Mke, mume washikiliwa kwa tuhuma za mauaji Mwanza

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng'anzi akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watano wakiwemo mke na mume kwa tuhuma za kuhusika kwenye mauaji ya watu watatu wa familia moja katika mtaa wa Mecco mkoani Mwanza.

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watano wakiwemo mke na mume kwa tuhuma za kuhusika kwenye mauaji ya watu watatu wa familia moja katika mtaa wa Mecco mkoani Mwanza.

Kwenye tukio hilo lililotokea Jumanne Januari 18, 2022 mfanyabiashara, Mary Charles (42), mtoto wake, Jenifa Fredy (22) na msaidizi wa kazi za ndani, Monica Jonas walipoteza maisha baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na shingoni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng’anzi amesema watuhumiwa wanadaiwa kutekeleza mauaji hayo Jumanne Januari 18 mwaka huu huku chanzo kikitajwa kuwa ni mgogoro wa kibiashara kati ya watu hao.

“Marehehemu (Mary Charles) alikuwa akiwatumia watuhumiwa fedha kwa ajili ya kwenda kumnunulia mazao mkoani Kigoma lakini mara ya mwisho baada ya kutumiwa fedha watuhumiwa hawakufanya hivyo, alipoanza kuwadai walishindwa kumlipa fedha hiyo wakaamua kumfanyia kitendo hicho,” amesema Ng’anzi.

Ng’anzi amewataja watuhumiwa hao kuwa ni mkazi wa Utemini kata ya Buhongwa jijini humo, Thomas Songay (26), mke wake, Hajir Thomas (23), Deoglas Malengwa (31), Emmanuel Lugaila (36) na Emmanuel Mathew, 19.

“Katika mahojiano yaliyofanywa watuhumiwa wamekiri kutenda tukio hilo. Aidha silaha aina ya panga lililotumika kutekeleza tukio hilo limepatikana na tumelipeleka kwenye ofisi ya mkemia mkuu kwa ajili ya kuoanisha vinasaba vya marehemu,” amesema Ng’anzi

Amesema watuhumiwa hao walikutwa na baadhi ya vielelezo vilivyotambuliwa na ndugu wa marehemu kuwa ni Jokofu moja aina ya Kyoto, Godoro, TV mbili aina ya Singsung nchi 18, Radio mbili na Jiko la kupikia vinavyodaiwa kuporwa na watuhumiwa baada ya kutekeleza mauaji hayo.

Pia amesema baada ya uchunguzi kufanyika, maofisa wa jeshi hilo walipata simu simu tatu za marehemu zikiwa zimefukiwa katika nyumba ya mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo.

“Watuhumiwa hawa watafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilisha upelelezi wa tukio hili kwa hatua zaidi za kisheria,” amesema Nganzi