MKONDO WA SHERIA: Wadau washauri mabadiliko ya dhamana kwa watuhumiwa

Dar es Salaam. Wakati kilio cha Katiba mpya kikiwa hakijatulia, kuna kilio kipya kinazidi kushika kasi; dhamana kwa watuhumiwa.

Wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu wanalitaka Bunge kutunga sheria itakayowaruhusu mahabusu kushiriki baadhi ya shughuli za kijamii kama vile misiba.

Wito huo umetolewa ikiwa ni siku mbili zimepita baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kushindwa kumpa ruhusa mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera kuaga mwili wa mama yake, Verdiana Mjwahuzi (80) ambaye alifariki dunia Jumanne iliyopita.

Kabendera, ambaye ameshtakiwa kwa tuhuma za kujihusisha na kundi la uhalifu na kutolipa kodi, yuko mahabusu kutokana na kosa jingine la tatu la kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilishindwa kumpa ruhusa kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo hadi kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa mujibu wa Hakimu Janeth Mtenga.

Uamuzi huo umeibua mjadala, ikiwa ni takriban miezi sita tangu Jaji Mkuu Ibrahim Juma adokeze matamanio yake ya kutaka kesi ziwe na dhamana ili kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani, ambao pia huchangiwa na upelelezi kuchelewa kumalizika.

Jaji Mkuu alisema hayo Julai 19 mwaka jana wakati wa sherehe za 60 kuanzia mwaka 1986 za kuwakubali na kuwasajili mawakili wapya, akitoa mfano wa nchi ya Kenya ambako hata mashtaka ya mauaji yana dhamana.

Pia, alishauri ofisi ya DPP kutokamata watuhumiwa kabla ya upelelezi kukamilika huku pia akipendekeza sheria iweke kikomo cha muda wa upelelezi ambacho kama hautakamilika, kesi ifutwe kabisa.

Lakini imeshawahi kutokea Zanzibar kwa mtuhumiwa kuruhusiwa kwenda kushiriki shughuli za kijamii.

“Mara nyingi mahakama huangalia mazingira na kuruhusu. Watu wengi tu wameachiwa, lakini si kwamba sheria imetamka hivyo,” alisema rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Awadh Said.

“Baba yake Juma Haji Duni alifariki akiwa ndani (mahabusu), lakini alitolewa akaenda akazika. Baadaye akafa mama yake, pia akatolewa na akaenda kuzika.

Said, aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, alisema wakati huo Haji Duni alikuwa ni mahabusu na kwamba mwanasiasa huyo mkongwe hajawahi kuhukumiwa kifungo.

“Awali alikuwa katika kesi ya uhaini, baadaye alipoingia Rais Amani Karume, wale wakatolewa,” alisema.

“Halafu walipofanya maandamano mwaka 2001 akatiwa ndani tena, wakati huo akafa mama yake naye akaenda kumzika. Akishatoka makaburini anakwenda rumande.”

Hali ilivyo nchini

Lakini hadi sasa hakuna sheria inayoruhusu wala kukataza mahabusu kuruhusiwa kushiriki shughuli za kijamii, jambo ambalo wanasheria na wanaharakati wanaona kuna umuhimu wa suala hilo kuwekwa kisheria au kanuni ambazo zitasimamia jambo hilo.

“Mahabusu ni watu ambao bado hawajakutwa na hatia, hivyo wana haki zao ambazo zinatakiwa kulindwa kwa utaratibu wa kisheria,” alisema mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC), Onesmo Olengurumwa.

Alisema kuna haja kwa Bunge kutengeneza sheria ambayo itatoa nafasi kwa mahabusu kushiriki masuala ya kijamii.

Alisema kuna umuhimu wa kuwa na sheria au kanuni kuwawezesha mahabusu kushiriki shughuli za kijamii na kwamba jambo hilo linafanyika sehemu nyingine duniani.

Wakili na mkurugenzi wa utetezi na uboreshaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe alisema kwa kuwa hakuna sheria inayokataza, jambo hilo lingeweza kufanyika kwa utaratibu maalumu.

Hata hivyo, alisema kuna haja ya kuliweka jambo hilo kisheria ili kutoa haki.

Kwa upande wake, mwanasheria Felix Kibodya alisema Serikali inapaswa kuzingatia mambo muhimu kama hilo ili kulinda haki za mtu ambaye anakuwa anashikiliwa kwa tuhuma.

“Wakati mwingine si lazima kuwe na sheria, bali hata kanuni za Magereza au mahabusu zinaweza kufanya kazi vizuri katika hili,” alisema mwanasheria huyo.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Anna Henga alitaka mifumo kutambua haki ya mahabusu kushiriki shughuli za kijamii ili dhana “mtu hana hatia mpaka ithibitishwe na mahakama” iweze kutimia.

“Suala la msiba ni zito sana, labda kama halijakupata. Kwa hiyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na sheria hiyo na ikumbukwe kwamba hawa watu ni mahabusu, bado hawajakutwa na hatia, ifike mahali mifumo ya haki jinai itambue haki zao,” alisema Anna.

Lakini mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga alisema wakati mwafaka bado.

Alisemna kwa sasa vyombo vya dola havijakaa sawa, akihoji itakuwaje iwapo mtuhumiwa akitoroka au akiuawa wakati akihudhuria shughuli za kijamii.

“Kama Serikali (inapata shida) kuwalinda mahakamani tu, itaweza kuwalinda hao watakaokuwa kwenye hizo shughuli?”

Wasemacho wabunge

Kuhusu suala la Bunge kutunga sheria hiyo, mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bungala maarufu ‘Bwege’, alisema ni jambo zuri lakini mpaka Serikali iwe na utashi.

“Mchakato wa kutunga sheria unaanzia serikalini. Wao ndiyo wanatengeneza miswada na kuileta bungeni, kwa hiyo wanaharakati walipigie kelele hili jambo mpaka kieleweke. Likija bungeni nasi tunapitisha,” alisema.

Naye mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika aliitaka Serikali kurekebisha sheria za Magereza ili kuwawezesha watuhumiwa kuruhusiwa kuhudhuria misiba.

“Haiwezekani kwa jambo zito mtu ni mahabusu si mfungwa ni mtuhumiwa tu kunyimwa fursa ya kutoka mahabusu, hata kama ni kwa ulinzi basi kama ilivyo kwa mahabusu wanaotoka gerezani wanapelekwa hospitalini kuhudumiwa,” alisema Mnyika ambaye pia ni katibu mkuu wa Chadema.

“Kwa jambo zito la msiba Erick kuzuiwa kuna kumwona mama yake ni jambo linaloumiza,” alisema akiishauri Serikali iwasilishe muswada wa kurekebisha sheria.

“Msiba huu wa Mama Erick iwe ni fundisho kwa Taifa kuwawezesha mahabusu wakipata majonzi, wawape fursa kuwapa pole wapendwa wao.”

Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya alisema sheria hiyo itakuwa na manufaa kwa jamii kwa sababu itafungua milango ya haki kwa wananchi kama ambavyo wamekuwa wakiipigania kila siku.

“Tukiletewa tu muswada wa sheria hiyo, wabunge tunaopenda haki tutaupitisha kwa sababu una nia njema ya kuwasaidia wenzetu wanaokuwa mahabusu na kukosa kushiriki mambo ya kijamii,” alisema Sakaya ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa CUF- Bara.