Mkenda; hakuna uhaba wa sukari

Muktasari:

  • Serikali imesema hakuna uhaba wa sukari nchini huku ikiwaonya wafanyabiashara kuacha kupandisha bei ya sukari kiholela.

Arusha. Serikali imesema hakuna uhaba wa sukari nchini huku ikiwaonya wafanyabiashara  waache kupandisha bei ya bidhaa hiyo kiholela.

Onyo hilo limetolewa leo Juni 11 na Waziri wa Kilimo,Profesa Adolf Mkenda wakati alipokutana na wawekezaji wa kilimo kutoka nchi za Ulaya kwa lengo la kujadili namna bora ya kuendeleza kilimo bila vikwazo hapa nchini.

Profesa Mkenda amesema Serikali imeshaagiza sukari tani 50,000 wakati mahitaji ya nchi nzima ni tani 40,000 sawa na ongezeko la tani 10,000.

"Wanaopandisha sukari bei watambue hakuna uhaba wa sukari nchini, viwanda vyetu vimeshaanza kuzalisha na sukari itashuka bei, tutaangalia maeneo yote kama usambazaji unaenda vizuri katika maeneo yote ili isije pandishwa bei kiholela,"amesema Profesa Mkenda

"Tuliagiza sukari nyingi kuliko tuliyokuwa tukitarajia ,tulikuwa tukihitaji tani 40,000 na sisi tumeagiza tani 50,000 ziada ya tani 10,000 imeingia yote ,"amesema Profesa Mkenda.