Miili ya wanandoa wapya kuzikwa leo Mbeya

Askari polisi wakiwa wamebeba majeneza yenye miili ya askari wenzao waliofariki kwa ajali ya gari (mtu na mkewe) wakati wa ibada ya kuwaaga iliyofanyika mkoani Iringa jana kabla ya kusafirisha kuelekea Mbeya kwa mazishi. Picha na Tumaini Msowoya

Muktasari:

Wingu la simanzi lilitanda katika eneo la Kituo cha Polisi Mjini Iringa, wakati miili ya wanandoa wapya ambao ni askari polisi Mkoa wa Arusha waliopoteza maisha kwa ajali ya gari eneo la Tanangozi, nje kidogo ya Manispaa ya Iringa ikiagwa.

Iringa. Wingu la simanzi lilitanda katika eneo la Kituo cha Polisi Mjini Iringa, wakati miili ya wanandoa wapya ambao ni askari polisi Mkoa wa Arusha waliopoteza maisha kwa ajali ya gari eneo la Tanangozi, nje kidogo ya Manispaa ya Iringa ikiagwa.

Wanandoa hao, Noah Semfukwe (30) na Agnes Kiyeyeu (27) walifariki dunia Jumanne wiki hii na watazikwa leo katika kijiji cha Makongolosi, Chunya mkoani Mbeya.

Noah na Agness waliodumu kwenye ndoa kwa siku tatu, walifunga pingu za maisha Desemba 17, mwaka huu.

Ajali hiyo ilitokea saa 3 asubuhi katika eneo hilo wakati gari dogo aina ya Vits iliyokuwa ikiendeshwa na Noah ilipopanda tuta na mbele yake kukawa na lori, hivyo wakati analikwepa akakutana uso kwa uso na basi la Luwizo lililokuwa likitokea Njombe kwenda Dar es Salaam.

Katika ajali hiyo watu watatu walipoteza maisha, akiwemo Enocka Mbata (35), mkazi wa Iringa aliyekuwa kwenye gari hilo na mwili wake ulizikwa juzi Iringa.

Miongoni mwa viongozi wa Jeshi la Polisi waliokuwepo katika shughuli hiyo ya kuaga marehemu hao ni mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Benedict Wakulyamba. Akitoa salamu kwenye msiba huo, Mwakulyamba alisema kifo cha askari hao kimeacha pengo kubwa kwa jeshi hilo.

Alisema askari mmoja ana umuhimu mkubwa katika kulinda mali na raia, hivyo kuondokewa na askari wawili ni pengo kubwa zaidi na kuwataka ndugu kuwa na subira hasa wakati huu wa maombolezo.

Baadhi ya waombolezaji walisema vifo vya wanandoa hao vimesababisha huzuni hasa ikizingatiwa walitoka kufunga pingu za maisha siku chache zilizopita.

“Inaumiza sana, nimesikitika lakini Mungu ndiye mpangaji wa kila kitu, sisi hatuna cha kufanya,” alisema Hilda Kiyeyeu, mmoja wa waombolezaji.

Alisema alipata taarifa za ajali hiyo juzi jioni akiwa kijiji cha Mgama, wilayani Iringa. “Agness ni ndugu yangu, hatuna cha kusema zaidi tunashukuru kwa faraja tunayopewa,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi alitoa pole kwa jeshi hilo, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na msiba huo.

Pia aliwakumbusha madereva kuwa makini barabarani, hasa wakati huu wa msimu wa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya. “Usione una haki ukalazimisha kupita eneo ambalo unaona mwenzako anafanya ndivyo sivyo, kwa hiyo chukua tahadhari ili kuepusha ajali. Tuwe waangalifu,” alisema Bukumbi.

Pia aliwataka watembea kwa miguu kuwa makini, huku madereva wakitakiwa kuchukua tahadhari kwenye maeneo ambayo yana msongamano mkubwa wa watu.