Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC ateuliwa kuwa Mwenyekiti mpya TBA

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi

Muktasari:

Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) kimemteua Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi kuwa Mwenyekiti wa chama hicho kwa kipindi cha miaka miwili, kuanzia Januari 2023.

Dar es Salaam. Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) kimemteua Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi kuwa Mwenyekiti wa chama hicho kwa kipindi cha miaka miwili, kuanzia Januari 2023.

Sabi anaweza kuongezewa kipindi kingine baada ya kukamilika kwa kipindi hicho kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho mapema leo.

Sabi alichaguliwa na wanachama wa TBA katika Mkutano wao Mkuu wa 10 wa Mwaka (AGM) uliofanyika Dar es Salaam Desemba 19, 2022 ambapo anachukua nafasi ya Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji - Benki ya CRDB, ambaye amekamilisha vipindi vyake viwili mwezi huu.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Citibank Tanzania, Geoffrey Mchangila alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho.

Akizungumzia uteuzi huo, Sabi alisema, “Ni heshima kwangu kuwa mwenyekiti wa chama hiki muhimu. Benki zina jukumu maalum katika maendeleo shirikishi ya uchumi wa nchi yetu. Natarajia kufanya kazi na wanachama wote ili kujenga thamani yenye tija kwa wadau wote,” alisema.

Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) kilianzishwa mwaka 1995 kama chama kabla ya kuwa kampuni yenye ukomo wa dhamana ya wanachama mwaka 2012. Ndiyo chombo kikuu cha utetezi wa sera kwa wanachama wake kwa lengo la kuweka sauti ya pamoja na mazingira mazuri ya maendeleo ya kiuchumi na kukuza ujuzi wa kifedha na ushirikishwaji. Kwa sasa, TBA ina jumla ya wanachama hai 42.

Aidha, mkutano huo pia uliidhinisha mkakati mpya wa miaka mitano (2023-2028) ambao unaweka Dira, Dhamira, na chaguzi za kimkakati zinazozingatia Utetezi, Utafiti na Uchanganuzi, Mawasiliano na ushirikiano na washirika wa kimkakati, pamoja na kukuza uwezo na taaluma kwa nia ya kuchangia ukuaji wa Sekta ya Mabenki na kuongoza ustawi wa kijamii na kiuchumi.

Mbali na uteuzi huu wa juu, Mkutano huo pia ulichagua wajumbe wapya tisa wa Baraza la Uongozi, ambao watakuwa na jukumu la uangalizi na maamuzi ya kisera kuhusu shughuli na mwelekeo wa TBA. Wajumbe hao waliochaguliwa ni Bi. Ruth Zaipuna, Ofisa Mtendaji Mkuu - NMB Bank Plc; Dk Salim Muhsin, Mkurugenzi Mtendaji - Benki ya PBZ; na Isabela Maganga, Mkurugenzi Mtendaji -Equity Bank (T);

Wengine ni Jaffari Matundu, Ofisa Mtendaji Mkuu - EXIM Bank; Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji na MD - CRDB Bank Plc.; Kevin Wingfield, Mkurugenzi Mtendaji- Benki ya Stanbic; Abdi Mohamed, Mkurugenzi Mtendaji na MD-Absa Bank(T); Herman Kasekende, Mkurugenzi Mtendaji na MD - Standard Chartered; na Edward Talawa, Mkurugenzi Mtendaji - FINCA Tanzania.