Mkuu wa mkoa ashangaa kuulizwa  ‘sangoma wake’

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza na viongozi wa sekreatieti ya mkoa huo leo Jumanne Aprili 9, 2024. Mtanda amefanya kikao hicho kuwaeleza vipaumbele vyake na kutoa maagizo kwao akiwataka kutatua changamoto za wananchi mkoani humo. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Said Mtanda kabla ya kuteuliwa Machi 31, 2024, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, amewahi kuwa Mbunge wa Mchinga mkoani Lindi (CCM) kati ya mwaka 2010 hadi 2020, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Arusha na Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Mwanza. “Mtu mmoja alinipigia simu, bwana nyota yako inazidi kung’ara, niambie mganga wako ni nani, nikaona huyu haelewi mambo.”

Ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akielezea alivyopigiwa simu na mtu (bila kumtaja) akitaka kujua siri ya kuendelea kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mtanda ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Mchinga mkoani Lindi (CCM) kati ya mwaka 2010 hadi 2020, amewahi kuwa mkuu wa wilaya za Nkasi na Arusha na baadaye mkuu wa Mkoa wa Mara kabla ya Machi 31, 2024, Rais Samia hajamteua kuwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza leo Jumanne Aprili 9, 2024, katika mkutano na watumishi wa Sekretarieti ya mkoa huo , Mtanda amesema anaamini miongoni mwa sababu zinazosababisha aendelee kuaminiwa ni pamoja na kuwajibika kwa kutekeleza majukumu yake.

Huku akikemea wanaoamini kwa waganga wa kienyeji ili wafanikiwe, Mtanda amesema kuwatumikia wananchi kwa haki na usawa, kuamini katika matokeo na kupingana na rushwa, ni miongoni mwa sababu zinazoweza kumfanya mtumishi yeyote aendelee kuaminiwa na wateuzi.

“Watendaji wa Serikali tusifanye kazi kwa sababu tunalipwa mishahara. Utumishi huu ukifanya mambo mazuri unajiangalia pia kesho yako mbele ya Mungu itakuwaje.

“Mtu mmoja alinipigia simu, ‘bwana nyota yako inazidi kung’ara, niambie mganga wako ni nani’, nikaona huyu haelewi mambo.”

“Nikwamwambia hata ukienda kwa mganga akishapiga ramli zake mwisho anasema ‘[kwa kadri ya uwezo wangu nimemaliza, yaliyobaki tumuachie Mungu’, sasa kwa nini nisiende kwa Mungu. Ukiishi kwa imani, ukatenda haki, ukasaidia watu, ukatoa sadaka, Mungu atakubariki na kukuinua,” amesema Mtanda.

Amewataka wakurugenzi na watendaji wa Serikali mkoani humo kuepuka kutengeneza mazingira ya rushwa wanapowahudumia wananchi na amekemea vikali watendaji wanaokwamisha jitihada za Serikali kufikisha huduma kwa wananchi, kwa masilahi yao binafsi.

“Sisi ni watumishi wa wananchi wa Mwanza, lazima tuwatendee haki, mwananchi akifika ofisi ya umma ana haki ya kupokelewa, kusikilizwa na kuhudumiwa bila masharti, sasa ukiona mtendaji wa umma anaanza njoo leo, au kesho, sijui Sekretari anaumwa huyo anatengeneza mazingira ya rushwa,” amesema.

Katika kuhakikisha huduma kwa wananchi zinatolewa, Mtanda amewaagiza Ma - DED kufufua magari yote yaliyoegeshwa kwa uchakavu na kufanya kazi kwa ukaribu na ofisi za wakuu wa wilaya ili kutatua kero za wananchi.

Pia ameagiza lianzishww dawati maalumu la kero za wananchi mkoani humo.

Huku akidokeza kugomea mapokezi ya makubwa mkoani humo, Mtanda amesema anaamini zaidi kwenye matokeo, ambayo amesema yataonekana kwa ushirikiano na kuelezana ukweli, baina ya watumishi wa Serikali mkoani humo.

“Katibu Tawala (RAS) aliniambia sasa mapokezi yako yaweje maana sasa hivi kuna mitindo mingi ya watu kupokeana, nikamwambia mapokezi yangu ni kimya kimya kwa sababu ninaamini jiwe linalodharauliwa na waashi ndilo jiwe la pembeni. Mimi ni mtu wa kawaida ila nimepata bahati ya kuaminiwa na kuwekwa mbele, naamini kwamba ajishushaye hukwezwa na ajikwezaye hushushwa,” amesema.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana amewataka watendaji kupunguza maneno badala yake watimize wajibu wao kwa kuwatumikia wananchi kwa kutoa huduma bora, haki, uwajibikaji na nidhamu ili kuwaletea maendeleo.

“Watumishi wa umma tuna dhamana ya kuwatumikia wananchi na kumsaidia Rais Samia. RC ameeleza kwamba tuna dhamana kubwa, hivyo tukatekele wajibu wetu,” amesema Elikana.

Akizungumza kwa niaba ya wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba mbali na kupokea maelekezo hayo, amesema wanaamini uteuzi wa Mtanda haukuwa bahati mbaya badala yake ni nafasi kwake kuonyesha uwezo wake mkoani humo.

“Umetupatia dira na mwelekeo wa namna gani tunatakiwa kuenenda huko ofisini, mambo gani huyapendi, na mambo gani unataka tukayafanyie kazi. Umetuelekeza kuwasikiliza na kuwatendea haki wananchi na watendaji tunaowaongoza na kusimamia ukusanyaji wa mapato, tutayatekeleza,” amesema Kibamba.


Matarajio ya wananchi

Wakati Mtanda akisema hayo, wakazi wa mkoa huo wanatarajia kumuona akiboresha makusanyo ya mapato, kutatua changamoto ya machinga, ujenzi holela, Uuvuvi haramu, viwanda vya samaki kurejea kufanya kazi, ubovu wa miundombinu na kuimarisha uchumi wa wananchi.

“Bado hatujawa na mfumo mzuri wa wafanyabiashara wadogo ndio maana ikikaribia sikukuu wanarudi mjini na masoko yaliyopo nje hayana mifumo mizuri, kwa hiyo anatakiwa kutengeneza mifumo mizuri ya ufanyaji biashara lakini pia miundombinu ya barabara ni mibovu hili nalo lipo kwake," alisema Godfrey Misana, katibu mwenezi mstaafu wa Chadema Wilaya ya Nyamagana.

Mwenyekiti wa Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Saidi Tembo alisema wanatarajia Mtanda atatue changamoto ya wamachinga kukosa maeneo ya kufanyia biashara yenye mzunguko mkubwa wa watu.

"Yapo mambo ambayo tutafikisha kwenye meza yake jambo la kwanza wafanyabiashara wadogo hatuna maeneo ambayo yapo karibu na mkusanyiko wa watu, pia Mkuu wa Mkoa atukubalie ombi la baadhi ya barabara kufungwa nyakati za usiku au mara moja kwa wiki kuruhusu kufanya biashara mpaka usiku," amesema Tembo.

Waziri kivuli wa Nishati na Katibu Mwenezi wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Filbert Macheyeki amesema shauku kubwa ya wananchi ni kuona changamoto ya maji, ukosefu wa ajira, ukosefu wa soko la uhakika la uvuvi na changamoto ya uchumi wa mwananchi una imarishwa.

“Sisi kama wanasiasa tunaona uteuzi huu ni maandalizi kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu lakini mambo ambayo yanamsubiri ni pamoja na changamoto ya uhaba wa maji kwa wana Mwanza ukizingatia tupo karibu na ziwa lakini wanaopata maji ni wachache, jambo lingine ni changamoto ya ajira, ukosefu wa soko la uhakika la wavuvi na pia anatakiwa kuimarisha uchumi wa wanachi wa Mwanza,” amesema.

Mdau wa uvuvi nchini, Bakari Kadabi amesema wavuvi wanahitaji mkuu huyo wa mkoa ashughulikie changamoto ya uvuvi haramu na kufufua viwanda vya uvuvi ambavyo havifanyi kazi kutokana na uhaba wa samaki.

Mkazi wa Kata ya Bulyaheke katika Kisiwa cha Kasalazi, Rafael Bituro alisema jitihada za haraka zinatakiwa ili kukabiliana na uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria na kuoka mazalia ya samaki.

“Changamoto nyingine ni kusuasua kwa ukamilishaji wa kivuko kipya cha Kome hapa Sengerema ambacho kilikuwa kikamilike Aprili lakini hakijakamilika ili kuwaondolea adha wananchi,” amesema.