Miili ya wanafamilia 13 waliofariki ajalini Tanga kuzikwa Rombo

Muktasari:

 Miili 13 ya familia moja kati ya 17 waliofariki kwa ajali ya gari Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga   inatarajiwa kuwasili leo jioni, Februari 4, 2023 katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya taratibu za maziko.


Rombo. Miili 13 ya familia moja kati ya 17 waliofariki kwa ajali ya gari Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga   inatarajiwa kuwasili leo jioni, Februari 4, 2023 katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya taratibu za maziko.

Ajali hiyo ilitokea jana usiku katika eneo la Magira Gereza, Kata ya Magira Gereza wilayani Korogwe, Barabara ya Segera - Buiko na kusababisha vifo hivyo pamoja na majeruhi 12.

Ndugu hao pamoja na majirani walikuwa wakisindikiza mwili wa mwanafamilia mwenzao, Athanas Mrema (59) aliyefariki dunia Februari Mosi, kutokea Dar es salaam kuja mkoani Kilimanjaro ndipo walipokutana na ajali hiyo  mbaya.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Februari 4, msemaji wa familia ukoo wa Mrema, Colman Mrema amesema miili ya ndugu wa nne itazikwa sehemu moja na ndugu wengine ambao ni watoto wa baba wadogo na mashangazi watazikwa katika maeneo mengine wilayani humo.

"Kifo hiki kwa kweli kimetuhuzunisha maana ni msiba juu ya msiba na leo hii tulikuwa tumzike ndugu yetu Athanas lakini jana usiku tukapata taarifa na wale waliokuwa wanaleta nao wamefariki ni masikitiko," amesema.

"Ni msiba ambao haujawahi kutokea katika kijiji hiki na hata wilaya nzima kwa kweli msiba ambao hauelezeki, kwa mtazamo wa kawaida," amesema.

Mwenyekiti wa Halamshauri ya Wilaya ya Rombo, Gilbert Tarimo amesema wataipokea miili hiyo jioni na miili 10 itahifadhiwa katika Hospitali ya Huruma, na miili mingine katika kituo cha afya Karume.

Hata hivyo taratibu za maziko zinaendelea nyumbani hapo katika Kitongoji cha Kirungu Mokala, Kata ya Kelamfua Mokala na miili hiyo itazikwa siku moja katika maeneo tofauti.