Mkurugenzi wa shule akamatwa akituhumiwa kupiga, kujeruhi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi akionyesha baadhi ya dawa na vifaa vilivyokuwa vikitumika kutengenezea fedha bandia na watuhumiwa.
Muktasari:
- Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia Mkurugenzi wa Shule ya Sun Academy Schools, Nguvu Chengula (50) kwa tuhuma za kumpiga na kujeruhi mzazi wa mwanafunzi kwa kutumia kitako cha bastola baada ya mzazi huyo kufika shuleni hapo kuomba uhamisho wa mtoto wake.
Iringa. Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia Mkurugenzi wa Shule ya Sun Academy Schools, Nguvu Chengula (50) kwa tuhuma za kumpiga na kujeruhi mzazi wa mwanafunzi kwa kutumia kitako cha bastola baada ya mzazi huyo kufika shuleni hapo kuomba uhamisho wa mtoto wake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Mae 17, 2022 Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Allan Bukumbi amesema tukio hilo limetolea jana maeneo ya shule hiyo mtaa wa Mawelewele Kata ya Mwangata Manispaa ya Iringa.
Bukumbi amesema kuwa mtuhumiwa Chengula akiwa ofisini kwake alimshambulia Alifa Mkwawa maarufu kama Wilbert ambaye alifika kuomba uhamisho wa mtoto wake.
"Mlalamikaji alijeruhiwa wakati alipokuwa ameenda na mwenza wake Prisca Kimaro kwa nia ya kuomba uhamisho wa mtoto wao Leonard Wilbert Mkwawa (6) mwanafunzi wa darasa la pilo" amesema
Kamanda Bukumbi amesema chanzo cha tukio hilo ni mzozo uliotokana na mtuhumiwa kugoma kutoa uhamisho wa mwanafunzi wa mlalamikaji.
Kamanda mtuhumiwa huyo amekamatwa na kielelezo hicho ambacho kimehifadhiwa kituoni upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Wakati huohuo, Kamanda Bukumbi amesema kuwa Jeshi hilo limekamata watu watatu wakiwa na mabunda ya karatasi nyeusi zilizokatwa na kupangwa mfano wa pesa za Tanzania ambapo walipanga kufanyia utapeli.
Amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa juzi usiku kwenye nyumba ya kulala wageni.
“Baada ya kuwakamata watuhumiwa tuliwafanyia mahojiano wamekiri kuwa wamefika Iringa wakitokea Dar es salaam kwa lengo la kufanya utapeli kwa watu jambo ambalo halikufanikiwa baada ya kukamatwa na polisi, kati ya watuhumiwa hao mmoja amekuwa akijifanya mganga wa kienyeji na kusafisha nyota ya bahati’’ amesema Kamanda Bukumbi