Mkutano wa demokrasia: Suala la Katiba mpya bado moto

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (kulia), akiwa na wadau wengine kwenye mkutano  wa kitaifa wa kutafakari na kujenga uelewa wa pamoja juu ya sheria za uchaguzi zilizopitishwa kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Muktasari:

  • Mkutano wa siku mbili wa wadau wa demokrasia na vyama vya siasa,  umependekeza masuala mbalimbali ikiwemo kufanya mabadiliko madogo ya kikatiba sambamba na kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.

Dar es Salaam. Kilio cha Katiba bado hakijapoa. Mkutano wa siku mbili wa wadau wa demokrasia na vyama vya siasa,  umependekeza masuala mbalimbali ikiwemo kufanya mabadiliko madogo ya kikatiba sambamba na kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.

Mapendekezo hayo yalisomwa jana na Buruani Mshale kutoka taasisi ya Twaweza katika mkutano wa kitaifa wa kutafakari na kujenga uelewa wa pamoja juu ya sheria za uchaguzi zilizopitishwa kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali  wa zamani, Andrew Chenge, Mbunge wa Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Bara), Issihaka Mchinjita, Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi (Bara), Joseph Selasini.

Wengine ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, pamoja na wabunge wa zamani Hawa Ghasia (CCM), Suzan Kiwanga (Chadema), Maftah Nachuma (CUF).

Akiwasilisha maazimio ya mkutano huo, Mshale amesema mabadiliko hayo madogo ya Katiba yatawezesha na kuruhusu yale mapendekezo katika sheria za uchaguzi ambayo hayakuzingatiwa.

Mshale amesema kuna hoja zilizotolewa kuwa mapendekezo hayo yanakinzana au kukiuka vifungu mbalimbali vya Katiba.

“Kunahitajika kufanya mabadiliko madogo ya Katiba ili kuongeza wigo wa maoni na maboresho yanayohitaji kufanyika, wakati mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ukiendelea,” amesema.

Mshale amesema wadau hao wameazimia kuwa vyama vya siasa viendeleze falsafa ya 4R ya Rais Samia katika utekelezaji wa majukumu yao.

Tangu aingie madarakani Machi 19, mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa na falsafa ya R nne anazozitumia katika utawala wake.

R hizo ni  Reconciliation- Maridhiano, Reforms- Mabadiliko,  Resilience- Ustahmilivu na Rebuliding- Kujenga upya, akiwataka watendaji wake kuzitekeleza katika majukumu yao ili kujenga Taifa lenye umoja.

Mbali na hilo, Mshale amesema wadau hao wamekubaliana kuendelea kutumia vema utashi na uhuru wa kisiasa unaoendelea kuchipukia nchini ikiwemo kufanya makongamano mbalimbali.

“Tunafahamu tulipotoka na tunafahamu tulipo, kufanya makongamano kama haya kwa kipindi cha nyuma ilikuwa ngumu. Tuna hii fursa tuendelee kuitumia. Wakati wa kuitumia fursa hii tusiumie sana wakati wengine wakiendelea kukosoa.

“Ni haki yao wanakosoa, wanaolaumu na kushauri lengo ni kujenga, wale wanaojihisi kukosolewa watambue kuwa wana wajibu kuwa wasikivu na kutotumia nguvu kunyamazisha mawazo mbadala. Tuendelee kusikilizana,  tutumie vyema utashi wa kisiasa,” amesema.

Mshale amesema jambo jingine ni kuendeleza utamaduni wa majadiliano na uelewa wa pamoja, akisema imeonekana kumekuwa na kiu kubwa ya kuwepo kwa midahalo na kila mmoja anaonekana kuwa na  kiu ya kuzungumza.

“Jambo la muhimu utamaduni huu uendelee na kuwekewa utaratibu wa kisheria, katika mapendekezo ya maboresho ya sheria ya uchaguzi wa wabunge, madiwani na Rais,  lazima kuwepo kwa midahalo hivyo tunaendelea kukumbusha kwa sababu limeibuka hapa, kwa sababu ni utamaduni mzuri wa kujenga demokrasia yetu,” amesema.

Mshale amesema wamekubaliana kuongeza na kuimarisha ushiriki wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, wakisema Serikali na wadau wa vyama vya siasa wana jukumu la kuweka mipango na mikakati madhubuti ya kampeni zinazolenga kuimarisha ushiriki wa makundi hayo.

“Imesisitizwa vijana ndio wengi katika jamii yetu na wanaendelea kuwa sehemu ya Taifa letu, hivyo  kuwe na mikakati ya makusudi ya kuwaandaa na kuwawezesha vijana kutimiza wajibu wao vema ili kupunguza presha inayojitokeza tunapokuwa katika midahalo ya pamoja.

“Wengine wamesisitiza katika kanuni na taratibu za ndani ya vyama, kuwepo kwa mikakati madhubuti ya kuwezesha mambo haya,” amesema.

Mshale amesema jambo jingine ni kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi zinazojitosheleza kwa wakati, zinaohusiana na michakato ya kidemokrasia kwa umma.

Alisema bila uwepo wa uwazi wa upatikanaji wa taarifa, Taifa haliwezi, kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa demokrasia.

“Tumesikia mifano jana (juzi) ikitolewa kwa kuna taratibu zinaendelea ambazo umma hazifahamu. Leo pia tumesikia tangazo la kukusanya maoni ya wadau kuhusu kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini wadau hawajui. Taarifa kama hizi zinapaswa kutoka mapema ili wadau watoe maoni yao vema,”

Amesema wamesisitiza uchaguzi wa serikali za mitaa kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).

Akichangia suala hilo, Wakili Jebra Kambole amesema,  Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia uchaguzi huo inawezekana, akisema ni muhimu kwa hapa tulipofikia kuliko Tamisemi kubaki na jukumu hilo.

“Tamisemi bado ina changamoto nyingi kusimamia uchaguzi huu, kuliko Tume ingawa yenyewe ina shida lakini haijafikia  kama Tamisemi, wakiamua Serikali jambo hili linawezekana,” alisema Kambole.

Akiendelea kutoa maazimio hayo, Mshale amesema kunahitajika matumizi ya teknolojia, katika sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.


Chenge na kanuni

Katika hatua nyingine, Chenge ambaye ni mbunge wa zamani wa Bariadi mkoani Simiyu akichangia kwenye mjadala huo kabla ya kufikia hatua ya maazimio,  amesema sheria mbili za uchaguzi wa serikali za mitaa na mamlaka za miji na wilaya,  zinampa mamlaka waziri wa Tamisemi kutengeneza kanuni.

“Hizi ni sheria za nchi, tunaweza tusizipende au kuzipenda lakini ni sheria za nchi, ningependa tuanzie hapa, nchi nzima wananchi wana shauku ya kutaka kuona uchaguzi wa mwaka huu wa serikali za mitaa,  unakuwa mzuri kuliko wa mwaka 2019, nilitegemea nguvu nyingi iwekwe katika kuweka utaratibu shirikishi wa kanuni.

“Kinachowasumbua wengi ni yale madhila ya mwaka 2019, ningeshauri taasisi kama hii (TCD) inayofahamika kwenye siasa,  isimamie hili kwamba zile kanuni kwa mwaka huu ziwe shirikishi,” amesema Chenge.

Uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2019,  ulilalamikiwa na  vyama vyua upinzani,  kutokana na kasoro zilizojitokeza ikiwemo wagombea wao kuenguliwa kwa sababu mbalimbali hali iliyosababisha CCM kuibuka kidedea katika maeneo mbalimbali.


Tamisemi yanadi kanuni

Hata hivyo,  juzi, Waziri wa Nchi, Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alilieleza Mwananchi juu ya uhitaji wa wadau wa kanuni hizo,  akisema kanuni hizo zitakuwa shirikishi na zinakwenda ka ratiba za uchaguzi.

“Tamisemi hatutakurupuka, kanuni hizi ni za wadau wenyewe, wao wenyewe ndio wataziandaa na sisi ni wasimamizi tu, kama ambavyo Rais amekuwa akisisitiza anataka ushirikishwaji na sisi tutafanya hivyo,” amesema Mchengerwa.

Katika mkutano huo huo, juzi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amehoji ukimya wa kutotolewa kwa kanuni za uchaguzi huo hadi sasa ikiwa umebaki muda mchache.

Amesema wanakwenda kwenye mchakato huo miezi michache ijayo lakini kanuni za uchaguzi huo.

Kwa upande wake, Selasini ambaye ni mbunge wa zamani wa Rombo mkoani Kilimanjaro aliungana na Chenge akisema mchakato wa mwaka 2019 mgombea alienguliwa kwa kosa la kutoandika jina lake vizuri, hata kama alikuwa akifahamika.

“Mtu anaenguliwa kwa kosa la kutoandika anuani yake, lakini anajulikana, sasa vitu kama hivi vinaweza kurekebishwa kwenye kanuni. Kanuni inaweza kusema hivi kitu cha kuangalia ni sifa za msingi za kikatiba ikiwemo umri, raia, kusoma na kuandika, au usiwe  unadaiwa kodi,” amesema Selasini.

Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake ya ACT-Wazalendo, Janeth Rithe,  ameshauri kuwepo kwa vitambulisho maalumu kwa ajili ya kupigia kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa,  ili kuondoa changamoto ya watu kupigiana kura kama ilivyotokea katika chaguzi zilizopita.

“Kumekuwa na tabia ya watu kupigiana kura katika mchakato huu, sasa ili kuondokana na tatizo hili kuwepo na vitambulisho maalumu,” amesema Rithe.

Wakili wa Chadema, Jonathan Mndeme amesema muda wa kampeni wa siku 14 za uchaguzi wa serikali za mitaa hautoshelezi, akishauri Serikali kuongeza ili kuwapa fursa wagombea kujinadi. “Mamlaka ya watu katika serikali za mitaa ni makubwa sana, siku 14 hazitoshelezi, wakati uchaguzi mkuu siku 60. Jukumu la mamlaka ya serikali za mitaa kwa wananchi tumelipuuza,” amesema Mndeme.