Miili ya watu watatu yaokotwa porini Mtwara

Muktasari:

Miili ya watu watatu ambao ni waendesha pikipiki maarufu bodaboda imeokotwa katika msitu ya Kijiji cha Hiari wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.

Mtwara. Miili ya watu watatu ambao ni waendesha pikipiki maarufu bodaboda imeokotwa katika msitu ya Kijiji cha Hiari wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.

Akizungumza na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo amesema kuwa tukio la kwanza limetokea katika Kijiji cha Hiati ambapo viliokotwa viungo vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu ambavyo ni mifupa, ugoko na utumbo mdogo.

Amesema viungo hivyo vinadhaniwa kuwa ni vya mwendesha bodaboda, Kelvin Mbale ambaye alitoweka tangu Februari 2, 2022.

Kamanda Katembo amesema katika eneo la tukio zilipatikana nguo na viatu ambapo ndugu za walivitambua kuwa vilikuwa vya marehemu.

Kamanda huyo amesema kuwa katika tukio la pili linahusisha mauaji ya Mohamed Juma ambaye anadaiwa kuuawa na watu wasiojulikana kwa kuchomwa kitu chenye ncha kali

 Amesema kuwa tukio hilo limetokea Februari 12, 2022 katika huko maeneo ya pori la Majengo Wilaya ya Mtwara.

Amesema kuwa taarifa zinaonyesha kuwa Juma alipakia watu wawili wakiwa na mabegi mgongoni na kuelekea kusikojulikana na baadaye bodaboda wenzake walianza kumtafuta maeneo kukukuta mwili wake katika pori hilo.

Mwili huo umepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula kwa ajili ya kuhifadhiwa huku ukisubiri ndugu wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi.

Katembo amesema Februari 15, 2002 Polisi walipokea taarifa ya kupatikana kwa mwili mwendesha bodaboda, Mohamed Juma Mohamed (22).

Kaimu Kamanda wa Polisi Mtwara amesema upelezi wa matukio hayo unaendelea kuwabaini wote waliohusika na mauaji hayo.

"Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea na msako, operesheni na ukusanyaji wa taarifa za kiitelijensia kukomesha aina zote za uhalifu" amesema Katembo.

Taarifa za awali kutoka kwa waendesha bodaboda katika maeneo mbalimbali ya halmashauri ya Manispaa ya Mtwara  Mikindani zinadai kuwa kuanzia Januari mwaka huu waendesha bodaboda nane wamepotea baada ya kukodiwa na watu wasiojulikana.

Akizungumza kwa niaba ya waendesha bodaboda zaidi ya mia moja ambao wameendesha operesheni maalumu ya kumsaka mwenzao katika msitu wa Kijiji cha Hiari, Hamis Mohamed ameiomba Serikali kufutilia taarifa za mauaji hayo.

Juma Hassan ambaye pia ni mwendesha bodaboda wa maeneo ya Dangote ameliomba Jeshi la Polisi kushirikiana na waendesha bodaboda kuwatambua wanaofanya vitendo hivyo vya mauaji.