Mitandao ya kijamii yamtoa kimaisha

Dar es Salaam. Asilimia kubwa ya matumizi ya mitandao ya kijamii imeongezeka kwa kasi nchini Tanzania inayopelekea  kuibua mambo mbalimbali ikiwemo kutumika vibaya kwa mitandao hiyo lakini vile vile wengine hutumia kujenga jamii na shughuli za uchumi.

Upande wa kujenga jamii na kutoa hamasa kwa watanzania yupo, Jesca Wilfredy Macha au kwa jina la kimtandao Jesca Wilfredy ameelezea faida za matumizi ya mitandao ya kijamii kwa upande wake kumtoa kimaisha.

Akizungumza na Mwananchi Online, amesema watu wengi maarufu wa kwenye mitandao ya kijamii bado hawajajua namna nzuri ya kutumia mitandao hiyo ili kuleta mafanikio au fursa mbali mbali katika maisha.

"Ukiitumia mitandao ya kijamii kwa manufaa zaidi itakuletea matokea chanya na utawezafanya mambo yako bila shida" asema Jesca.

Jesca ambaye ni mjasiriamali na moja ya watu maarufu mitandaoni amekuwa chachu kwa vijana wadogo wa kike katika kuwahamasisha kwenye suala la kujifunza namna ya kujitegemea na kuwa mjasiriamali.

Licha ya umaarufu wake, Jesca amesema kwamba njia pekee anayoweza kuwafikia vijana wengi na hata wateja katika mambo mbalimbali kwa sasa ni kupitia mitandao ya kijamii.

“Nilianza kwa kuposti baadhi ya huduma zangu kupitia kurasa zangu za mitandao ya kijamii lakini leo nimeweza kufungua duka langu la nguo Kariakoo, wateja wangu wengi ni wale wale ambao ni wafuasi wangu katika kurasa zangu za mitandao ya kijamii.”