Mke wa Rais wa China awakumbuka wanawake, watoto Dar

Dar es Salaam. Shughuli ya kutunza afya ya watoto wa Tanzania imefanyika leo Mei 28, 2023 na ubalozi wa China katika Kituo cha Ijango Zaidia Orphanage Centre kilichopo Sinza D Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Hatua hii ilianzishwa na mke wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Profesa Peng Liyuan, pamoja na Shirika la Wanawake wa Marais wa Afrika na Maendeleo (OAFLAD) yenye kaulimbiu ya "Upe joto moyo wa mtoto."

Akizungumza katika hafla hiyo balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema, China na Afrika ni marafiki na mke wa Rais wa China, Peng Liyuan ameanzisha urafiki huo kwa nia ya kujali afya ya wanawake na watoto.

"Mke wa Rais Xi Jinping, ameanzisha urafiki wa kina na wake wa kwanza wa marais wa nchi za Afrika na kwa muda mrefu amejali kuhusu sababu za afya barani Afrika."

Amesema serkali ya China pia inashirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Makundi Maalumu, kutoa chanjo ya COVID-19 kwa wanawake na vijana wa Kitanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dorthy Gwajima alisema Serikali itakuwa karibu na vituo vinavyosaidia watoto na itaweka taratibu na mipango kwa taifa zima ili kuwezesha wanaotaka kusaidia vituo kupata namna nzuri.

"Tutaunga mkono juhudi za huduma ya kusaidia watoto kwakushirikia na wadau mbalimbali," amesema.

Pia alitoa shukrani kwa Serikali ya China na jopo la madaktari kwa kujali afya za watoto na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwenye kila hatua.

Mmiliki wa kituo hicho, Zaidia Nuru Hassan amesema, nia na madhumuni ya kituo hicho ni kuwasaidia watoto walioko katika mazingira magumu na kuwezesha kufikia malengo.

"Kituo kimetoa vipaji na taaluma mbali mbali wakiwemo madaktari, wahasibu, madereva pamoja na mafundi kwenye fani mbalimbali," amesema.

Zaidia alisema mpaka sasa kituo kimeweza kuwasaidia watoto zaidi ya 80 kuungana na familia zao kupitia kituo na ushirikiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Miongoni mwa vitu vilivyotolewa kituoni hapo ni kwa ajili ya watoto ni maziwa, dawa za kinywa pamoja na vifaa vya kuandikia pamoja na upimaji wa afya kwa watoto hao uliofanywa na madaktari kutoka nchini China.