Misa-Tan yataka mamlaka husika kumtafuta Azory Gwanda

TAMKO LA MWANANCHI COMMUNICATIONS LIMITED KUPOTEA KWA MWANDISHI AZORY GWANDA

Muktasari:

Zimepita siku 22 tangu Gwanda atoweke baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana wilayani Kibiti mkoani Pwani.

Dar es Salaam. Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (Misa-Tan) imeeleza kuguswa na tukio la kupotea kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Azory Gwanda ikitoa wito kwa mamlaka husika kumtafuta hadi apatikane.

Wito wa Misa-Tan umetolewa leo Jumanne Desemba 12,2017 ikiwa zimepita siku 22 tangu Gwanda atoweke baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana wilayani Kibiti mkoani Pwani.

Misa-Tan imesema imepokea barua ya Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai yenye kichwa cha habari ‘Kupotea kwa mwandishi Azory Gwanda’.

Awali, taarifa iliripotiwa katika kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kibiti Novemba 23 na mke wa Azory kuwa mume wake amepotea tangu Novemba 21,2017.

“Katika taarifa iliyotolewa na MCL Desemba 4,2017, Nanai alisema Polisi katika wilaya hiyo iliahidi kushughulikia suala hilo lakini hakuna kilichofanyika na mahali alipo Azory kumebaki kuwa kitendawili,” imesema taarifa ya Misa-Tan iliyosainiwa na mwenyekiti, Salome Kitomari.

Amesema, “Fikra na maombi yetu yanakwenda kwa familia ya Azory, ndugu na marafiki katika kipindi hiki. Tunaziomba mamlaka zinazohusika kufanya kila jitihada kumpata Azory na kutoa taarifa kwa kila mtu anayempenda.”

Misa-Tan ambayo lengo lake ni kutetea na kuimarisha wingi wa vyombo vya habari; kutetea uhuru wa kujieleza na haki ya kupata taarifa, imesema vyombo vya habari vinaungana na kusimama pamoja na Azory, familia yake na marafiki zake.