Prime
Migogoro ya mazishi inavyotikisa familia
Muktasari:
- Migogoro ya kugombea miili ya marehemu inatokana na tofauti za familia, ndoa na urithi wadau wanashauri mazungumzo ya mapema, maridhiano na kuweka wazi matakwa ya marehemu kabla ya kifo.
Dar es Salaam. Kipindi kinachopaswa kuwa cha maombolezo na kuagana kwa heshima na mpendwa aliyefariki dunia, baadhi ya familia hugeuka chanzo cha migogoro, malumbano na hata kesi mahakamani.
Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na matukio ya ndugu kugombea miili, kila upande ukidai haki ya kuamua mahali pa mazishi na anayepaswa kusimamia shughuli hizo.
Mara nyingi migogoro humhusisha mke au mume dhidi ya wazazi wa marehemu, ndugu wa damu dhidi ya watoto au familia mbili zinazodai kuwa na mamlaka ya mwisho.
Julai 24, 2026 kulitokea mvutano kati ya mke mkubwa na ndugu wa marehemu Wambura Mumbiya (54) kuhusu nani anayepaswa kusimamia mazishi yake huku kila upande ukitaka kuhusika na mazishi yake.
Pia, Juni 13, 2026, Katoro mkoani Geita, ndugu waligombea mwili wakidai aliyekuwa akiishi naye hakuwa na haki ya kumzika kwa kuwa hakulipa mahari.
Mbali na hao, Oktoba 2, 2023, Dodoma Makulu, mwili wa Christiana Chigunda ulizikwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya mabishano kati ya familia ya marehemu na upande wa mume.
Mwaka 2021, Kilimanjaro, kulikuwa na kesi ya kugombea mwili wa Fatma Kileo kati ya mumewe Zuberi Shango na familia ya marehemu.
Vita ya maiti na mali
Akizungumza hivi karibuni Jackson Mwakibete, Mkazi wa Mbeya amesema alikataliwa na upande wa mke wake ambaye alimbadilisha dini wakidai hawana taarifa ya ndugu yao kubadili dini na kuolewa.
“Niliishi na mke wangu kwa miaka saba na tulifunga ndoa ya kanisani na kipindi chote alinambia ni yatima hana ndugu na sikuwahi kumsikia akiwasiliana nao,”amesema Mwakibete.
Mwakibete amesema baada ya mkewe kufariki dunia walitokea watu na kudai ni ndugu yao na walizungumza na marehemu kabla ya kufariki, hivyo wanahitaji mali zake na wanamchukua kwa ajili ya kumzika huku wakidai hawawatambui watoto wao.
Tukio hilo lilitokea Mei 2024, mkoani Mbeya akisema ndugu walifanikiwa kuondoka na mwili kwenda mkoani Kagera kwa sababu hawakumtambua mumewe (Mwakibete) na hata kubadili dini hawakuwa wanafahamu hivyo alizikwa Kiislamu kwa imani yake ya awali.
Kisheria
Wakili Janeth Kimaro amesema jambo la kwanza kuangaliwa kama marehemu aliwahi kueleza matakwa yake kuhusu sehemu anayotaka kuzikwa au namna mazishi yafanyike.
Amesema Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 haielezi moja kwa moja nani anaamua kuhusu mazishi, hivyo uamuzi huongozwa na mila, desturi, taratibu za kifamilia na mazingira ya maisha ya marehemu.
“Tanzania ina tamaduni mbalimbali, kuna tamaduni zinazotambua zaidi upande wa baba na nyingine upande wa mama, hivyo mazingira ya kila familia hupewa uzito,” amesema.
Kimaro amesema pale marehemu alipokuwa katika ndoa halali, mke au mume ndiye mwenye mamlaka ya kwanza ya kufanya uamuzi kuhusu mazishi kwa kuwa, sheria humtambua kama mtu wa karibu zaidi.
Hata hivyo, kwa watu walioishi pamoja bila ndoa inayotambulika kisheria, uamuzi hutegemea makubaliano ya familia au mila za jamii husika.
Amesema migogoro pia hutokea wanandoa wanapotengana kwa miaka mingi bila talaka. Mmoja akifariki, familia ya marehemu inaweza kutaka kusimamia mazishi huku mwenza wa ndoa akidai haki yake ya kisheria.
Frank Mashiri, Mkazi wa Geita na Dar es Salaam anakumbusha mkasa uliotoka mwaka 2015 katika familia yao dada yake aliyeolewa, baada ya kufariki mumewe akataka kwenda kumzika kwao mwanamke.
“Mimi nilikuwa naishi kwa dadangu, sasa kuna kipindi dadangu alikuwa akimweleza shemeji (mumewe) kwamba kama atatokea akatangulia kufariki basi akazikwe kwao na si ukweni,” anasimulia Mashiriki.
“Kweli, dadangu akatangulia kufariki, shemeji akawaeleza kwamba mkewe anakwenda kumzika kwao (kwa mwanamke), kwani ndivyo alisema, sasa kwao mwanamume wakagoma kwa nini wakati alikwisha muoa na mahari alitoa.”
Mashiri amesema baada ya mvutano ikiwamo kwa upande wa mwanamke kukataa wasiende kumzika kwa sababu alikwisha kuolewa akazikwe ukweni na ndiyo utaratibu.
“Mimi niliwaambia dadangu alimweleza mumewe kwamba kama atatangulia akifariki aje kuzikwa nyumbani na hapo mambo yakaa sawa lakini kishingo upande kwani kwao mwanamume walitaka akazikwe huko kwa sababu alimwoa na mahari walitoa.”
Mashiri amesema kama asingekuwa sehemu ya familia hiyo na kusikia wosia wa dada yake, shemeji yake angepata shida kuwashawishi upande wa ndugu zake na ukweni.
“Mimi ndiye nilisaidia kuwaeleza pande zote za nyumbani kwetu na kwa mwanamume.”
Mahakama inaweza kuamua
Kimaro ambaye ni wakili, amesema familia zikishindwa kufikia mwafaka, suala linaweza kupelekwa mahakamani na hapo Mahakama huzingatia ushahidi kwa aliyekuwa karibu na marehemu, aliyemhudumia wakati wa ugonjwa na kama aliwahi kueleza matakwa yake kabla ya kufariki.
“Mahakama haitazingatia uhusiano wa damu au ndoa pekee, bali mazingira halisi ya maisha ya marehemu na ushahidi uliopo,” amesema.
Kufufuliwa migogoro ya zamani
Mwanasaikolojia Clara Mwambungu amesema mara nyingi ugomvi wa maiti huwa mwendelezo wa migogoro iliyokuwepo kabla ya kifo ambayo ndugu walikuwa hawaelewani kwa miaka mingi kutokana na migogoro ya mali, urithi au uhusiano, kifo kinapotokea tofauti hizo hujitokeza kwa nguvu zaidi.
"Utakuta mtu hajawahi kuonana na ndugu yake kwa miaka mingi, lakini anapofariki anataka kushiriki kikamilifu katika uamuzi wa mazishi na kuhitaji kusikilizwa kwa kila kitu na hapo ndipo migogoro huanzia," amesema Clara.
Mtaalamu huyo amesema baadhi ya ndugu hutumia msiba kama nafasi ya kuthibitisha mamlaka yao mbele ya jamii au kulinda heshima ya ukoo jambo ambalo wengi wao hawakubaliani nalo na kutokuwepo kwa uwazi kuhusu mahusiano ya marehemu.
Athari zake
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Iringa, Anastazia Eliya amesema watoto ndio kundi linaloumia zaidi pale familia zinapogombania maiti.
Amesema watoto wanaompoteza mzazi tayari huwa katika maumivu makubwa ya kihisia, lakini wanaposhuhudia ndugu wakitukanana na kugombana hali hiyo huongeza majeraha ya kisaikolojia.
"Wapo watoto wanaobaki na hofu, msongo wa mawazo na chuki kwa baadhi ya ndugu kutokana na matukio wanayoyaona wakati wa msiba wa mzazi wao au wanaposimuliwa kisa kizima," amesema Anastazia.
Dini zinasemaje?
Mchungaji Joshua Mwakalinga wa Kanisa la Upendo la Tanzania, lililopo Uyole, jijini Mbeya amesema migogoro ya kugombea maiti imekuwa ikiondoa maana halisi ya maombolezo yanayopaswa kuwa kipindi cha kuungana, kufarijiana na kumuombea marehemu.
Amesema badala ya wanafamilia kushirikiana katika kipindi kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao, baadhi yao hujikuta wakigawanyika katika makundi yanayopingana, hali inayosababisha maumivu kwa waliofiwa na hata kuharibu uhusiano wa kifamilia uliokuwepo kwa miaka mingi.
"Tunapaswa kukumbuka marehemu hawezi tena kujitetea wala kutoa uamuzi, wajibu wa familia ni kuhakikisha anaagwa kwa heshima na amani, si kugeuza mazishi kuwa sehemu ya migogoro na malumbano," amesema Mwakalinga.
Naye, Sheikh Rashid Kiondo wa Msikiti wa Mongolandege, jijini Dar es Salaam, amesema kitendo cha kugombea mwili wa marehemu huondoa heshima anayostahili marehemu na kuwaachia maumivu zaidi kuliko yale ya kumpoteza mpendwa wao.
"Kama kuna tofauti kati ya wanafamilia, ni muhimu zitatuliwe kwa mazungumzo na busara, msiba si wakati wa kushindana wala kulipizana kisasi, bali ni wakati wa kuonesha upendo, mshikamano na kuheshimu utu wa marehemu," amesema Sheikh Kiondo.