Mjadala wa bandari ulivyowagawa vigogo

Dar es Salaam. Mjalada wa mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa uwekezaji na uboreshaji wa bandari nchini kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai umeendelea ukishuhudiwa sura mbili tofauti.

Wanasiasa, wanasheria, wachumi na makundi mengine yametofautiana kuhusu ushirikiano huo kati ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Dubai kupitia Kampuni yake ya Dubai Port World (DPW).

Mjadala huo ulianza mapema mwezi huu baada ya mkataba huo wa ushirikiano wa awali (IGA) baina ya Tanzania na Dubai kusambaa mitandaoni. Juni 10 mwaka huu, Bunge liliridhia azimio la kuruhusu ushirikiano huo.

Mjadala huo unapata uzito zaidi kila kukicha kutokana na kuwaibua waliowahi kuwa vigogo serikalini, kila mmoja akizungumzia kwa mtazamo wake huku wabobezi wa sheria na uchumi wakiwa miongoni mwa wanaouchambua ushirikiano huo.
Baadhi ya vigogo walioibuliwa na sakata hilo ni, mawaziri wakuu wastaafu, Jaji Joseph Warioba na John Malecela.

Wengine ni Balozi Wilbrod Slaa, viongozi wa dini, mfanyabiashara maarufu, Rostam Azizi na waziri wa zamani wa ardhi, Profesa Anna Tibaijuka.

Pia, wamo profesa wa sheria, Issa Shivji, wenyeviti wa vyama vya siasa, Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Mbali na vigogo hao kutofautiana kimitizamo, viongozi wa TPA, wizara wa ujenzi na uchukuzi wakiongozwa na waziri wake, Profesa Makame Mbarawa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Samia Suluhu Hassan wamezungumzia suala hilo.

Hoja zinazojirudia zaidi kutoka kwa wanaoupinga ni ukomo wa mkataba, nchi itakavyonufaika, suala la ajira, utatuzi wa migogoro, ukinzani wa sheria, jinsi ya kuusitisha na au kuuvunja mkataba na suala la bandari ni la muungano au la.

Kutokana na mgawanyiko huo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema ameyaona makundi hayo, wakiwamo wanaounga mkono mkataba wanaona hauna dosari, hivyo wanaona wanaopinga ni wapotoshaji.

“Ila hawa wanaopinga wanaingia ndani kwa kutaja dosari kifungu kwa kifungu. Hivyo, inabidi hawa wanaounga mkono wawasikilize.

“Mambo haya ya rasilimali za Taifa kama madini, maliasili, wanyama na sasa hii bandari hayapaswi kutugawa, bali yatulete pamoja kwa kuangalia upungufu na kufanyia kazi. Tusije tukapitisha mkataba utakaohatarisha uhuru wa nchi,” alisema Dk Mbunda.

“Inawezekana baada ya miaka mitano ikatokea kampuni nyingine yenye teknolojia kubwa kuliko hiyo DP World, halafu tukashindwa kuikaribisha maana mkataba wetu hauna ukomo, kwa sababu mambo ya teknolojia yanabadilika haraka.”

Dk Mbunda anaungwa mkono na mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), Dk George Kahangwa akisema hali iliyojitokeza kwa kugawanyika kwa mitizamo ya wazi, “ni busara kusimama na kufanyiwa jambo kisawasawa na mwenye uwezo ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan”.

“Rais ana uwezo wa kuwaita wote wanaoupinga na kuwasikiliza ili kulifanya jambo hili kuwa shirikishi na yeye atatusaidia kutoa mwelekeo wa mwisho wa jambo hili,” alisema Dk Kahangwa.

“Ukisikiliza wale wanaotetea kwa nini tufanye hivyo, wanasema tumeshindwa kuendesha wenyewe, basi ni aibu kama Taifa na inaweka hata maswali juu ya uadilifu wetu, kuweka maswali juu ya elimu yetu tulivyojitayarisha katika kujitegemea.”

Dk Kahangwa alisema kama msingi mkubwa wa kuwekeza kwenye bandari ni kutokuwa na rasilimali fedha, “ina maana kama sababu ni kushindwa kuendesha bandari, sisi wenyewe kila kinachotushinda ni kwenda huko, tukishindwa kifedha na kitaalamu tutakwenda huko madamu tuna sera ya uwekezaji. Tunahitaji kujenga uwezo wetu wenyewe.”
 

Alichokisema Rais Samia

Tangu awali, TPA kupitia Mkurugenzi Mkuu, Plasduce Mbossa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wamekuwa wakiutetea mkataba huo kupitia vyombo vya habari.
Licha ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kusoma azimio la mkataba huo bungeni ili kuridhiwa, amekuwa pia akitoa ufafanuzi kutetea uwekezaji huo.

Wakati mjadala huo ukianza kushika kasi, baada ya Bunge kuridhia azimio hilo, Juni 13 mwaka huu, baada ya kuwasili jijini Mwanza kwa ziara ya kika-zi, Rais Samia alizungumzia sakata hilo, ikiwamo hoja kuwa nchi inauzwa na madai ya kauli za kibaguzi.

“Salamu moja kubwa ni kwamba, mama huyu ni Mtanzania, atafanya kila analoweza kufanya Tanzania iendelee na Tanzania ni moja, haigawanyiki wala haiuziki,” alisema Rais Samia.

“Kwa hiyo ndugu zangu, mama ni Mtanzania, maendeleo yetu ni muhimu, kila linalofanyika ni kwa maendeleo ya Watanzania.” Kama hiyo haitoshi, Juni 24 akiwasili mkoani Arusha alikokwenda kwa ajili ya maadhimisho ya kupiga vita dawa za kulevya, Rais Samia alizungumza na wananchi waliokuwa wamejitokeza kumpokea katika eneo la Tengeru.

“Mimi sina maneno mengi, vitendo ndio vingi, wakisema nafanya masikio hivi, naangalia wapi nakwenda; kwa hiyo waseme, sisi tunafanya, tunajenga kesho kwa ajili ya vijana, Serikali yenu iko makini na tuko sober tunajipanga vyema kuwatumikia wananchi,” alisema Rais Samia.

Jana, akitoa salamu kwenye Baraza la Eid-Adh’ha katika Msikiti wa Mohammed wa VI, Kinondoni jijini, Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizungumzia kwa mara ya tatu kuhusu sakata hilo akisema, Serikali itafanyia kazi maoni na ushauri wote unaotolewa na wananchi.
Majaliwa. aliyemwakilisha Rais Samia alisema kilichopitishwa na Bunge ni makubaliano ya ushirikiano baina ya Tanzania na Dubai.

“Kilichofanyika kwanza ni kuanza kutengeneza makubaliano yanayoweka misingi kwenye eneo husika. Kwa hiyo, Tanzania imekubaliana kuwa na uhusiano kwenye eneo la uwekezaji wa Bandari na Dubai na ndilo azimio lililopelekwa bungeni kuridhiwa,” alisema Majaliwa.

Baada ya makubaliano hayo, alisema yatafuatia makubaliano kuhusu maeneo ambayo DP World inapaswa kufanyia kazi na hapo ndipo Serikali itakapozingatia maoni ya wananchi.

“Kwenye maeneo ya uwekezaji hapo sasa ndipo tutazingatia maoni yenu, lakini hatuchukii mkishauri, mkitoa maoni ni jambo zuri,” alisema huku akisisitiza kinachofanywa na DP World si kuchukua bandari, bali itapewa baadhi ya maeneo kwa ajili ya kufanya kazi yake.

Majaliwa alisema umiliki wa bandari utaendelea kusalia TPA kwa mujibu wa sheria: “Tunachokifanya ni kama ilivyokuwa kwa TICTS (Kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania), atapewa maeneo ya kufanyia kazi na atafanya hayo.”
Majaliwa alitoa kauli hiyo baada ya Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma kuishauri Serikali kupokea maoni ya wananchi na kufafanua vifungu vinavyowatia shaka.

“Nitoe wito kwa Serikali kupokea maoni ya wananchi na kufafanua maeneo yote yanayotiliwa mashaka,” alisema Mruma wakati akitoa salamu za baraza hilo.
Juni 27 katika kipindi cha Jambo Tanzania cha Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) jijini Dodoma, Spika Tulia Ackson alizungumzia suala hilo akisema Serikali imeingia makubaliano na Serikali ya Dubai, sio mkataba.

“Yale ni makubaliano sio mkataba, kwa nini imekuja bungeni? Kwa sababu Katiba inataka hivyo, maana aina ya makubaliano haya yanataka chombo ambacho nchi imekipa madaraka kuridhia,” alisema Spika Tulia.
 

Kuibuka kwa AG

Baada ya kimya kingi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Eliezer Feleshi naye aliibuka kwa mara ya kwanza kuzungumzia suala hilo Juni 26 mwaka huu.

Kupitia video fupi iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii ilimwonyesha Dk Feleshi akieleza masuala mbalimbali yaliyopo katika mkataba, ikiwamo hoja ya ukomo wa mkataba huo, miongoni mwa vipengele vilivyokuwa gumzo.

“Mtu anasema mkataba wa miaka 100 au maisha, hii ilikuja kabla ya Bunge kuazimia, lakini ukipekua vifungu kimoja hadi mwisho hakuna,” alisema Dk Feleshi, aliyewahi kuwa Jaji Kiongozi.

Alifafanua kati ya miongo mitatu au miwili ya nyuma Tanzania ilisaini na kukubaliana kuhusu matumizi ya mabaraza mengine ya kimataifa katika utatuzi wa migogoro, akisema bado Taifa halijajiondoa katika mchakato huo.

Viongozi wengine waliotetea makubaliano ya mkataba huo wa ushirikiano ni Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela aliyesema hauna shida kwa kuwa umechelewa kutokana na ufanisi wa bandari ulivyo sasa.

Pia, mfanyabiashara na wanasiasa, Rostam Aziz mara kadhaa alisema uwekezaji huo utakuwa na tija huku akiishauri Serikali kushughulikia maeneo yenye changamoto kwenye mkataba huo.
 

Wanaoukosoa

Baadhi ya vigogo wanaoukosoa ni Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, Balozi Wilbrod Slaa, viongozi wa dini, TLS, waziri wa zamani wa ardhi, Profesa Anna Tibaijuka, Profesa wa sheria, Issa Shivji, wenyeviti wa vyama vya siasa, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF).

Juzi, katika mjadala uliofanyika UDSM, gwiji la sheria, Profesa Shivji alisema hatua hiyo ya Serikali kuingia makubaliano hayo ni sawa na kujifunga mikono kabla hata ya kwenda kusaini mikataba ya utekelezaji.

Alitoa mfano wa ubinafsishaji wa Benki ya NBC, akisema Serikali iliruhusu mwekezaji akaingia hadi chumbani na kuiba siri zote kabla hata hajasaini mkataba.

“Kuna sekta nyeti katika uchumi na huwezi kuweka katika kampuni ya watu binafsi; na bandari ni sekta nyeti, ni roho na mishipa ya uchumi, hivyo huwezi kuweka katika mikono ya watu binafsi kwa sababu mbalimbali,” alisema Profesa Shivji.

Kuhusu ukomo wa mkataba, Profesa Shivji alisema, “waliposema miaka 100 hawakumaanisha ni miaka 100, walichomaanisha ni kwa muda mrefu. Ni kweli muda mrefu. Mkataba huu utaishi pale ambako mikataba yote ya mradi ya kwanza awamu saba imetekelezwa.

“Kila mkataba utakuwa na muda wake na muda huo hautakuwa mdogo, unaweza kuwa miaka 20, miaka 30 na kadhalika na unaweza kuongezwa. Kwa hiyo mtu akisema mkataba hauna kikomo yuko sahihi,” alisema.

Kuhusu faida, Profesa Shivji alisema mkataba huo hauna kifungu kinachoonyesha mgawanyo wa mapato.

“Hii hela itakwenda kwa nani? Itakwenda kwa DP World. Wakipata faida, huwezi ukaitoza kodi, hakuna chochote kinachozungumzia revenue sharing (mgawanyo wa mapato).
“Sawa wataongeza ufanisi, lakini nani atafaidika na ufanisi huo,” alihoji Profesa Shivji.

Alichokisema Profesa Shivji, kinafanana na kile kilichoelezwa na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba aliyekosoa suala hilo akisema kunahitajika kufanyiwa marekebisho vifungu vyenye utata.

Alipozungumza na televisheni ya Azam Juni 23, mwaka huu, Jaji Warioba alisema, “ni kweli mkataba ule una vipengele ambavyo vingezua wasiwasi, hili tusilikwepe, tuliangalie tuone tutakavyoweza kuboresha hiyo.”

“Nadhani tumechelewa katika utaratibu huu, kwa sababu tulikuwa na TICTS, pale tulijua mwisho wake umefika, tungejua tungefanya mapema, kwa sababu bandari ni muhimu sana.

“Haitoshi tu kusema haya ni makubaliano, hayo yanayozunguzwa yatakuja kwenye mikataba mingine, hapana. Waangalie hayo yapo kwenye mkataba huo, ambayo yanaleta wasiwasi watafute njia ya kuyaondoa,” alisema Jaji Warioba.

Mbali na wanasheria, mchumi na mwanasiasa aliyewahi kuwa mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Tibaijuka amekosoa mkataba huo akisema, una upungufu mwingi unaohitaji kufanyiwa kazi.

Juni 17 mwaka huu akizungumza na Mwananchi, Profesa Tibaijuka, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa UN Habitat, alisema,“mimi nimesoma mkataba kwa makini na nimeona kunahitajika marekebisho.

“Ukishakuwa na ‘foundation’ mbovu, hivi vingine vitakuja kukaa vizuri? Mkataba mdogo unakuwaje mzuri wakati mkataba mama ni mbovu,” alisema Profesa Tibaijuka.
Profesa Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi, naye ameuokosoa mkataba huo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Buguruni Dar es Salaam.

“Mkataba huu hautavunjwa, hautaondolewa, hautasitishwa kwa jambo lolote lile, hata mkivunja uhusiano wa kidiplomasia, mkataba huu itabidi uendelee.
“Najiuliza, huyu mwanasheria mkuu Serikali aliusoma mkataba huu? Au ndugu zetu wa Dubai wameuandika wakatuletea kila mtu akawa CCM kweli kweli?”
 

Viongozi wa dini

Miongoni mwa viongozi waliokosoa mkataba huo ni Katibu Mkuu wa Bara la Maaskofu wa Katoliki (TEC), Dk Charles Kitima, ambaye Juni 12 katika mkutano wa viongozi wa dini uliofanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Mbarawa, alionya kuhusu uwekezaji huo.

“Sisi viongozi wa dini tumeshiriki kuiambia Serikali itumie uungwana na wananchi watendewe utu, Loliondo haijafanyika mpaka sasa wananchi wanaendelea kuteseka.
“Wananchi hawajapenda kumpa mtu bandari zote, hawajafurahi, muone vitu ambavyo watu hawajapenda. Halafu watu tumeweka Sh1 trilioni, unampa mtu aendeshe, kwa nini sisi tusijenge uwezo wetu tukaendesha,” alihoji Dk Kitima.