Milipuko mabomu ya Mbagala yatafuna Sh17 bilioni

Bomu likiwa limeharibu moja ya nyumba iliyopo katika eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Mabomu hayo yalilipuka Aprili 29, 2009 katika Kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) KJ 671 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 25, huku mamia ya watu wakijeruhiwa na familia nyingi kukosa makazi baada ya nyumba zao kubomoka kabisa.

Dodoma. Jumla ya Sh17.4 bilioni zimetumika kutoa mkono wa pole kwa wananchi 12,647 walioathirika na milipuko ya mabomu yaliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi Mbagala jijini Dar es Salaam.

Mabomu hayo yalilipuka Aprili 29, 2009 katika Kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) KJ 671 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 25, huku mamia ya watu wakijeruhiwa na familia nyingi kukosa makazi baada ya nyumba zao kubomoka kabisa.

Akijibu swali bungeni leo Novemba 2, 2022 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene ambaye amesema kilichotokea ni mkono wa pole siyo fidia.

Katika swali la msingi Mbunge wa Mbagala (CCM), Abdallah Chaurembo ametaka kujua nini kauli ya Serikali juu ya mapunjo kwa wananchi walioathirika na mlipuko wa mabomu Mbagala ambao ulitokea Aprili 29, 2009.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), George Simbachawene akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma, Novemba 2, 2022

Waziri Simbachawene amesema katika tukio Serikali iligharamia huduma za mazishi kwa familia 29 zilizopoteza wapendwa wao kutokana na milipuko hiyo ya mabomu.

"Zoezi la kutoa mkono wa pole kwa waathirika lilisitishwa rasmi na Serikali mweziachi 2020 baada ya walengwa wote waliokusudiwa kujitokeza na kulipwa," amesema Simbachawene.

Hata hivyo Waziri ameliambia Bunge kuwa bado kuna watu wanaodai kifuta machozi na wamekuwa wakifiatilia malalamiko yao kuhusu uhalali.