Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mke wa bilionea Msuya aomba korti impe nafasi ya kuonana na Rais

Mke wa Bilionea Msuya, Miriam Mrita akiwa katika Chumba cha Mahakama ya Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo, akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Miriam, ambaye ni mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji namba 5 ya 2017 pamoja na Revocatus Muyela wanaodaiwa kumuua kwa kukusudia Aneth Msuya.

Dar es Salaam. Mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji, Miriam Mrita ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, impe nafasi ya kwenda kuonana na Rais John Magufuli akidai hatendewi haki.

Miriam, ambaye ni mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji namba 5 ya 2017 pamoja na Revocatus Muyela wanaodaiwa kumuua kwa kukusudia Aneth Msuya.

Aneth, dada wa bilionea Msuya aliuawa Mei 25, 2016 eneo la Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Awali, wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita aliieleza mahakama jana kuwa, kesi imepangwa kwa ajili ya kutajwa na jalada lake limeshatoka kwa mkurugenzi wa mashtaka (DPP) na kurudishwa kwa wakili kwa ajili ya kukamilisha maelekezo aliyopewa.

Baada ya maelezo hayo, Miriam alinyoosha mkono na hakimu mkazi mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba alimpa nafasi ya kuzungumza.

“Mheshimiwa hakimu, ni mwaka wa pili sasa nipo mahabusu na upelelezi haujakamilika. Juni 4, niliomba iundwe tume huru kuchunguza kesi hii. Kutokana na hali hii, naiomba mahakama inipe nafasi niweze kuonana na Rais John Magufuli au Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwanamke mwenzangu ili niweze kueleza matatizo niliyonayo, kwa sababu naona sitendewi haki katika kesi yangu,” alidai Miriam.

Alisema anaona haki yake ya msingi inacheleweshwa, hivyo yupo tayari kuongea sehemu yoyote endapo atapewa nafasi.

Hakimu Simba alipomuuliza kesi yake inacheleweshwa na nani, mshitakiwa alijibu kuwa inacheleweshwa na Mahakama kwa kuwa upelelezi umechelewa na kuna kitu kikubwa kimejificha nyuma ya kesi hiyo.

Hakimu Simba alimpa nafasi wakili wa Serikali kujibu hoja zilizowasilishwa na mshtakiwa, ndipo Mwita alipodai Mahakama haina mamlaka ya kuunda tume kuchunguza malalamiko yaliyowasilishwa na mshtakiwa. “Kuna njia nyingi za kuwasiliza malalamiko haya, kama kuandika barua na kumkabidhi wakili wake ambaye naye ataiwasilisha kwa mkuu wa gereza husika,” alisema Mwita.

Alisema njia nyingine ni mshtakiwa kuwaandikia barua Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambao wana jukumu la kusimamia na kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini. Hakimu Simba alisema jukumu la Mahakama ni kuhakikisha upelelezi wa kesi unakamilika ili hatua nyingine ziweze kufuatwa, hivyo kama mshtakiwa ana malalamiko anapaswa kuyawasilisha kwa barua kupitia wakili wake.

“Uwezo wa kuifuta kesi mimi sina kwa sababu ni kesi ambayo Mahakama hii haina uwezo wa kuisikiliza, hivyo nikushauri tu malalamiko yako uyawasilishe kwa barua kupitia wakili wako,” alisema hakimu.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hadi Julai 9, itakapotajwa na kuutaka upande wa mashtaka kuhakikisha unakamilisha maelekezo ya DPP kwa wakati ili kesi iendelee na hatua nyingine.