Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mirembe yatoa mafunzo ya matumizi ya dawa za afya ya akili kwa watoto

Mratibu wa mafunzo, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wataalamu wa Teknolojia ya Dawa Tanzania (TAPHATA), Thabit Milandu, akizungumza wakati wa mafunzo yaliyowakutanisha wataalamu wa teknolojia ya dawa. Picha na Elidaima Mangela.

Muktasari:

  • Mafunzo hayo yamehusisha kupunguza makali ya dawa na kubadili dawa hizo kutoka mfumo wa vidonge kwenda kwenye mfumo wa maji ili kuwawezesha watoto hao kutumia dozi sahihi kulingana na matatizo waliyonayo.

Dodoma. Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe imetoa mafunzo ya urekebishaji wa kiwango cha dawa kwa wataalamu wa famasia ili kuboresha utoaji wa matibabu sahihi kwa watoto wenye matatizo ya afya ya akili ambao huhitaji dozi maalumu kulingana na ukubwa wa tatizo, hali zao za kiafya na umri.

Mafunzo hayo yamekuja baada ya kubainika kuwa baadhi ya watoto wenye matatizo ya afya ya akili hawawezi kutumia dawa zilizo katika mfumo wa vidonge kutokana na makali ya dawa hizo, na wengine huhitaji kiwango cha dawa ambacho hakipatikani katika aina ya dawa zilizopo, hivyo ni lazima zipunguzwe makali au zibadilishwe.

Akizungumza katika mafunzo hayo leo Jumamosi, Julai 11, 2026, Mratibu wa Mafunzo, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wateknolojia wa Dawa Tanzania (TAPHATA), Thabit Milandu, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwezesha uandaaji wa dawa katika viwango vinavyolingana na mahitaji ya kundi hilo ili kuwawezesha kupona kwa wakati.

“Tumefanya mafunzo haya baada ya kugundua kuwa kuna changamoto ya kiwango cha dawa kinachohitajika kwa wagonjwa wetu wenye matatizo ya afya ya akili, ikiwemo mahitaji ya kiwango cha dawa kwa mgonjwa kutokana na umri,” amesema Milandu.

Amesema mafunzo hayo yamewakutanisha wataalamu wa Idara ya Famasi kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, wanafunzi wa vyuo, watumishi kutoka halmashauri za Bahi na Kondoa, wataalamu kutoka Bohari ya Dawa (MSD), Baraza la Famasi, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) na Wizara ya Afya.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa wafamasia kuhusu urekebishaji wa kiwango cha dozi kwa watoto wadogo wenye matatizo ya afya ya akili kwa kupunguza ukali wa dozi na kuifanya iwe katika kiwango kinachohitajika ili kuwawezesha kupona kwa wakati.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk Innocent Mwombeki, amesema mafunzo hayo pia yataamsha ari ya matumizi ya fani ya famasi katika kuzalisha dawa na vifaa tiba, badala ya kujikita katika kugawa dawa pekee kama inavyoaminika na wengi kwa sasa.

Amesema yatasaidia kuongeza matumizi ya wataalamu wa ndani ya nchi katika uzalishaji wa dawa, hali itakayoongeza ufanisi katika upatikanaji wa bidhaa hizo nchini na kuondoa utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

“Tunajua uzalishaji wa dawa nchini upo chini, hivyo ni lazima tuweke mikakati ya muda mrefu na mfupi ili kuondoa tatizo hili, na miongoni mwa njia hizo ni kuzalisha wataalamu bobezi wenye uwezo wa kuzalisha dawa ndani ya Taifa letu,” amesema Dk Mwombeki.

Aidha, mshiriki wa mafunzo hayo, Lorraine Mpasi, ambaye pia ni mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Famasia kutoka Chuo Kikuu cha St. John, ameomba kutatuliwa kwa adha ya mlolongo mrefu katika upitishwaji wa bunifu wanazofanya katika sekta ya afya ili zipate kibali cha kutumika katika sekta hiyo.

Lorraine pia ameomba kuwepo kwa chanzo kimoja cha kuaminika cha uzalishaji wa malighafi za utengenezaji wa bidhaa za afya ili kuwasaidia kutengeneza bidhaa zenye ubora na zinazokubalika sokoni.