Mipango miji wapewa kibarua kipya fedha za miradi

Muktasari:

  • Wataalam wa mipango miji nchini ametakiwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi ili kupata fedha nje ya mfumo wa kiserikali ambazo zitawawezesha kutekeleza shughuli zao, sambamba na kuleta suluhisho  ya migogoro na migongano ya ardhi itokanayo na ukuaji wa miji.

Arusha. Wataalam wa mipango miji nchini ametakiwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi ili kupata fedha nje ya mfumo wa kiserikali ambazo zitawawezesha kutekeleza shughuli zao, sambamba na kuleta suluhisho  ya migogoro na migongano ya ardhi itokanayo na ukuaji wa miji.

Kibarua hicho kimetolewa leo June 8, 2023 na Mkuu wa mMkoa wa Arusha, John Mongela wakati akifungua mafunzo ya namna ya kuandaa maandiko ya kusaka fedha nje ya mfumo wa serikali kwa wataalamu wa mipango miji kutoka halmashauri zote za mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Mongela alisema kuwa changamoto mbalimbali za mipango miji imekuwa ikiigharimu serikali, hali ambayo inasababisha kuwepo uhitaji wa kuwa na utalaam wa kutafuta fedha ambazo zitawezesha utatuzi wa matatizo yanayowakabili wananchi ikiwemo migogoro ya Ardhi.

"Kasi ya ukuaji wa miji unaoambatana na ongezeko la watu, imekuwa chanzo kikubwa cha matatizo mbalimbali ikiwemo kuzidiwa kwa miundombinu ya mahitaji muhimu ya binadamu kama afya, elimu barabara na maji, hivyo lazima mkae mtafute suluhisho wenyewe," alisema.

Amesema kuwa serikali imetoa fedha kwa ajili ya umilikishaji pekee, hivyo kuwataka wataalam hao kusaka fedha nje ya mfumo wa serikali kwa ajili ya shughuli zingine za mipango miji.

"Natambua kwamba upangaji na upimaji wa maeneo unategemea upatikanaji wa rasilimali ikiwemo fedha, wataalam pamoja na vitendea kazi na serikali imetoa bilioni 50 kwa ajili ya umilikishaji wa maeneo hivyo Bado inahitajika juhudi kubwa upande wenu wataalam kusaidia kipande kilichobaki"

Akizungumzia semina hiyo Msajili, Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipango Miji (TPRB) Lucas Mwaisaka amesema kuwa, uhaba wa rasilimali fedha umekuwa changamoto katika utekelezaji wa miradi ya mipango miji hali inayopelekea kukithiri kwa migogoro ya ardhi nchini.

"Miradi mingi ya mipango miji inakwama kutokana na tunategemea kutekeleza kwa kutumia fedha za serikali ambazo zinatoka kibajeti, ndio maana kama bodi tumeamua kuwanoa wataalamu hawa, juu ya namna ya kuandaa maandiko ya kusaka rasilimali fedha nje ya mfumo wa Serikali," amesema.

Amesema mafunzo hayo yanayotolewa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), na kwamba wanategemea kupata wataalam watakaoisaidiana na wadau wa ndani na nje ya nchi, ili kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali katika kutekeleza miradi ya upangaji miji.

Nae Mjumbe wa bodi ya TPRB Regina Lyakurwa, amesema ipo mipango mingi ambayo imekuwa ikipangwa lakini haitekelezwi kutokana na ukosefu wa fedha, hivyo elimu tajwa itawasaidia maafisa hao kutumia fursa au changamoto zilizopo kuandaa andiko la kupata fedha na hivyo kutatua matatizo hayo.

"Ni vikumu kwa Serikali kuwa na fedha za kutosha kutekeleza miradi yote katika sekta zote, hivyo lazima wataalam wa sekta hii wabuni vyanzo vya mapato yao kutoka maeneo mengine ili waweze kutekeleza mipango ya maendeleo," amesema.

Naye Ofisa Mipango Miji Jiji la Arusha Dorothy Absolum amesema kuwa Mafunzo hayo yanaenda kutatua changamoto ya mipango miji wanayokumbana nazo kutokana na ukosefu wa fedha za kutekeleza na kusimamia miradi.