Miili ya watu sita wa familia moja waliouawa yazikwa pamoja
Muktasari:
Watu hao sita wa familia ya Mussa Cheche waliuawa kwa kukatwa katwa sehemu mbalimbali za miili yao kwa kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumapili Julai 3, 2022 wakiwa wamelala.
Kigoma. Miili ya watu sita wa familia moja waliouawa kwa kukatwa na kitu chanye ncha kali na watu wasiojulikana imezikwa katika Kijiji cha Kiganza, wilayani Kigoma mkoani Kigoma.
Miili hiyo imezikwa kwa pamoja jana Jumapili Julai 3, 2022 usiku.
Watu hao waliuawa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana wakiwa nyumbani kwao wamelala huku watoto wawili, mmoja mwenye umri wa miezi mitatu na mwingine miaka minne wakijeruhiwa.
Jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Menrad Sindano alithibitisha mauaji hayo huku akisema kuwa Jeshi hilo limeanza msako wa waliofanya unyama huo.
Sindano alisema kuwa watoto waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Maweni
Wakizungumza katika mazishi hayo baadhi ya wananchi wa eneo hilo waliiomba Serikali kuongeza vituo vya polisi ili kuimarisha ulinzi na usalama.
Mkazi wa kijiji hicho, Abed Said amesema tukio hilo limeacha huzuni katika maeneo hayo.
Ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kuongeza ukaguzi wa wageni wanaoingia nchini.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Ally Ahmad amesema mauaji hayo yamesababisha hofu katika familia kutokana na tukio hilo kuwa geni.
Watu hao sita wa familia ya Mussa Cheche waliuawa kwa kukatwa katwa sehemu mbalimbali za miili yao kwa kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumapili Julai 3 mwaka huu wakiwa wamelala.