Mkandarasi atakiwa kukamilisha miradi ya maji mwaka huu

Thursday August 04 2022
Ruwasa PIC

Mkurugenzi wa RUWASA, Clement Kivegalo akitoa maelekezo kwa wahandisi wa maji Rombo kukamilisha miradi ya maji kwa wakati. Picha Mussa Juma

By Mussa Juma

Rombo. Kampuni ya Best One Ltd inayotekeleza miradi ya maji katika wilaya ya Rombo mkoa wa Kilimanjaro, imetakiwa kukamilisha miradi ya kusambaza maji mwaka huu katika vijiji 44 itakayogharimu Sh5.3 bilioni mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Mhandisi Clement Kivegalo, ametoa agizo hilo leo Agosti 4, 2022 alipofika wilayani Rombo kukagua utekelezaji wa miradi hiyo

Mhandisi Kivegalo amesema miradi hiyo ambayo inatekelezwa kwa pamoja baina Ruwasa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Rombo, lazima ikamilike kwa wakati ili wananchi wa Rombo wapate huduma muhimu ya maji.

“Nimekuja Rombo na wataalam wangu kuona utekelezaji wa miradi ya maji ndani ya wilaya ya Rombo kufuatia wito uliotolewa na mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda baada ya kuona utekelezaji unasuasua,” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema baada kukagua miradi hiyo ukiwepo mradi wa Njiro II unaotekelezwa kwa fedha za Uviko-19 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, amefarijika kuona kuwa mradi huo umekamilika kwa kiasi kikubwa na tayari baadhi ya vijiji vimeanza kupata maji.

Amesema amebaini kuna changamoto katika utekelezaji wa miradi miwili mojawapo ikiwa ni ucheleweshaji wa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani, hivyo amekutana na wataalam wake na mkandarasi kujadiliana nao.

Advertisement

Awali, mkurugenzi wa kampuni ya Best one Ltd, Juma Mvamba aliahidi kukamilisha miradi hiyo kwa wakati, akaomba apatiwe malipo ya awali na mahitaji mengine kama msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ili kuharakisha Kazi.

“Tunaendelea kutekeleza mradi mmoja, mwingine tayari umekamilika na wananchi wanapata maji na Ruwasa wameahidi kutusaidia kukamilisha mradi kwa wakati,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji  Rombo, Martin Kinabo amesema kwa sasa miradi ambayo inatekelezwa katika wilaya hiyo ni miwili; mradi wa Njoro II ambao utagusa vijiji 15 na kusaidia wananchi 24,454 kwa gharama ya Sh3.4 bilioni.

Amesema mradi mwingine ni mradi wa Ona ambao utahusisha vijiji 29 na utagharimu Sh2.9 bilioni na miradi yote inaendelea vizuri.


Advertisement