba ya kutoamini sekta binafsi hivyo kumbukizi hiyo iwe sehemu ya kuwakumbusha viongozi umuhimu wa mabadiliko,” amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi ame­sema Hayati Mkapa alikuwa muasisi wa sera za sekta binafsi kufanya kazi kwa karibu na Serikali kupitia sera ya kubinafsisha mashirika ya umma kwa watu binafsi ili kuongeza ufanisi.

Amesema ikiwa sekta binafsi itafanya kazi kwa karibu na Serikali, hiyo ndiyo inaweza kuwa njia bora ya kumuenzi Mzee Mkapa ambaye aliipenda nchi na wananchi wake kwa kuhakikisha anawaboreshea huduma za afya.

Aidha, Rais Samia amesema anatarajia sekta binafsi itatoa ushirikiano kwa Serikali pamoja na kuzingatia kuwa afya ni hitaji la jamii hivyo wasiweke faida kama kipaumbele bali huduma ndio ipewe kipaumbele.

“Afya ni stahili ya umma na siyo biashara kwa asilimia 100, hivyo laz­ima mzingatie urali kati ya kupata faida kiasi na kuwekeza katika kutoa huduma endelevu za afya kwa jamii na kuwekeza pale kwenye mahi­taji makubwa zaidi kwa maslahi ya umma,” amesisitiza Rais Samia.

Rais Samia amesema njia bora ya kuendelea kumuenzi Hayati Mkapa ni kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi hasa katika kuboresha afya za Watanzania.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduz, Dk Hussein Mwinyi amesema kumbukizi hii ya pili ina nafasi adhimu kwake. Kwanza, ni mara ya kwanza anakuwa mwenyeji kwenye shughuli hiyo na pili, ni mara ya kwanza kuhudhuria kumbukizi hiyo akiwa kama Msarifu (settlor) wa Taasisi ya Mkapa Foundation.

“Leo napenda nihadithie kwamba wakati nilipofuatwa kuombwa kuwa Msarifu nilikuwa na kigugumizi kuku­bali. Uzito wangu ulikuwa ni kwa mashaka kuwa viatu ninavyovyaa ni vikubwa ukizingatia kwamba Msarifu wa kwanza alikuwa ni yeye mwe­nyewe Mzee Mkapa. Sikuwa na njia wala uthubutu wa kukataa dhima ya jukumu la kuwa Msarifu,” anasema Dk Mwinyi.

“Nilipata nguvu zaidi ya kukubali kuongoza taasisi hii nikitambua kuwa matunda ya kazi zinazofanywa na taasisi hii yanalenga kuleta ustawi wa Taifa letu, na kazi njema lazima iendelezwe ikiwa pia ni njia bora ya kumuenzi Mzee Mkapa,” anasema Dk Mwinyi.

Anasema kwa kutambua ukubwa na dhima wa jukumu hilo, amejidhati­ti kadiri ya uwezo wake kuongoza taasisi hii kuhakikisha kwamba dira na dhamira ya kuanzishwa kwake inafikiwa.

Dk Mwinyi amesema taasisi hiyo kwa upande wa Zanzibar, inafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Afya katika kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma, mafunzo na hivi sasa katika kutekeleza mipango itakayo­tuwezesha kuanzisha Bima ya Afya hapa Zanzibar.

Naye Rais Mstaafu wa Msumbiji Joa­quim Chissano amesema mara ya kwanza ya urafiki wake na Hayati Mkapa ilikuwa mwaka ambao mata­tizo yaliyokuwa yakionekana ni ya ndani ya chama cha Ukombozi cha Msumbiji ambapo walianza kujikita na kuwaunganisha watu wa Msumbiji na wa Tanzania.

“Tulitaka ndugu zetu Watanzania wat­uunge mkono katika mapambano yetu. Tulikuwa na migawanyiko mbalimbali ndani ya nchi yetu na tulitaka kuion­doa. Tuliueleza uongozi wa TANU na Afro-Shirazy Party ili watusaidie kueleza katika taasisi zao mbalimbali na kwa wananchi wote wa Tanzania,” amesema Chissano.

Chissano anasema mbali na vipawa vyake binafsi, Hayati Mkapa alikuwa na hisia za Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliamini kwamba Tanzania haitaweza kuwa huru kama taifa lingine la Afrika lipo chini ya Ukoloni.

Kwa upande wake Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema hayati Mkapa hatoweza kusahaulika kwa sababu ni mtu aliyeibadilisha Tanzania katika nyanja nyingi kupitia uongozi wake uliofanya mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Amesema hayati Mkapa alifuata mipango ya kufufua uchumi, sera thabiti za uchumi mkuu pamoja na mageuzi ya kimuundo wa sera ya ubinafsishaji iliyoanzishwa na mtan­gulizi wake.

Alieleza kuwa utawala wake ulipata misingi ya uchumi ambayo iliongeza imani ya wawekezaji kwa nchi na Serikali, hivyo kutokana na juhudi hizo wamekusanyika kutafakari na kuweka mikakati juu ya nafasi ya sekta binafsi katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia uwekezaji katika sekta ya afya.

Aidha amesema Hayati Mkapa alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha taasisi za uwajibikaji na kubadilisha sekta ya umma ambayo ilichochea ukuaji wa sekta binafsi.

Amesema kongamano hilo limewaku­tanisha pamoja na kutafakari juhudi za kuboresha utendaji kazi wa sekta ya afya, jambo ambalo ni mwanga wa matumaini kwa watanzania wote hasa wale wanaoishi maeneo ya pembezoni na maeneo yasio na huduma.

Ameeleza kwamba anaamini kum­bukizi zitatumika kuheshimu maisha yake na kuyaenzi maono yake ya kuboresha hali ya kiuchumi na kijamii ili kupata mamilioni ya huduma Bora za afya kwa wanawake na wanaumme.

“Nimeambiwa kuwa kupitia jukwaa hili washiriki watajadili na kuchangia maoni ya kisera na kimakakati juu ya kujenga sera na mifumo thabit ya maendeleo ya uchumi wa Jamii huku mkiimarisha ulinzi wa kijamii kwa afya kupitia ushirikiano wa kimakakati kati ya serikali zetu kitaifa na kima­taifa,” amesema Othman.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjameni Mkapa Dk Ellen Mkondya-Senkoro amesema ni miaka miwili bila ya kuwa na Mkapa ni mambo mengi ambayo yanakumbukwa wakati wa uhai wake.

Amesema Hayati Mkapa ndie mua­sisi uwekezaji wa sekta binafsi (PPP) ambapo wakati wake ndipo alipo­karibisha wawekezaji katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wa afya alisema taasisi hiyo ilianzishwa kwa ajili ya kubore­sha huduma za afya hususan upande wa ugonjwa wa ukimwi lakini muda unavyokwenda taasisi hiyo imepanua huduma zake ikiwemo utoaji wa mafunzo na kuboresha miundombinu ya afya Hayati Benjamin William Mkapa.

Leo, Taasisi ya Benjamin Mkapa inamkumbuka kiongozi shupavu.