Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Michezo ya ‘PS’ yawaliza wazazi

Muktasari:

Wadau mbalimbali wametaka michezo ya mitandaoni inayochezwa mitaani maarufu kama ‘Play Stations’ (PS) ipigwe marufuku kwa watoto au kupangiwa muda maalumu.

Dar/mikoani. Wadau mbalimbali wametaka michezo ya mitandaoni inayochezwa mitaani maarufu kama ‘Play Stations’ (PS) ipigwe marufuku kwa watoto au kupangiwa muda maalumu.

Mkazi wa Yombo Dar es Salaaam, Asha Ramadhan alisema Serikali iliangalie suala hilo kwa nguvu zote, kwani watoto wanashindwa kufanya mambo mengine, ikiwamo kusoma na mazoezi wanayopewa na walimu shuleni.

“Hizi fremu za kuchezeshea hizo games zimekuwa nyingi mno. Si mbaya kwa sababu ni burudani, lakini suala hili liangaliwe. Kwa mfano mwanangu ni darasa la sita, akiamka asubuhi anawaza kwenda PS, kuna wakati anarudi nyumbani hata saa 4 usiku, ukimuuliza anakwambia alikuwa kwenye games,” alisema Asha.

Mkazi wa Tabata Kisiwani Dar es Salaam, Joyce James alisema mwanawe yuko darasa la tano, amekuwa na uraibu wa michezo hiyo, kuna wakati anatoroka shule na wakati mwingine kushindwa kula chakula kwa wakati.

“Namnyima hela ya shule ili asiende huko, ila akikutana na hela imekaa vibaya ndani anaiba anaondoka, sijui itakuwaje siku akiiba nyumbani kwa watu wengine.

“Sisemi games zisiwepo, maana kila mtu na starehe yake, lakini serikali za mitaa waweke muda maalumu wa kufungua, mfano iwe kuanzia saa 10 jioni mpaka saa mbili usiku. Au Jumamosi na Jumapili,” alisema Joyce.

Mkazi wa Majengo Arusha, Fatumah Mlay alisema kuwa ongezeko la michezo hiyo ni tishio kwa maendeleo ya wanafunzi, kwani wengi hawasomi kabisa.

“Wanafunzi wanaishia kucheza hii michezo na hakuna udhibiti. Ifike mahali serikali ichukue hatua kunusuru watoto wetu, kabla hawajapotea njia kimaisha,” alisema.

Kwa upande wake Peter Mollel, mkazi wa Sanawari jijini Arusha alisema ongezeko la michezo ya games inaashiria kwamba kuna mahali mamlaka husika zinafeli.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Dodoma, Stanley Ndahani alisema michezo hiyo siyo mibaya kwani inachangamsha akili za watoto, lakini tatizo ni jinsi inavyotumika.

Alisema ingechezwa kwa kuzingatia ratiba za watoto ingekuwa ni sehemu ya darasa kwa kujifunza kutokana na ukweli kuwa inafikirisha, kwa hiyo mtoto anatumia akili kuwaza.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Sayansi cha Mbeya, Agnes Stephen alisema michezo hiyo ina madhara makubwa kwa vijana na watoto kwa kuwa akiingia kucheza hawezi kufikiria kingine.

Alisema japokuwa inafikirisha kwa watoto, lakini madhara yake ni makubwa ukilinganisha faida iliyomo, kwa hiyo Serikali itazame upya kuhusu sheria zake.

Mkazi wa Mkolani wilayani Nyamagana Mwanza, Maua Pazi aliiomba serikali kudhibiti vituo vya kuchezea games katika jiji la Mwanza, akidai michezo hiyo inasababisha tabia ya udokozi kwa watoto.

“Mtoto mdogo hana uwezo wa kufanya kazi ya kumpatia fedha ya kucheza michezo hiyo, matokeo yake wengine wanashawishika kuiba fedha ili wakacheze, huyo akikua anaweza kuwa mhalifu mkubwa,” alisema Maua.

Jubileth Joseph ni mfanyabiashara wa intaneti mjini Morogoro, ambaye alisema kuwa mara kadhaa wanafunzi wamekuwa wakienda na kutaka kompyuta kwa ajili ya kucheza game, lakini wamekuwa wakiwanyima.

“Mbali na biashara pia mimi ni mzazi, hivyo siwezi kuruhusu watoto kutumia muda mwingi kukaa hapa na kucheza game,” alisema Jubileth.

Alisema baadhi ya wanafunzi wa sekondari wamekuwa wakihitaji kompyuta kwa ajili ya kupakuwa mambo mbalimbali ya kimasomo, wanawakagua inapogundulika wanacheza games huwa wanawaondoa.


Watoto wanasemaje?

Masudi Seleman (11) alisema kila siku akitoka shule na kumaliza kula lazima aende PS, kwani huko anakutana na rafiki zake mbalimbali na kurudi jioni.

Alisema akipewa Sh1,000 ya shule anahifadhi kidogo kwa ajili ya kuchezea PS, kwamba ikitokea hana huwa anawaomba rafiki zake au hata wakubwa ambao anawafahamu.

Naye Erasto Samwel (15) alisema mchezo huo kwake unampa burudani kama ilivyo michezo mingine.

“Napenda sana kwenda PS, kule kuna game za michezo ya aina mbalimbali…na ile ni michezo kama ilivyo michezo mingine, kama ambavyo watoto wengine wanapenda kucheza mpira,” alisema Samwel.

Wanaochezesha michezo hiyo

Mmoja wa wachezeshaji wa PS hizo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini wa Dar es Salaam, alisema zipo aina mbalimbali za michezo, lakini zinazotumika kwa sasa ni PS Three, Four na Five ambazo zinauzwa kwa gharama tofauti.

Alisema biashara ya PS inalipa na wateja wake wakubwa ni wanafunzi kuanzia darasa la tatu mpaka vyuoni; kwamba muhimu ni kupata fremu rafiki ambapo wanafunzi na wanavyuo wanapita mara kwa mara.

Alieleza kuwa kila mchezo mmoja gharama yake ni Sh 500 kwa mchezo ni wa dakika 10.

“Ndani ya dakika 10 tu hela yake imeisha. Lakini pia inategemea, kwa sababu kunakuwa na michezo ya aina tofauti mingine analipa yule aliyefungwa,” alisema.

Kuhusu kufungua anasema huwa inategemea na serikali yako ya mtaa, ila yeye anafungua saa mbili asubuhi na kufunga saa 5 usiku.

“Mimi biashara yangu nafanyia hapa Sinza lakini naishi Gongolamboto ambapo pia huko kuna PS, lakini wao wanafanya kazi kwa saa 24,” alisema.


Walimu wanena

Mwalimu Zainabu Sanga kutoka Morogoro alisema game hizo ni chanzo cha tabia mbaya kwa watoto kwa sababu maeneo wanayochezea wanakutana na watoto wenye tabia tofauti.

Naye Mwalimu wa Shule ya Msingi Sanjo ya Moshi, Timoth Isaya alisema wanafunzi wanaocheza game hawafanyi kazi za nyumbani (home work) kwasababu wakitoka darasani hawafikirii tena kujisomea.

“Game ni kama ugonjwa, mwanafunzi anataka kila muda anaopata akimbilie huko,” alisema mwalimu Isaya.


Wanasaikolojia washauri

Mhadhiri Msaidizi wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shagembe Magolanga alisema PS sio mbaya, isipokuwa ni namna ambavyo watoto wanazitumia.

“Inatakiwa ichezwe kwa ajili ya kuwasaidia katika afya ya akili, wasimamiwe vizuri, hiyo inasaidia katika makuzi yao kwa kuwaongezea ubunifu, kumbukumbu na kujifunza lugha, pia wasicheze kwa muda mrefu, zaidi ya hapo watapata uraibu,” alisema Magolanga.

Alisema uraibu huo unafanana na zile nyingine zinazoleta shida ya kisaikolojia katika afya ya akili, hivyo ni vyema wakasaidiwa kwa kupatiwa msaada wa kitaalamu kwa kuwaona wanasaikolojia.

“Mtoto akifikia hatua hiyo atashindwa hata kujituma katika kazi ndogondogo za nyumbani na za kijamii, inatakiwa wanaoziendesha wawe na elimu ya kuendesha michezo ya watoto na kupata elimu ya malezi ili waweze kujua mahitaji yao kwa ujumla katika umri tofauti tofauti,” alisema Magolanga.

Mwanasaikolojia Charles Kalungu alisema uraibu wa michezo hiyo hutokea hata kwa watu wazima, lakini kwa watoto inachangiwa na malezi ya mzazi au mlezi.

“Wazazi wako na mambo yao binafsi, kuna ambao wana kazi za kufanya na kuna ambao hawana kazi za kufanya ila wanawachukia tu watoto wao kulingana na mazingira waliyowapata. Sasa hiki kitendo kinaweza kikawafanya wawaache tu wenyewe wacheze, watoto wajitafutie burudani zao wao wenyewe

“Na kuna muda mwingine watoto wanashawishiana na wenzao kwenda kucheza na ukiangalia hata gharama ya kwenda kushiriki ni kidogo lakini kwa mtoto 500 ni kubwa. Mtoto anakaa asubuhi mpaka jioni na wengine hawaendi shule, vibanda vingi pia vimetengenezwa katika namna ya kutokuruhusu mtu kuona ndani,” alisema.

Alifafanua kuwa, mchezo huo usipochezwa kwa umakini unaweza ukaleta athari, ila kisaikolojia pia ni mojawapo ya tiba ya kumsaidia mtu katika kuchangamsha akili.

“Mtoto anatakiwa alelewe chini ya sheria na uhuru kiasi, asifungwe kabisa ila apewe masharti na vigezo pasipo kuwakwaza wazazi au walezi wake,” alisema.

Kalungu alieleza kuwa mtoto ambaye amepata uraibu na hizo PS ili kumsaidia anatakiwa kwanza apewe sababu ya kwa nini unamkataza kwa kumfafanulia faida na hasara.

“Inategemea na mtoto ana umri gani maana wanatofautiana umri wa kuelewa. Pia atengenezewe kitu kipya ambacho kitakuwa mbadala wa huo mchezo, hapo inatakiwa uangalie yeye binafsi ana uwezo gani. Unajua kuna wazazi huwa wanawalazimisha watoto wafanye vitu ambavyo wenyewe hawavipendi,” alisisitiza.


Serikali za Mitaa wanasemaje?

Katamba Amadi, mjumbe wa Serikali ya Mtaa Kata ya Bomambuzi mjini Moshi, alisema matokeo ya game kwa watoto ni udokozi ambapo wanachukua fedha za nyumbani wanaenda kuchezea gemu.

“Mtoto akitumwa dukani chenji inayobaki anaichukua anaenda kichezea game mama akija kutafuta chenji nyumbani haikuti. Kesi hizi tunazipata mara nyingi,” alisema Amadi.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa Tabata Kisiwani jijini Dar es Salaam, Atway Mohamed aliliambia Mwananchi kwamba amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali kuhusiana na vituo vya PS.

“Malalamiko tunayapata, wanaotoa malalamiko sio wazazi wa watoto hao, utakuta mtu anapita anamuona mtoto wa jirani yake muda wa shule kaingia PS, anakuja kutueleza, hali ya usalama pia ni ndogo, watoto hao wanajazana hakuna feni na wanawafungia milango,” alisema.


Mbozi mambo ni tofauti

Huko Mbozi, mkoani Songwe mambo ni tofauti, kwani wafanyabiashara hiyo wanasema biashara ya PS hailipi, na hivyo wameamua kufunga fremu zao.

Mfanyabiashara, Nasoro Msukwa, mkazi wa Mbozi alisema biashara hiyo hailipi kwa kuwa hakuna wateja wa kutosha, waliopo ni wachache na ambao pia wengi wao wakifika kucheza hawana fedha za kulipia, hali ambayo inasababisha kushindwa kulipa gharama za umeme, pango la chumba na mahitaji mengine.

Naye Eliud Nzowa alisema ameamua kuachana na biashara hiyo baada ya kuona haimlipi kwa kukosa wateja wa kutosha na kuwa mashine hiyo ameamua kuiuza.

“Wateja wetu ni watoto wadogo ndiyo wanapenda mchezo huo, kutokana na mwamko mdogo katika mji wetu wanaofahamu na wanaoshiriki ni wachache hivyo kufanya kipato pia kuwa kidogo,” alisema Nzowa.


Kilio kipya jijini Mbeya

Wakati maeneo mengine wakitaka serikali kuangalia upya suala uchezaji wa watoto na vijana kwenye PS, jijini Mbeya mambo ni tofauti ambapo, Serikali jijini humo imeombwa kupiga marufuku michezo ya kubahatisha ya mashine za Kichina maarufu kama dubu.

Kuna madai kuwa imekuwa ikichochea uhalifu kwa watoto wadogo na kutumikishwa ajira za utotoni kwa lengo la kupata kipato.

Katika Mtaa wa Mabatini kunatajwa kuibuka kwa wimbi la watoto kati ya miaka 10 mpaka 15 wakishiriki kucheza michezo hiyo muda wa masomo na wengine kukatisha masomo.

Dereva bodaboda kijiwe cha Mabatini, Elaston Mwakalonge alisema hali hiyo inahatarisha kizazi kijacho kwa kuzalisha kundi la wahalifu, kwani kuna wakati wanaokota vyuma chakavu ili wapate fedha za kwenda kucheza mchezo huo.

Peter Maiko, Mkazi wa Forest ambaye anachezesha mchezo wa kubahatisha alisema kwa kiwango kikubwa wateja wake ni watu wazima kutokana na Sera na sheria zilizowekwa kwa kuruhusu vijana wenye umri wa zaidi ya miaka 18 kucheza.

Imeandikwa na Tatu Mohamed, Mussa Juma, Habel Chidawali, Omeni Daniel, Hamida Shariff, Stephano Simbeye na Hawa Mathias.